NAIBU MEYA SAADY KHIMJI AGAWA FUTARI KWA WAJANE

NA HERI SHAABAN

NAIBU Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Saady Khimji amegawa futari kwa wajane na watu wenye mahitaji maalum wa Kata ya Ilala.
Naibu Meya Khimji aligawa futari hiyo katika Ofisi ya Kata ya Ilala ambapo alikutana na wajane pamoja na makundi maalum.

Khimji alisema, futari hiyo aliyotoa kwa wananchi wake amepewa na wadau wake Shule ya FEZA International School na mwakani atajipanga vizuri kwa ajili ya tukio kubwa, kwani anajali mchango wa viongozi na makundi yote ambayo anashirikiana nao vizuri katika kuleta maendeleo pamoja na kujenga Ilala.

Alisema, amefarijika katika jambo hilo kwa kushirikiana na Kamati ya Maendeleo Kata na Wenyeviti wake wote.
Khimji aliwataka eenyeviti wake wa Serikali za mitaa waendelee kushirikiana katika utendaji kazi sambamba na kuleta maendeleo.

Aliwashukuru wajane na watu wenye mahitaji maalum kuitikia wito wa kikao hicho maalum cha kupokea futari hiyo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Ally Mshauri alimpongeza Diwani Saady Khimji kwa msaada huo ambao amesema una dhumuni la kuunganisha watu wa Kata ya Ilala pamoja.

Diwani wa Viti Maalum Wanawake Kata ya Ilala, Asha Kipini alimpongeza Diwani Saady Khimji kwa kugawa futari hiyo kwa wajane na makundi maalum.

Post a Comment

0 Comments