CRDB yafuturisha wateja na wadau Shinyanga, RC Mjema atoa wito

NA KADAMA MALUNDE

BENKI ya CRDB imewafuturisha wateja na wadau wa benki hiyo Mkoa wa Shinyanga ikiwa ni mwendelezo wa utamaduni wa benki kuungana na waumini wa dini ya Kiislamu wanaoishiriki Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Sophia Mjema (wa pili kulia) akichukua futari wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa wateja na wadau wa Benki ya CRDB Mkoa wa Shinyanga. (Picha na Malunde 1 blog).

Hafla ya futari iliyoandaliwa na Benki ya CRDB imefanyika Aprili 13,2022 katika ukumbi wa NSSF Mpya Mjini Shinyanga na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini ya Kiislamu, watoto yatima na wateja na wadau wa Benki ya CRDB ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema akizungumza wakati wa Hafla ya Futari iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa Wateja na Wadau wa Benki ya CRDB Mkoa wa Shinyanga.

Akizungumza kwenye hafla hiyo ya kufuturisha, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema ameishukuru Benki ya CRDB kwa kuandaa futari hiyo pamoja na kuendelea kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya jamii.

“Napenda kuushukuru Uongozi wa Benki ya CRDB kwa Iftari siku ya leo, Mwenyezi Mungu azidi kuwaongoza na kuangaza katika shughuli zenu. Niwapongeze Waislamu wote kwa kuendelea na funga katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani kwani funga hii ni faradhi kama ilivyoelezwa katika Kitabu Kitukufu cha Quran,”amesema Mjema.
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zuwena Omary akizungumza kwenye Hafla ya Futari iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa Wateja na Wadau wa Benki ya CRDB Mkoa wa Shinyanga.

“Benki ya CRDB inatoa huduma zinazokidhi mahitaji ya jamii ikiwemo huduma ya Al- Barakah Banking ambayo ni mahsusi kwa ajili ya waumini wa dini ya Kiislamu. Nimeambiwa huduma hii ya Al- Barakah Banking inafuata sheria za Kiislamu ikiwemo mikopo ya bila riba,”amesema. 

Amewaomba Waislamu ambao waliokuwa wanashindwa kutumia huduma ya Benki kwa sasa CRDB imezingatia mahitaji yao hivyo kuwasihi waende wakafungue akaunti ili fedha zao ziwe salama.
“Katika Mapinduzi ya Viwanda huduma za kibenki ni muhimu sana kwani awamu hii ya mapinduzi ya viwanda imejikita huduma kiganjani. 

"Maana yake ni kwamba unapata huduma palepale ulipo. Kwa mfano leo ukiweka fedha zako benki unaweza kulipia huduma yoyote kwa kutumia simu yako ya mkononi ikiwemo kulipa bili za maji, Kununua LUKU, kulipa ada za watoto na huduma mbalimbali za kibenki,”amesema Mkuu huyo wa Mkoa wa Shinyanga.
Amesema, kwa wakati huu ni vyema wananchi wakatumia huduma za kibenki ambazo zinarahisisha upatikanaji na utumiaji wa huduma mbalimbali ikiwemo mikopo kwa ajili ya kujiinua kiuchumi.

“Napenda kuupongeza uongozi wa Benki ya CRDB kwa kukubali maombi ya serikali ya kushusha riba ya mikopo ya sekta ya Kilimo hadi asilimia 9. Niwaombe wananchi tuchangamkie fursa hii ili kilimo chetu kiweze kuwa cha kisasa ambacho kitaongeza tija,”amesema Mjema.

Mjema ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika Agosti 23,2022 huku akiwataka kuendelea kutoa ushirikiano katika zoezi la anwani za makazi.

Akitoa Salamu wakati wa hafla ya kufuturisha iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa wateja na wadau wa benki hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi wa Benki ya CRDB, Bw. Pendason Philemon amesema Futari hiyo ni mwendelezo wa utamaduni wa Benki ya CRDB kuungana na Waumini wa Dini ya Kiislamu wanaoishiriki Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi wa Benki ya CRDB, Bw. Pendason Philemon akizungumza wakati wa Hafla ya Futari iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa Wateja na Wadau wa Benki ya CRDB Mkoa wa Shinyanga.

“Kwetu Benki ya CRDB umekuwa ni utamaduni wetu kuandaa futari maalumu kwa ajili ya wateja wetu, wadau pamoja na wenzetu wenye uhitaji ambao wapo katika Mfungo wa Mwezi wa Ramadhani. Futari hii ya leo ni mwendelezo wa utamaduni wetu kuungana na ndugu zetu wanaoshiriki mfungo kujinyenyekeza kwa Mwenyezi Mungu,”amesema Philemon.

Amesema sambasamba na kuandaa futari, Benki ya CRDB imekuwa ikishirikiana na Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kuainisha vituo vya kulelea watoto wenye uhitaji mkubwa na kuvipatia msaada wa futari ili kuwasaidia watoto na walezi wao kuitekeleza na kuikamilisha ibada ya swaumu kikamilifu.
“Katika futari hii ambayo ni ya pili kuifanya kipindi hiki baada ya kufanya mkoani Tanga, pia tumejumuika na watoto wetu wenye mahitaji maalumu ambao pamoja na kushiriki nao futari lakini pia tumewaandalia zawadi kidogo ya unga wa ngano, sabuni, mafuta ya kupikia na vitu vingine ambavyo vitawafaa katika kipindi hiki cha mfungo.Jambo hili litafanyika katika Kanda zote saba za Kibiashara za Benki ya CRDB.

“Pamoja na ushiriki wetu katika mfungo wa Mwezi wa Ramadhani kupitia futari na misaada kwa wenye uhitaji, Benki yetu ya CRDB kwa kutambua uwepo wa mahitaji maalumu ya huduma za fedha kwa wenzetu wenye imani ya Kiislamu, tuliweza kukaa chini na kutengeneza bidhaa maalumu kwa ajili yao inayoitwa Al – Barakah ili kudhihirisha ni kiasi gani ambavyo Benki yetu inaishi katika kauli mbiu yake ya ‘Benki inayosikiliza mteja,”ameeleza.
Meneja Biashara wa Benki ya CRDB Kitengo cha Al – Barakah Banking, Thabit Galia akielezea huduma ya Al Barakah Banking wakati wa Hafla ya Futari iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa Wateja na Wadau wa Benki ya CRDB Mkoa wa Shinyanga.

Akielezea kuhusu Huduma mpya ya Al – Barakah Banking, Meneja Biashara wa Benki ya CRDB Kitengo cha Al – Barakah Banking, Thabit Galia amesema huduma hiyo ambayo haina riba na inayofuata misingi ya Sharia za Kiislamu inapatikana katika dirisha maalumu kwenye maeneo yote ambayo Benki ya CRDB inatoa huduma zake hivyo kuwaomba waumini wa dini ya Kiislamu kutumia huduma hiyo kwa ajili ya huduma za kifedha.
Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi Saidi Pamui akizungumza wakati wa Hafla ya Futari iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa Wateja na Wadau wa Benki ya CRDB Mkoa wa Shinyanga.

Kwa upande wake, Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi Saidi Pamui wameamua kuandaa futari hiyo, baada ya Tanga ili kuonesha ni kiasi gani wanauthamini na kuupa thamani na heshima kubwa mkoa wa Shinyanga na kuthamini ushirikiano wa kibiashara unaotolewa na wakazi wa Shinyanga.

“Shughuli ni watu, isingekuwa na maana kama tungeandaa shughuli hii na kusiwepo na watu wa kushiriki nao. Tunawashukuru wote kwa kuitikia wito wa kujumuika nasi, mmetupa heshima kubwa.

Benki ya CRDB itaendelea kuwa tayari kushirikiana na wadau mbalimbali na jamii ya Watanzania siyo tu katika kipindi hiki ch Mwezi Mtukufu wa Ramadhani bali nyakati zote kama ambavyo tumekuwa tujinasibu na kauli mbiu yetu ya ‘Ulipo Tupo’”,amesema Pamui.
Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, Ismail Makusanya akizungumza wakati wa Hafla ya Futari iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa Wateja na Wadau wa Benki ya CRDB Mkoa wa Shinyanga.

Naye, Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga Ismail Makusanya amewashukuru Benki ya CRDB kwa kuandaa Futari hiyo akieleza kuwa kipindi cha Mfungo wa Mwezi wa Ramadhani ni wakati wa kujitafutia thawabu nyingi kwa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kupitia ibada,ukarimu na upendo kwa ndugu,jamaa na marafiki na kutoa zaka na sadaka kwa wingi.
Sheikh wa Wilaya ya Shinyanga Soud Kategire akizungumza kwenye Hafla ya Futari iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa Wateja na Wadau wa Benki ya CRDB Mkoa wa Shinyanga.
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Shinyanga Sheikh Balilusa Khamis akizungumza kwenye Hafla ya Futari iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa Wateja na Wadau wa Benki ya CRDB Mkoa wa Shinyanga.
Meneja wa Benki ya CRDB tawi la Shinyanga, Luther Mneney akizungumza kwenye Hafla ya Futari iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa Wateja na Wadau wa Benki ya CRDB Mkoa wa Shinyanga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news