NYASI HUKU ZAUNGUA:Wenyewe mngeamua, silaha chini kutua

NA LWAGA MWAMBANDE

MGOGORO kati ya Urusi na Ukraine umetajwa na mataifa mengi ndani na nje ya Afrika kuchangia bei ya mafuta kupanda kwa kasi duniani. Kupanda kwa bei ya mafuta duniani kumesababisha mnyororo wa bei za uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa kuanza kuongezeka kwa kasi.
Kwa upande wa vyakula, Urusi na Ukraine ndiyo wasambazaji wakuu wa ngano,mafuta ya kula na mazao mengine ya nafaka duniani ikiwemo mbolea kwa ajili ya kukuzia mazao. Vita ya pande hizo mbili inatajwa kuleta athari kubwa, ambapo kwa sasa mataifa mengi yanalazimika kutumia gharama kubwa kupata bidhaa hizo huku bei zikiwa zinaendelea kupanda kwa kasi.

Hivi karibuni Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umeonya kwamba mgogoro wa Urusi na Ukraine unaweza kuwa na athari mbaya za kupandisha bei za vyakula na kusababisha njaa kwa maskini katika maeneo mengi duniani hususani Afrika.

Ungana na mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande uweze kujifunza jambo hapa chini kwa njia ya ushairi;

1:Endapo mngelijua, jinsi latupiga jua,
Wenyewe mngeamua, silaha chini kutua,
Nasi tuweze pumua, na kivuli kukijua,
Tembo mnapopigana, nyasi huku zaungua.

2:Haya yote mlijua, na vita mkaamua?
Au yanawastua, vile yanatushtua?
Haya hatukuyajua, sasa ndio tunajua,
Tembo mnapigana, nyasi huku zaungua.

3:Visima tulivyojua, na wenyewe mwavijua,
Kule tulikokamua, mafuta mwavifumua,
Vita vyenu twaungua, hari tusiyoijua,
Tembo mnapopigana, nyasi huku zaungua.

4:Mafuta ya kununua, ya kula na kuungua,
Bei tusizozijua, ndio zinatulangua,
Zama tusizozijua, sasa zinatutungua,
Tembo mnapopigana, nyasi huku zaungua.

5:Tunanyongwa tunajua, hakuna kwa kutanua,
Hali inatuzingua, na vumbi inatimua,
Hivi wababe mwajua, vidonda mwavifumua?
Tembo mnapopigana, nyasi huku zaungua.

6:Kusemasema mwajua, huku ndege mwatungua,
Mnapanda mwafukua, mavuno mtapakua?
Ni lini mtatambua, kwamba mnatupunyua?
Tembo mnapopigana, nyasi huku zaungua.

7:Afrika kali jua, bei za huku mwajua,
Na watalii mwajua, pia nao wapungua,
Ni lini mtatangua, amani mkachukua?
Tembo mnapopigana, nyasi huku zaungua.

8:Marekani nako jua, bei zingine twajua,
Malimao twayajua, bei zinawasumbua,
Bila hatua chukua, mbele kubaya twajua,
Tembo mnapopigana, nyasi huku zaungua.

9:Finland wanajua, bei wanavyoungua,
Lita mafuta twajua, huku bado twatanua,
Elfu tatu likuwa, elfu sita nunua,
Tembo mnapopigana, nyasi huku zaungua.

10:Kote kote wanajua, ni vita vimetibua,
Lakini kuvitangua, bado wanasuasua,
Mgogoro kutatua, wanachochea twajua,
Tembo mnapopigana, nyasi huku zaungua.

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

Previous Post Next Post

International news