WATALII HIFADHI YA MSITU WA PUGU KAZIMZUMBWI WASIFU SERIKALI YA AWAMU YA SITA ILIVYOBORESHA MAZINGIRA YAKE,WASEMA MAAJABU YA MSITU HUO NI MAKUBWA DUNIANI

NA ROTARY HAULE

BAADHI ya watalii katika Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi uliopo Kisarawe mkoani Pwani wamepongeza juhudi za Serikali ya Awamu Sita kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa namna ambavyo wameboresha msitu huo.
Wamesema kuwa Hifadhi ya Msitu wa Kazimzumbwi umekuwa na vivutio vingi na vizuri kiasi ambacho kinaleta ushawishi na hamasa kwa Watanzania na wageni kutoka nje ya Nchi kutembelea msitu huo kwa ajili ya kujionea mambo mbalimbali.

Mmoja wa watalii hao ambao alikutana na waandishi wa habari katika Hifadhi hiyo Marietha Kileo amesema kuwa, kazi iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan inapaswa kuungwa mkono.

Kileo amesema kuwa, Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi kwa sasa umekuwa na mvuto mkubwa kutokana na vivutio vyake pamoja na mazingira yake kuwa mazuri kiasi ambacho kinapelekea kila mtalii anayeingia kuwa balozi wa wenzake.
Kileo amesema, Msitu wa Kazimzumbwi ni moja ya Hifadhi ya kihistoria yenye pango maalum la mizimu linalojukana kwa jina la Pango la Mizimu ya Mavoga ambalo mtalii yeyote anaweza kuomba jambo lake na akafanikiwa.

"Nimefika kutalii katika Msitu huu wa Hifadhi ya Pugu Kazimzumbwi lakini nimejionea mambo makubwa mazuri ikiwemo Pango la Mizimu ,Panzi mwenye bendera ya Taifa na nimefika katika kilele cha mlima wenye urefu wa Kilomita mbili kutoka usawa wa bahari kinachoonyesha Mji mzima wa Dar Es Salaam,''amesema Kileo.
Mtalii Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi uliopo wilayani Kisarawe, Marietha Kileo akihojiwa na waandishi wa habari.

Aidha, Kileo amewashauri Watanzania kujenga tabia ya kutembelea Msitu huo ili waweze kujionea namna ambavyo msitu huo unavyoleta faraja kwa kuwa na vivutio vizuri visivyopatikana sehemu nyingine duniani.

Nae Alain Lihoteliter mtalii kutoka nchini Ufaransa akiambatana na mkewe Cecile Furet amesema kuwa, amefarijika kuingia katika Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi kwakuwa ameona vivutio vingi.

Amesema ,katika Msitu huo ameona bwawa la asili la Minaki (Minaki Dam),mnyama aina ya Komba,Pango la Mapopo pamoja na kuona mazingira mazuri yenye utulivu yanayovutia mtu kutalii na kujifunza vitu mbalimbali.

Mtalii huyo amesema kuwa, baada ya kutoka katika hifadhi hiyo atakwenda kuwa balozi mzuri kwa watu wa Ufaransa ili na wao waje kuona maajabu na vitu vyenye kuvutia vilivyopo ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi.
Mhifadhi Misitu wa Wilaya ya Kisarawe, Fred Ndandika kutoka TFS amesema miundombinu zaidi ya kilomita kumi katika hifadhi ya Pugu Kazimzumbwi inaendelea kufunguliwa ili kutoa fursa zaidi kwa watalii kuona vivutio vingi zaidi.

Ndandika amesema, watalii katika Hifadhi ya Msitu huo wameongezeka kutoka 500 mwaka 2019 hadi kufikia 13,000 katika kipindi cha mwaka 2021/2022 ambapo asilimia 70 ni watalii wa ndani.

Ofisa Misitu Mkuu kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki, Shaban Kiula amesema, TFS wanaendesha mpango wa Kayaki wakuhakikisha wanatunza na kuboresha miundombinu yote iliyopo katika Msitu huo.
Baadhi ya watalii wakiwa katika Pango la Mizimu ya Mavoga lililopo katika Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi.

Hata hivyo,Kiula amewataka Watanzania kujenga tabia ya kufanya utalii wa ndani badala ya kusubiri wageni kutoka nje ya nchi ambapo amesema utalii unasaidia mtanzania kujua umuhimu wa raslimali zilizopo nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news