Rais Dkt.Mwinyi aguswa na utayari wa Chuo cha CBE kujenga kampasi Zanzibar

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza azma ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) ya kujenga Kampasi ya Chuo hicho hapa Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi wa Chuo hicho Prof.Wineaster Saria Anderson (kulia kwa Rais) walipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo.(Picha na Ikulu).

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Aprili 6,2022 Ikulu jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na uongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) ulioongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa Chuo hicho, Profesa Wineaster Sania Anderson.

Katika maelezo yake Rais Dkt. Mwinyi ameueleza uongozi huo kwamba, uamuzi huo wa kujenga chuo cha elimu ya Biashra hapa Zanzibar utawasaidia kwa kiasi kikubwa wanafunzi wa Zanzibar ambao walikuwa wakifuata elimu hiyo huko Tanzania Bara.

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha chuo hicho kinajenga Kampasi yake hapa Zanzibar kwani uamuzi huo ni mzuri na unahitaji ushirikiano.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amepongeza azma ya chuo hicho ya kutoa mafunzo hata kwa vijana walioishia Kidato cha Pili ambao wameshindwa kuendelea na elimu ya juu.

Ameongeza kuwa, hatua hiyo ya kuwasomesha vijana walioishia Kidato cha Pili na kushindwa kuendelea na elimu ya juu ni miongoni mwa malengo na mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Ameeleza kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendeleza mikakati yake ya kuimarisha elimu ya Vyuo vya Amali ili kuhakikisha vijana walioshindwa kuendelea na elimu ya juu nao wanapata elimu za stadi za maisha katika vyuo hivyo hapa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Prof.Wineaster Saria Anderson alipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo.

Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa Chuo hicho, Profesa Wineaster Sania Anderson alimueleza Rais Dkt.Mwinyi azma ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) ya kujenga Kampasi yake hapa Zanzibar.

Katika maelezo yake Profesa Anderson alimueleza Rais Dkt.Mwinyi kwamba tayari mchakato wa kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho umeshafanyika na kupongeza ushirikiano mzuri walioupata kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Sambamba na hayo, Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Uongozi wa Chuo cha CBE, Professa Anderson alieleza hatua zitakazochukuliwa na uongozi huo kupitia Serikali Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika bajeti yake juu ya utaratibu wa kuanza ujenzi huo ambao utakuwa kwa awamu tatu na kutarajiwa kugharibu shilingi Bilioni 10.12.

Pamoja na hayo, Mwenyekiti huyo wa Bodi ya CBE alieleza matarajio yake kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuunga mkono juhudi zao hizo kwa kutambua kwamba kumekuwa na mashirikiano mazuri kati ya Chuo hicho na Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na kuagana na Ujumbe wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho Prof.Wineaster Saria Anderson, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar leo.(Picha na Ikulu).

Ameongeza kuwa, miongoni mwa wanafunzi watakaowachukua kwa ajili ya kujiunga na chuo hicho kitakapokuwa tayari kuanza mafunzo ni wale walioishia Kidato cha Pili na kushindwa kuendelea na elimu ya Juu ambao watawaanzisha elimu ya Cheti mpaka Digirii katika kada hiyo ya elimu ya biashara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news