Dawa za kulevya zilivyoacha kilio kwa Mtumishi wa Umma Shirika la Posta-2

NA GODFREY NNKO

KATIKA chapisho lililopita Aprili 27, 2022 tuliona namna ambavyo, Bw.Yohana Komba ambaye alihudumu nafasi ya utumishi wa umma katika Shirika la Posta Mkoa wa Tabora kwa miaka karibu sita kati ya mwaka 2007 hadi 2012, akiwa amebobea zaidi katika masuala ya Teknolojia ya Habari (IT) na baadaye kuachishwa kazi kutokana na matumizi yaliyopitiliza ya dawa za kulevya, hivyo kujihusisha na vitendo vya wizi Ili kupata fedha za kununulia heroine akiwa kazini,

Tuliona baba yake mzazi alimpatia fedha kwa ajili ya kwenda kulipia mtihani,lakini hakufanya hivyo badala yake alikwenda kununulia heroine kwa ajili ya kuvuta.

"Ila ule mtihani niliokuwa ninapaswa kufanya wa online ambao ulikuwa ni wa muhimu sana, sikufanya kwa sababu nilikuwa natumia madawa (dawa za kulevya). Basi nilipewa zile pesa, mimi nikaenda kuvuta unga, yaani ninajutia hiyo nafasi mpaka leo, maana hiyo programu Tanzania nzima haikuwepo mpaka uende Uganda ule mtihani wa mwisho kabisa sikufanya maana kuna module 1 mpaka 4.

"Mzee alinipa pesa zote, alikuwa hana shida kabisa, nilimdanganya nimelipia kumbe mimi nimevuta unga, basi nilipomaliza chuo nikaenda kukaa nyumbani, mzee wangu. Endelea sehemu ya pili...
Mwaka 2007, mzee wangu akawa amehamishiwa Dodoma kuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Simu Kanda ya Kati, nikawa nami nimemfuata huko, baada ya kumaliza chuo".

Ajira yaanza Posta

"Basi akanitafutia ajira Shirika la Posta, kazi yangu ni kusimamia kazi Dodoma kama temporary na nikawa ninalipwa kama miezi miwili,baadae tukafanyiwa 'interview' (usaili) nikafaulu, nikawa nimeajiriwa kwa mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2007, nikapangiwa kwenda kufanya kazi Tabora ila bado nikawa ni mbobezi wa kuvuta unga.

"Nilipofika Tabora kukawa hakuna unga (heroine) kabisa, ila nilikuwa nimenunua unga wangu kama wa laki hivi, nilivuta weee...hatimaye ukaisha kabisa, nikaanza kuuliza vijiwe bila mafanikio huko Tabora maana palikuwa hapajachangamka, basi nilikaa kama miezi minne, lakini kulikuwa na mke wangu alikuwa anatoka Ulaya anakuja Dar es Salaam, halafu anakuja Tabora kuniona.

Mke apeleka Heroine bila kujua

"Kwa hiyo nikawa ninaagiza marafiki zangu wanafunga 'parcels' (vifurushi) mabox kama mawili wanampa, wanamwambia huu mzigo wa Kamanda, mpelekee Kamanda, yeye (mke wake) anabeba bila yeye kujua ananiletea unga (heroine) ninavutaa wee..mpaka unaisha.

"Lakini kwenye kutembea tembea nikakutana na jamaa mwenyeji wa Tabora, familIa yao wanamiliki choo pale stendi ya Treni, wao...yeye alikuwa msimamizi mkuu, kumbe nae anatumia unga, alikuwa anaagiza mzigo kutoka Dar es Salaam.

"Kwa hiyo kila treni ikija anatumiwa, na mimi kwa kuwa tulikuwa marafiki, tukaanza kuchanga pesa tunaagiza tunaletewa, tunagawana ilikuwa ni mwaka 2008.

"Baadae tukapata rafiki yetu mwingine alikuwa anauza unga Mwanza, tukawa tunamuagiza mzigo wetu anatupatia tunaachana anaendelea na safari na tukaendelea na utaratibu huo na baadae nikampata jamaa mmoja rafiki yangu 'aliwatani', alikuwa anauza bangi mji mzima pale na yeye alikuwa hajawahi kuvuta unga ila ukiwa unavuta bangi ni rahisi kuvuta unga, basi nikawa naenda pale kwake kuvutia unga pale.

"Ila yeye alikuwa na uwezo mkubwa kiuchumi, kwani ana manyumba (nyumba), mifugo na mimi nilikuwa nategemea mshahara tu (kutoka Shirika la Posta), basi nikaanza kumshawishi aanze kuvuta unga, kweli akaanza kuvuta na nikaendelea kumshawishi aanze kuuza ili iwe rahisi kwetu kupata kwa urahisi, kweli alianza hiyo biashara ya kuuza akawa anaagiza kwenye treni inatuletea unga anauza, nyingine anavuta.

Uhaba wa Heroine

"Wakati mwingine tulikuwa tunakaa hata siku mbili au tatu mzigo haufiki. Tukawa tunakaa hata wiki bila kuvuta, tunakuwa hatujaridhika, 'solution' (ufumbuzi) ya unga ni unga tu hakunaga mbadala eti utakunywa pombe.

"Basi tukawa tumeshajuana na Twaha (Twaha Amani), akawa ndio mtumiaji mkubwa sana, tukawa tunaagiza wote na mimi uvutaji ukawa unaongezeka na kazini nikawa situlii.

"Maana mwanzoni nilikuwa navuta jioni kwa jioni, lakini nikabadili ratiba muda wa chai,chakula na jioni ndiyo kabisa ninakaa mpaka usiku narudi kwangu kulala".

Mambo yaanza kuharibika

"Basi utendaji kazi wangu ukaanza kupungua kwa sababu matumizi yameshakuwa makubwa, ninavuta unga,ninakunywa pombe, matumizi yakawa kama ya Dar es Salaam, mbaya zaidi pale kazini kwangu kulikuwa na Chuo cha Utumishi wa Umma.

"Hivyo, kulikuwa na wanawake kwa hiyo nikawa natembea na wanawake kibao, mara navuta unga na bado nategemea mshahara wangu huo huo.

"Basi pale kazini kulikuwa na mfanyakazi mwenzagu, yeye alikuwa kwenye 'Strong Room', nikawa ninafanya ujanja ujanja, nina-edit (kuhariri), ninafuta, halafu ninatuma, anafanya mahesabu ya mwisho, yeye ana-balance, tunagawana fedha, ninakwenda kununua unga (heroine), nilifanikisha hilo kwa sababu mimi ndio nilikuwa na password ya system (nywila ya mfumo wote) yote."

Onyo Ofisini

"Tuliendelea hivyo hivyo, na ujanja wetu wa kuedit, nikawa ninapata pesa ya kutumia vitu vyangu (dawa za kulevya aina ya heroine),ofisini walinishtukia kwa mara ya kwanza wakanipa onyo, sikulitilia maanani, nikaendelea na mambo yangu, halafu pale Tabora mimi tu ndiyo nilikuwa mtu wa IT kipindi hicho.

"Sasa watu wa makampuni, taasisi mbalimbali walikuwa wananiletea vitu vyao mfano laptop (kompyuta mpakato) niwasaidie kutengeneza, baada ya kutoka kazini nilikuwa nimeshatengeneza fedha nyingi, kutokana na uaminifu mkubwa sana kwa watu na walikuwa hawajanijua kama ninatumia unga (heroine), kiukweli nikikumbuka mpaka najuta.

"Na kipindi hicho Twaha alikuwa anaishi kota za polisi ila matumizi yalivyoongezeka ilibidi ahame pale kota aende kupanga mtaani, karibu na jamaa yetu muuzaji ili awe huru zaidi na kupata unga kwa urahisi.

Mfungaji mkuu wa Heroine

"Sasa kipindi tunamshawishi jamaa auze unga, alikuwa hajui kufunga unga, kwa hiyo akawa ananitegemea mimi nije kumsaidia kufunga, mimi si nimetoka Dar es Salaam? Nilikuwa ninafahamu vizuri sana kazi hiyo ya kufunga, kwa hiyo nilikuwa nadanganya kazini (Shirika la Posta Tabora) kuwa nimepata udhuru ili niende kusaidia kufunga unga (heroine), hakuna mtu mwingine alikuwa anajua, na bila mimi watu walikuwa hawavuti.

"Ilikuwa mwaka 2009 kwenda 2010 mambo yameshachanganya, unga umekolea sawa sawa, nikaanza mara wizi huko kazini licha ya kwamba walishanipa onyo kwa sababu nilishaharibu.

"Siku moja nikapata matatizo, nikakamatwa na polisi wakati tuko kwa jamaa yangu niliyemshawishi aanze kuuza na wakati huo unga (heroine) umekolea, baada ya hapo kila mtu na shughuli zake, hakuna tena cha undugu.

"Kwa hiyo walipotukamata nikawapa hela, wakatuacha nilikuwa ninafanya kazi, kwa hiyo nina vihela hela sana, lakini wakawa wameishajua wapi wanauza unga, akina nani wanavuta na inapatikanaje na tayari unapatikana kiurahisi kabisa na kukawa na mwingine ambaye alikuwa anauza unga, lakini yeye havuti".

Heroine yasambaa

"Kwa hiyo unga (heroine) ukawa uko sehemu nyingi na muda wote na maaskari walipotukamata wakajua fika unga unauzwa Tabora, na mimi wakati huo nilikuwa natengeneza makompyuta (kompyuta), kwa hiyo kuna kompyuta zilipotea siku moja huko mjini, kwa sababu nilikuwa na tayari walishajua natengeneza kompyuta na bado ni mvutaji mjanja mjanja.

"Basi askari walijua pa kunipata, waliandika barua kutoka kwa RCO wakaleta ofisini, wakampa bosi wangu, wakisema kuna kompyuta zimeibiwa, kwa hiyo tuna mahojiano nae (Yohana Komba),na tunamhisi anajihusisha na madawa (dawa za kulevya),hivyo wakasema wana mahojiano na mimi, japo sikuiba, waliiba watu wengine japo walijua wataleta kwangu kwa kuwa natengeza kumbe walipeleka kwa mwingine,"anasema Bw. Yohana.

Ahojiwa Polisi

"Basi nikaenda kwa RCO nikahojiwa hojiwa, nikaambiwa tuna habari zako zote, tunazo umetolewa Dar es Salaam kwa ajili ya maunga unga (dawa za kulevya) na ukatuletea mambo yako ya maunga unga, ila wale askari walishawahi kunikamata na wana uhakika.

"Lakini walishindwa kusema kama walishanikamata kwa kuwa niliwapatia pesa, angewauliza siku hiyo wametukamata ila wakasema mbele ya bosi wao kuwa huyu tunamjua anatumia madawa.

"Nikachukuliwa nikalala polisi siku ya pili, nikatolewa maana baba yangu aliongea na Meneja wa Posta nikatolewa, nikarudi kazini kama kawaida, kwani baba yangu alikuwa bado meneja, akaongea nae mambo yakaisha,lakini baba akaanza kunionya na kuanza kunisema kuwa amepata habari zangu, nikasema sio kweli wananisaspect, baba akahoji kwa nini uwe suspected? Mzee akaanza kuwa na wasiwasi.

Usingeweza Kumjua

"Mimi nilikuwa nafanya kazi, lakini mtu asingeweza kunijua ambaye hajawahi kuniona, nikivuta maana nilikuwa msafi, ninanukia vizuri,navaa vizuri, ninaoga na ninalipwa vizuri na bado ninafanya kazi nyingine ninapata pesa nyingi tu, nikawa naendelea nakamatwa natoa pesa polisi ninaachiwa, hivyo gari likaanza kukolea hatari mwaka 2009 kwenda 2010 nikawa niachelewa kazini, naleta sababu ambazo hazina mashiko mara siku nyingine siendi kabisa.

"Sasa huko Tabora kuna eneo linaitwa Isevya ( Isevya ni Kata ya Manisipaa ya Tabora katika Mkoa wa Tabora) lilikuwa ni maarufu kwa uhalifu, ujambazi na bangi na marafiki zangu wa ofisini wakawa wananiona huko wakati wakipita kuelekea kwenye majukumu yao, wakaanza kunihofia na kuanza kuamini yale ninayotuhumiwa nayo ni kweli, ninafanya, lakini kazini parfomance sio mbaya, nilipewa onyo tena.

"Ilifikia hatua kwa sababu uga umekolewa, nikawa ninampigia bosi wangu simu, ninamdanganya nimepata dharura, nitakuja baada ya saa moja, hapo unakuta nimevuta zote (dawa za kulevya heroine) usiku nimeamka nimeishiwa. Kwa hiyo inanilazimu niende unga unapouzwa asubuhi, nivute kwanza ndipo niende kazini, basi bosi wangu akawa ananiambia jitahidi uwahi haraka na huko unakuta unga umeisha lengo nivute, halafu niende ofisini ikawa ni unga kazini."

Afoji cheki

"Nikaenda hivyo hivyo na wizi unaendelea ilipofika mwaka 2011 kwenda 2012 tukio lililonifukuzisha kazi nikiwa Mtumishi wa Shirika la Posta, nilifoji cheki na mshikaji wa CRDB, nilipata ishu ya cheki ila kwa mara ya kwanza tulifanya vizuri tukagawana hela, nyingi tu. Nikaenda kununulia unga (heroine).

"Mara ya pili nikakamatwa walishtukia na kuweka mitego kwenye mtandao nikanaswa, ikanipelekea nikasimamishwa nikiwa kazini, lakini nikawa naenda kazini ninasaini ninaondoka na mshahara ninapewa kama miezi mitatu, wenyewe wako kwenye vikao vya nidhamu na uchunguzi."... Itaendelea chapisho lijalo hapa DIRAMAKINI BLOG.

Post a Comment

0 Comments