Rais Samia kushiriki Mdahalo wa Miaka 100 ya Mwalimu Nyerere, RC Kunenge afunguka

*Kufanyika Kibaha mkoani Pwani kesho

NA ROTARY HAULE

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anatarajia kushiriki mdahalo wa maadhimisho ya kumbukumbu ya Kitaifa ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere utakaofanyika Aprili 9, mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewaambia waandishi wa habari leo ofisini kwake kuwa, mdahalo huo utafanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

Kunenge amesema kuwa, Aprili 13 ya kila mwaka nchi nzima huwa inaadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere, lakini mwaka huu utatangulia mdahalo mkubwa utakaofanyika Kibaha huku mgeni rasmi akiwa Mheshimiwa Rais Samia.

Aidha, Kunenge amesema kuwa lengo la mdahalo huo ni kufanya tafakuri na mwenendo wa maisha ya Mwalimu Nyerere enzi ya uhai wake pamoja na kuenzi shughuli mbalimbali alizozifanya katika uongozi wake.

Amesema,maadhimisho hayo hufanyika nchi nzima lakini Mkoa wa Pwani mwaka huu umepata heshima kubwa ya kutembelewa na Mheshimiwa Rais katika kushiriki pamoja na wananchi na wanachama wa CCM kwa ujumla.

"Namshukuru Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutupa heshima sisi wana Mkoa wa Pwani kwa kutumia muda wake kuja Pwani kushiriki mdahalo wa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Hayyat Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere,hakika kwetu ni faraja,"amesema Kunenge.
Kunenge ameongeza kuwa, mdahalo wa maadhimisho ya kumbukumbu ya Kitaifa ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere yameandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini kila mwananchi amepewa fursa ya kushiriki bila ubaguzi wa kiitikadi.

"Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeandaa mdahalo wa kuadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwa mwasisi wa nchi yetu Mwalimu Julius Nyerere mdahalo ambao utafanyika Aprili 9 mwaka huu siku ya Jumamosi katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere,hii ni heshima kubwa kwa mkoa wetu,"amesema Kunenge.

Kunenge amewaomba wakazi wa Mkoa wa Pwani,Watanzania kwa ujumla pamoja na wale wa nchi jirani kujitokeza kwa wingi katika mdahalo huo kwa kuwa umuhimu wa mdahalo huo ni mkubwa.
"Naomba nitumie nafasi hii kuwakaribisha wananchi wa Mkoa wa Pwani,nchi jirani na Watanzania kujitokeza kwa wingi katika mdahalo huu Muhimu wa Aprili 9 ili tuungane pamoja na Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan kukamilisha kumbukumbu hiyo,"amesema Kunenge

Kunenge amesema kuwa, mdahalo huo utaanza saa mbili asubuhi, lakini wananchi wataanza kuingia saa 12 asubuhi na kila mtu anakaribishwa hivyo ni vyema wananchi wakatumia nafasi hiyo.

Hata hivyo,Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alizaliwa Aprili 13 mwaka 1922 huko Butiama mkoani Mara na alifariki Oktoba 14, mwaka 1999.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news