Rhobi Samwelly, Ustawi wa Jamii watoa tumaini la wasichana kufikia ndoto zao Serengeti

NA FRESHA KINASA

WANANCHI wa Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara wamesema, ushirikiano wa pamoja baina ya Dawati la Jinsia na Watoto, Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia wilayani humo na Mkoa wa Mara kwa ujumla, umeendelea kuwapa tumaini wasichana kufikia ndoto zao.
HGWT chini ya Mkurugenzi wake, Rhobi Samwelly, linamiliki vituo viwili vinavyotoa hifadhi kwa wasichana wanaokimbia vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni, ambapo kwa Wilaya ya Butiama ni Kituo cha Nyumba Salama (Safe House) kilichopo Kiabakari na Serengeti Kituo cha Nyumba ya Matumaini.

Wameyasema hayo kwa Nyakato tofauti wakati wakizungumza na DIRAMAKINI ambapo wamesema kuwa, uwajibikaji wao wa pamoja ikiwemo kutoa elimu ya madhara ya ukatili wa kijinisia kwa wananchi, kuchukua hatua za haraka wanapopata taarifa juu ya uwepo wa vitendo vya ukeketaji na kudhibiti kabla havijafanyika, kupaza sauti zao kwa pamoja kuhimiza umuhimu wa elimu kwa wasichana kumeendelea kuwapa hamasa wasichana kusoma kwa bidii wakitambua wanaowatetezi katika kufanikisha malengo yao.

Mbali na hayo wamesema, uwepo wa Kituo cha Nyumba ya Matumaini kinachomilikiwa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) ambacho hutoa hifadhi kwa wasichana ambao hukimbia ukeketaji na aina nyingine za ukatili kimeendelea kusaidia wasichana kuendelea na masomo yao wakiwa kituoni hapo kufuatia kukimbia kutoka katika familia zao na hivyo kutoathiri malengo yao ya siku za usoni.

"Kituo hiki kisingekuwepo ninaamini ndoto za wasichana wengi zingekuwa zinashindwa kutimia, lakini wanapofika katika kituo hicho huendelezwa kielimu na wengine katika fani mbalimbali jambo ambalo linapaswa kupongezwa, watoto wa kike wana mchango mkubwa wa kuleta maendeleo ya jamii na taifa ni vyema wakapewa sapoti wafikie malengo yao badala ya kukatishwa kwa lengo la kuozeshwa," amesema Joyce William.
Fabiani Paschal ni mkazi wa Mugumu amesema, ushirikiano Kati ya Dawati la Jinsia na Watoto, Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Jamii na shirika hilo wilayani humo katika kampeni mbalimbali za kupambana na vitendo vya ukatili wa kinjinsia umeongeza mwamko kwa jamii kuwa na ufahamu thabiti wa madhara ya ukatili. Na hivyo baadhi ya wazazi kuachana na mila ya ukeketaji ingawa bado wengine wanaendeleza mila hiyo kama sehemu ya kujipatia kipato huku wakitambua ni kosa kisheria.

"Tumekuwa tukiona wakito elimu kwa pamoja katika mikutano ya hadhara, shuleni, makongamano, barabarani juhudi hizi zote zinalenga kutokomeza ukatili wa kijinsia hapa Serengeti na kumpigania mtoto wa kike apewe nafasi ya kusoma upande wangu nawapongeza. Niwaombe waendelee kufanya hivyo bila kuchoka, pia niwashauri Wananchi wenzangu wanapoona mtu anafanya ukatili wamripoti haraka mbele ya sheria bila kuchelewa kwa hatua kali,"amesema Paschal.

Neema Shaban ni mkazi wa Kijiji cha Burunga Kata ya Uwanja wa Ndege Wilaya ya Serengeti ambapo amesema kuwa, kadri ambavyo elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia inavyoendelea kutolewa pamoja na kuwachukulia hatua kali za kisheria wanaobainika kujihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia jamii inazidi kupata fundisho na kuona ukatili hauna faida bali una madhara mengi.
Editha Matiko ni mkazi wa Mtaa wa Misitu Kata ya Mugumu ambapo alisema kuwa, kampeni za kupinga ukatili wa kijinsia ambazo zimekuwa zikitolewa shuleni zimezidi kuongeza uelewa kwa wanafunzi na kuwafanya waendelee kuwa mabalozi wema katika kupinga vitendo hivyo katika maeneo yao na kuwajengea kujiamini watoto wa kike.

"Wasichana kwa sasa wanatambua kwamba wana watetezi nyuma yao iwapo watataka kufanyiwa ukatili watasaidiwa ili wafikie ndoto zao. Hatua hii ni muhimu sana, nishauri tu kwamba sote tunajua lengo la Serikali ni kutokomeza ukatili na ndio maana ukifanya ukatili utaona dawati wanakuja juu, ustawi wa piga kelele, mashirika pia hawa wote lengo lao ni kuona jamii inakuwa salama na kwamba hakuna anayeharibu usalama wa mwenzake lazima tuwape ushirikiano ikiwemo kutoa ushahidi mahakamani watuhumiwa wanapofikishwa huko,"amesema Matiko.

Aprili 6, 2022 Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Isack Mwankusye akihitimisha mafunzo ya ujasiriamali kwa wasichana wa Kituo cha Nyumba ya Matumaini Mugumu alipongeza Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania kwa kuendelea kuwaendeleza katika fani mbalimbali wasichana wanaohifadhiwa katika kituo hicho kwani ujuzi wanaoupata unafaida katika maisha yao hususan kujipatia kipato.

Pia, Mwankusye aliihimiza jamii kuachana na mila ya ukeketaji na ndoa za utotoni, kwani hazina faida bali zina madhara ikiwemo hatari ya kupatwa na magonjwa ya kuambukiza, kutokwa damu nyingi na kuwa katika hatari ya kupoteza maisha, madhara ya kisaikolojia, hatari ya kuchanika wakati wa kujifungua kutokana na kovu la muda mrefu akasisitiza kila mwananchi kushiriki kuunga mkono mapambano dhidi ya vitendo hivyo vilivyo kinyume cha sheria za nchi na haki za binadamu.
Daniel Misoji ni Mkuu wa Kituo cha Nyumba ya Matumaini Mugumu kilichochini ya Shirika la (HGWT) akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa shirika hilo, Rhobi Samwelly, alisema kuwa Shirika hilo litaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na serikali katika kuhakikisha kwamba vitendo hivyo vinakomeshwa.

Misoji alibainisha kwamba wasichana ambao hupata hifadhi Kituo cha Nyumba ya Matumaini Mugumu na Nyumba Salama Kiabakari Wilaya ya Butiama wamekuwa wakiendelezwa kielimu, kifani pamoja na kupatiwa mahitaji yote na shirika hilo ili kusudi waweze kufikia ndoto zao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news