Wizara yatoa mwezi mmoja kwa TEMESA kubadilika kiutendaji

NA MWANDISHI MAALUM

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Balozi Aisha Amour ametoa mwezi mmoja kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kubadilisha utendaji kazi wao na kuleta matokeo chanya katika kutekeleza majukumu yao.
Ametoa agizo hilo alipofanya ziara katika ofisi za wakala huo, pamoja na mambo mengine aliongea na watumishi pamoja na kukagua eneo la kivukoni na karakana ya Songoro iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam inayokifanyia ukarabati kivuko cha MV. KAZI.

Balozi Aisha amewataka TEMESA kusimamia nidhamu katika utendaji katika kitengo cha matengenezo ya magari, kwani ndiyo iliyobeba taswira ya wakala, hivyo wahakikishe magari yanayotengenezwa yanakidhi thamani ya fedha ili kuepuka malalamiko ya wateja.

"Hakikisheni mnajipanga upya kwenye ukaguzi wa vivuko ili kuepusha kupeleka vivuko vikiwa kwenye uharibifu mkubwa na kwa upande wa magari hakikisheni mnatumia vipuri vyenye ubora unaotakiwa," amesema Balozi Aisha.

Amesema, mwezi mmoja aliowapa wautumie katika kujipanga ili kuhakikisha gharama za kutengeneza magari zinapungua na kuendana na matengenezo wanayofanya na pia kuangalia upya rasilimali watu kama inakidhi mahitaji yao.

"Punguzeni kufanya kazi kwa mazoea na watumishi wanaoharibu taswira ya TEMESA wachukuliwe hatua,”amesema Balozi Aisha.

Aidha, amewapongeza kwa hatua ya haraka waliyochukua kupeleka kivuko cha MV.KAZI kwenye matengenezo ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea endapo wangechelewa kukifanyia ukarabati.

Pia amesema, Serikali inatarajia kutenga fedha za manunuzi ya kivuko kipya kitakachotoa huduma katika eneo la Magogoni na Kigamboni mkoani Dar es Salaam, ikiwa ni ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni mkakati wa serikali wa kuboresha huduma eneo la Kigamboni.

"Kivuko hicho kitakuwa na uwezo wa kubeba tani 500 sawa na abiria 2,000 na magari 60 na tayari fedha zimeshatengwa kwenye bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2022/23,"amesema Balozi Aisha.

Awali akitoa taarifa kwa katibu mkuu, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala alisema serikali imefanya maboresho ya ukataji tiketi kwa kusimika mfumo mpya wa kielekroniki (N-CARD) wa kusimamia mapato katika eneo hilo.

"Mfumo huo unaondoa mfumo wa zamani wa kutumia tiketi za karatasi na tayari tumeona mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupunguza msongamano wa abiria katika sehemu ya kukatia tiketi,"alisema Kilahala.

Aliongeza kuwa, abiria ambao wanatumia kivuko hicho kwa nadra wamewekewa utaratibu wa kadi za muda watakazozitumia wakati wa kuvuka katika eneo hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news