Sekta binafsi ni muhimu sana katika maendeleo mkoani Mara-Dkt.Haule

NA FRESHA KINASA

SERIKALI mkoani Mara imesema inatambua kwa dhati mchango mkubwa unaotolewa na sekta binafsi mkoani humo katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa Aprili 8, 2022 na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Halfan Haule wakati akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Ally Hapi katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa TCCIA uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu Huria (MCC) uliopo Manispaa ya Musoma.

Dkt. Haule mesema, sekta binafsi inachangia kwa kiwango kikubwa katika kutoa ajira, ulipaji wa kodi za maendeleo serikalini, kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Huku akisema wazalishaji wakubwa na wafanyabiashara wakubwa nchini, wanatoka sekta binafsi.
Amesema, Serikali itaendelea kushirikiana na sekta hiyo ikiwemo kuweka mazingira mazuri ili kuleta ufanisi. Huku akipongeza jitihada zinazofanywa na TCCIA mkoani humo kwa ushirikiano na Serikali zimeendelea kuleta matokeo chanya.

Dkt. Haule mesema, maendeleo na uchumi wa Taifa unachangiwa kwa kiwango kikubwa na sekta binafsi. Huku akiitaka TCCIA kuendelea kuchagiza uanzishaji wa viwanda vidogovidogo vya kuongeza thamani na kusindika mazao ya kilimo, ufugaji na uvuvi pamoja na kutafuta masoko kwa ajili ya wazalishaji hao ili waweze kuuza kwa tija.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Kilimo na wenye Viwanda mkoani Mara, Boniphace Thomas Ndengo akiwasilisha taarifa ya Mwaka 2021 kwa wajumbe wa mkutano mkuu amesema, umoja huo umeandaa mpango mkakati wa kujenga uchumi na kukuza biashara ya wananchi wa mkoa wa Mara kwa kushirikiana na Serikali.

Ndengo amesema, mpango mkakati huo umebainisha fursa na rasilimali nyingi zinazopatikana mkoani Mara kupitia shughui za Uwekezaji, Utalii na Biashara.

Amezitaja baadhi ya fursa na rasilimali hizo kuwa ni ardhi nzuri kwa uzalishaji, maji ya kutosha ya Ziwa Victoria, watu, mifugo mingi, Mpaka wa Sirari, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Historia ya mkoa wa Mara kupitia Makumbusho ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Akielezea mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka uliopita 2021, Ndengo amesema, umoja huo umeweza kuzalisha wajasiriamali mahiri ambao wanalipa kodi kwa maendeleo na uchumi wa Taifa.
Mafanikio mengine amesema ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa chakula na malighafi zitokanazo na kilimo, uvuvi na ufugaji ili kukidhi mahitaji ya viwanda vya ndani ya mkoa wa Mara na nchi jirani.

Akielezea miradi ya kimkakati ambayo ikikamilika itakuwa na tija kubwa katika uchumi na maendeleo ya mkoa wa Mara ni pamoja na ujenzi wa uwanja vya ndege Musoma na Serengeti.

Miradi mingine ni ujenzi wa Soko la Afrika Mashariki katika mpaka wa Sirari wilayani Tarime na Mpaka wa Kilongwe wilayani Rorya, kukamilika kwa ujenzi wa chuo kikuu cha Mwalimu Nyerere na ujenzi wa vyuo vya mafunzo ya ufundi Stadi VETA katika kila halmashauri.

Naye Mwenyekiti wa Wamachinga mkoa wa Mara, Charles Waitara amesema,wamachinga bado wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa mitaji, kwani hawana dhamana ya kuwawezesha kupata mikopo katika taasisi za fedha ambazo zinahitaji mkopaji awe na nyaraka za Usajili na dhamana.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara Wanawake Mkoa wa Mara, Judith Maganja Lugembe amesema, wanawake wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na maeneo ya kufanyia shughuli za uzalishaji.

Lugembe ameiomba Serikali kupitia Shirika la Viwanda Vidogo nchini (SIDO) kuongeza majengo na maeneo kwa wazalishaji wasiokuwa na maeneo ya kufanyia kazi zao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news