Lulanzi Matunda waandamana kupinga adhabu ya kufungiwa masuala ya siasa Balozi wao

NA ROTARY HAULE

BAADHI ya wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mtaa wa Lulanzi Matunda uliopo Kata ya Picha ya Ndege Kibaha wameandamana katika ofisi ya CCM tawi la Lulanzi kwa ajili ya kupinga adhabu ya balozi wao, Saimoni Kushoka ya kuzuiwa kufanya siasa katika kipindi cha miezi 12.

Maandamano ya wananchi hao yamefanyika Aprili 2, 2022 katika ofisi hizo ikiwa ni saa chache baada ya balozi Kushoka kukabidhiwa barua maalum kutoka ofisi ya tawi hilo juu ya kufungiwa masuala ya siasa katika kipindi hicho.
Mmoja wa wananchi hao, Athumani Said amesema kuwa, wameshtushwa na taarifa ya balozi wao kuzuiwa kufanya siasa kwa kipindi kirefu ndio maana wameandamana kujua sababu ya adhabu hiyo.

Said amesema kuwa, wananchi wa Mtaa wa Lulanzi Matunda wamekuwa wakimtegemea Kushoka katika mambo mbalimbali ya kijamii hasa katika ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo lakini anashangazwa kuona amepewa adhabu kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi.
Ameongeza kuwa,katika kipindi hiki cha uchaguzi walikuwa wakimtegemea Kuchoka achukue fomu kwa ajili ya kugombea nafasi ya ujumbe wa CCM katika tawi hilo lakini ghafla wakashangaa anapewa barua ya adhabu.

"Huyu Kushoka sisi tunamhitaji sana katika eneo letu kwa ajili ya kusimamia na kufuatilia miradi yetu ya maendeleo, lakini tumeshangaa wakati anakuja kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya ujumbe anakutana na barua ya adhabu jambo ambalo hatujaliafiki,"amesema Said.

Nae Martha Kalinga amesema kuwa, Kushoka ni mchapakazi ambaye amekuwa anamsaada mkubwa katika Mtaa huo huku akisema amepigania eneo hilo kupewa hati miliki eneo ambalo awali walitakiwa kuondolewa na Serikali kwa madai ya kuwa wavamizi.

Martha amesema,wanachotaka wao adhabu ya Kushoka iondolewe ili aweze kuchukua fomu kwakuwa ndiye mtu sahihi wanayemhitaji katika eneo lao na kwamba hawapo tayari kuchaguliwa mtu wala kuletewa mtu mwingine katika eneo lao.

"Tunawataka viongozi waliokuwa madarakani waendelee kwakuwa wamefanyakazi kubwa na nzuri katika Mtaa wetu na yapo mengine wameyaanzisha wanatakiwa kuyamalizia kwanza,kwahiyo hatutaki watu wakuletewa ,"amesema Martha.

Kwa upande wake balozi wa Mtaa wa Lulanzi Matunda, Saimoni Kushoka amesema kuwa, amepewa barua ya kusimamishwa kujihusisha na Siasa katika kipindi cha miezi 12 kutoka kwa mwenyekiti wa tawi la CCM Lulanzi Michael Ngosi April 1,2022.

Kushoka amesema kuwa, siku aliyopewa barua hiyo ni siku ambayo ni siku ambayo kwa mujibu wa utaratibu wa Chama fomu zilikuwa zimeanza kutolewa lakini alipofika ofisini hapo alishangaa anapewa barua ya adhabu.

Kushoka amesema njama za kuzuiwa kuchukua fomu za kugombea nafasi ya uongozi katika tawi hilo zimepangwa na Diwani wa Kata ya Picha ya Ndege Karim Mtambo kwa madai ya kulinda maslahi yake.
Aidha,Diwani Mtambo katika mahojiano na DIRAMAKINI BLOG amesema, hana mamlaka yoyote ya kumzuia mtu kuchukua fomu isipokuwa chama kina utaratibu na kila mtu anatakiwa kuufuata.

Mtambo amesema, kwa nafasi yake ya udiwani yupo tayari kufanyakazi na mtu yeyote bila ubaguzi kwa maslahi na maendeleo ya wananchi wote na kwamba kama mtu ameonewa ni vyema akafuata utaratibu wakichama.

Mwenyekiti wa tawi hilo, Michael Ngosi,ameiambia DIRAMAKINI kuwa ofisi ya tawi haina makosa kwa kuwa barua waliyompa Kushoka imetoka katika ofisi ya CCM Kata ya Picha ya Ndege.

Hata hivyo,Katibu wa CCM Kata ya Picha ya Ndege Ally Lwambo, amesema barua ya kusimamishwa Kushoka imetokana na maamuzi ya kamati ya siasa katika kikao chake kilichofanyika Machi 15 mwaka huu.

Lwambo amesema kuwa, Kamati ya Siasa imefikia maamuzi hayo baada ya Kushoka kuandika barua ya malalamiko ya kuwatuhuma viongozi akiwemo diwani huyo kupanga safu za uchaguzi huo.
Amesema kuwa,baada ya ofisi ya kata kupata barua ya malalamiko kutoka kwa Kushoka walimuhita ofisini ili atoe ushahidi, lakini alikosa na hatimaye kamati kufikia maamuzi hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news