Rais Samia awataka waigizaji wa Tanzania wampe muda, uzinduzi wa The Royal Tour wafana New York

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesema anaanza kuwakutanisha waigizaji wa Tanzania na kampuni kubwa zilizofanikiwa kwenye masuala ya filamu duniani.
Miongoni mwa makampuni hayo ni Paramount Pictures na AMC ambazo tayari amekutana na wawakilishi wao awali kwenye kikao jijini New York,Marekani.

Paramount Pictures Corporation ni kampuni kubwa ya Kimarekani ya utengenezaji na usambazaji wa filamu za runinga na kampuni tanzu kuu ya Paramount Global (zamani iliyokuwa ViacomCBS).

Ni studio ya tano kongwe ya filamu duniani, na studio ya pili kongwe ya filamu nchini Marekani (nyuma ya Universal Pictures), na mwanachama pekee wa studio za filamu za Big Five iliyopo jijini Los Angeles, Marekani.
Mheshimiwa Rais Samia ameyasema hayo baada ya kuulizwa swali na mmoja wa wageni kwenye uzinduzi wa filamu ya The Royal Tour ambayo imetengenezwa mahususi kutangaza utalii wa Tanzania.

Uzinduzi huo ambao ulifanyika katika ukumbi wa Guggenheim Museum, New York nchini Marekani ulisindikizwa na burudani safi kutoka Kikundi cha Ngoma za asili cha Bagamoyo. "Ninaanza kuwaunganisha na Dunia waigizaji wa kike na kiume wa Tanzania.Jana nilikuwa na kikao kizuri sana na kampuni kubwa tano za utalii hapa Marekani na kwingineko, yalikuwa mazungumzo mazuri na nilikutana na mtu anayefanya kazi na Paramount na AMC, tulikuwa na mazungumzo mazuri ya kuunganisha utamaduni na sanaa ya Tanzania kwao, nipeni muda,"ameeleza Mheshimiwa Rais Samia.

The Royal Tour ambayo ni filamu ya matukio halisi (documentary film) ambayo iliandaliwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezinduliwa Aprili 18, 2022 huko New York nchini Marekani.

Kazi hiyo ya mwanahabari mkongwe Peter Greenberg iliandaliwa mwaka 2021 na ilihusisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa kama muongozaji mkuu, ambapo Rais alihudhuria uzinduzi huo wa filamu huku ikiwakutanisha wageni mbalimbali duniani.
Akizungumza kuhusu kazi hiyo kabla ya uzinduzi rasmi, Rais Samia amesema, lengo kuu la kazi hiyo ni kutangaza Tanzania kama eneo zuri la utalii katika juhudi za kufufua sekta utalii baada ya janga la UVIKO-19.

Baada ya New York kazi hiyo itazinduliwa tena huko Los Angeles nchini Marekani tarehe 21 mwezi huu wa Aprili mwaka 2022 kabla ya kurejeshwa nyumbani Tanzania tarehe 28 jijini Dar es Salaam na baadaye jijini Zanzibar.

Rais Samia kupitia ziara hiyo ya kikazi nchini Marekani ameandamana na jopo maalumu la viongozi kutoka serikalini na sekta binafsi ambalo lina jukumu kubwa la kuwashirikisha wawekezaji kutoka Marekani fursa mbalimbali zilizopo Tanzania kuanzia sekta ya utalii na nyinginezo.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inajivunia vivutio vingi vya utalii ambavyo vina upekee duniani ukiwemo Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Ngorongoro, vivutio vya kipekee vya Zanzibar na nyinginezo.
Wakati huo huo, baada ya kuitazama filamu hiyo Rais Samia aliketi jukwaani na kuulizwa maswali machache na watu mbalimbali pamoja na mtangazaji na muandaaji wa filamu hiyo, Peter Greenberg ambapo hakusita kuinadi Tanzania kuwa sehemu nzuri ya kutembelea na yeyote atayefika Tanzania hatojutia uamuzi wake.

"Nchi ya Tanzania ni sehemu ambayo mtu anaweza kuitembelea muda wowote japokuwa muda mzuri wa mwaka huwa ni kati ya Juni na Julai ambako hakuna joto sana,"amesema Mheshimiwa Rais Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news