Viongozi 200 wa dini Pwani wakusanyika kumuombea Rais Samia

*RC Kunenge aonesha kufarijika kwa hatua hiyo, awapongeza na kuwapa rai

NA ROTARY HAULE

ZAIDI ya viongozi wa dini 200 kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Pwani wamekusanyika leo katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge kwa ajili ya kuzindua na kufanya kongamano maalum la kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Mbali na kumuombea Rais Samia, lakini pia viongozi hao wa dini wameelekeza maombi yao katika kuwaombea viongozi wengine wa Kitaifa,Mkuu wa Mkoa wa Pwani pamoja na Hayati Dkt.John Magufuli aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano.

Kongamano hilo limefanyika ikiwa ni mawazo yaliyotokana na Kamati ya Amani ya Mkoa wa Pwani katika kikao chao cha pamoja kilichofanyika mwishoni mwa mwezi Februari kwa kumshirikikisha Mkuu wa Mkoa, Abubakar Kunenge,Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Mhandisi Mwanasha Tumbo pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama.

Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani Mkoa wa Pwani ambaye ni Shehe Mkuu wa mkoa Hamis Mtupa amesema kuwa, lengo la kufanya kongamano hilo ni kumuombea Rais Samia katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wake.
Mtupa amesema, Rais Samia amefanya kazi kubwa katika kipindi cha mwaka mmoja na viongozi wa dini wameona jinsi nchi ilivyofunguka kwa kupata mafanikio mbalimbali hivyo kwa kuona hilo viongozi wa dini waliguswa na hivyo kuamua kuzindua kongamano hilo.

Amesema kuwa, malengo mengine ya kongamano hilo ni kukemea vitendo ya mauaji na unyanyasaji wa kijinsia,kukemea mauaji pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa linalotarajia kufanyika mwaka huu,suala la chanjo na Anwani za Makazi.

Aidha,Mtupa amesema baada ya kuzindua kongamano hilo utaratibu utakaofuata ni kwamba kila dhehebu litaendelea kufanya maombi hayo katika makanisa yao na misikiti yao katika kipindi chote cha mwezi huu.

"Sisi viongozi wa dini tumekusanyika hapa kutoka Wilaya mbalimbali kwa ajili ya kuzindua kongamano la Amani kwa ajili ya kumuombea Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha mwaka mmoja tangu aingie madarakani na hakika amefanyakazi kubwa sana,"amesema Mtupa.
Akizindua kongamano hilo leo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema kuwa, jambo lililofanywa na viongozi wa dini ni jambo kubwa lililoleta faraja ndani ya Mkoa wake.

Kunenge,amesema kuwa viongozi wa dini ni watu muhimu katika jamii na kitendo walichokifanya kimeleta taswira nzuri ya mshikamano na ushirikiano hasa katika kujenga amani na kuchochea maendeleo.

"Nawashukuru na kuwapongeza viongozi wa dini kwa kuanzisha jambo hili jema la kumuombea Rais wetu hakika hili jambo nzuri la kuigwa na Mikoa mingine ,Serikali itaendelea kushirikiana nanyi muda wowote,"amesema Kunenge

Kunenge, amewaomba viongozi hao wa dini kuhakikisha wanashiriki katika mabadiliko ya Kiuchumi kwa kuhamasisha vijana watumie fursa zilizopo kufanyakazi kwakuwa bila hivyo fursa hizo zitachukuliwa na watu wa mbali.
Kwa upande wake mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani Mkoa wa Pwani Padre Benno Kikudo kutoka Parokia ya Kibaha amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kukubali maombi yao ya kufanya kongamano hilo ndani ya Mkoa huo.

Kikudo amesema kuwa, Kamati ya Amani imefarijika jinsi ambavyo Mkuu wa Mkoa anavyotoa ushirikiano kwao na kwamba wataendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha Serikali inafikia malengo yake.
Amesema,suala la Sensa wamelichukua kwa uzito mkubwa na watakwenda kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi huku akiahidi Mkoa wa Pwani utaongoza kwa suala la Sensa.

Hata hivyo,Kikudo amesema kuwa Kauli Mbiu ya Kongamano hilo ni Amani,Utulivu, Ustawi wa Jamii,na Uchumi imara .

Post a Comment

0 Comments