Shehe Mtupa awanyooshea kidole wanaoanzisha NGO's za watoto kwa maslahi yao

NA ROTARY HAULE

SHEHE Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Hamis Mtupa amezinyooshea vidole taasisi binafsi (NGO's) zinazoanzishwa kwa ajili ya kusaidia watoto yatima kuwa ziache kugeuza taasisi hizo kama sehemu ya kujipatia mitaji na utajiri.
Mtupa ametoa kauli hiyo Aprili 19,2022 wakati akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu,viongozi wa vyama vya siasa pamoja na wananchi katika hafla ya futari iliyoandaliwa na Mweka Hazina wa Chama cha Walimu Taifa (CWT), Abubakar Allawi.

Aidha,katika futari hiyo iliyofanyika katika Mtaa wa kwa Mbonde Kata ya Mkuza Halmashauri ya Kibaha Mjini, Allawi aliwaalika pia watoto yatima wa vituo mbalimbali vilivyopo Mjini Kibaha kikiwemo kituo watoto kutoka Kata ya Msangani.

Mtupa akitoa nasaha kwa waumini na wananchi hao amesema kuwa, jambo la kusaidia watoto yatima ni dhawabu kwa Mwenyezi Mungu, lakini wapo watu wanakwenda kinyume na utaratibu.
Amesema kuwa,miaka ya hivi karibuni kumeibua wimbi la watu kuanzisha taasisi za kusaidia watoto yatima lakini wengi wao wamekuwa wakianzisha vituo hivyo kwa maslahi yao binafsi.

Amesema,baadhi yao wamegeuza watoto yatima kama sehemu ya kujipatia magari ya kifahari ,majumba ya kifahari na hata utajiri wa pesa jambo ambalo halimpendezi Mungu na kwamba watu kama hao mwisho wao ni kuingia motoni.

"Ndugu zangu tuliokusanyika hapa, watoto yatima wanapaswa kusaidiwa kama watoto wengine,wanamahitaji muhimu kama binadamu wengine,kwa hiyo ni vyema tukajitoa kuwasaidia ili tupate dhawabu kwa Mwenyezi Mungu,"amesema Mtupa.

Mtupa ametumia nafasi hiyo kukemea tabia za watu wanaoanzisha NGO's za watoto yatima kwa maslahi yao kwa kusema waache tabia hiyo mara moja kwa kuwa ni kinyume na utaratibu wa maagizo ya mwenyezi Mungu.
"Kama kweli mtu anaanzisha NGO's kwa ajili ya watoto yatima basi ahakikishe misaada anayohipata inawafikia walengwa kuliko kutumia misaada hiyo kwa kununua magari na nyumba za kifahari kwani kufanya hivyo kunakupeleka motoni,"ameongeza Mtupa.

Mtupa,amesema hatua aliyoifanya Abubakar Allawi,ya kuwaalika watoto yatima katika futari hiyo inatoa mafunzo kwa waumini wa dini ya Kiislamu,wasio Waislamu ,matajiri na wananchi wengine kuwa yatima ni binadamu wenye uhitaji.

"Nitumie fursa hii kumpongeza mwenzetu Abubakar Allawi kwa kuwakumbuka watoto yatima katika futari hii,naomba wengine tujifunze hili maana dhawabu inayotokana na kusaidia yatima ni kubwa,"amesema.
Amesema,suala la kusaidia watoto yatima ni jukumu la kila mwanajamii pasipo kuangalia uwezo wa mtu na kwamba mtu yeyote anaweza kusaidia yatima kulingana na uwezo alionao.

"Hawa watoto yatima hawakupenda kuishi hivi, isipokuwa wapo katika mazingira haya kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo wazazi wao kufariki,na wengine kutelekezwa na hata mambo mengine mengi,hivyo niwaombe tuelekeze nguvu zetu kuwasaidia,"amesema Mtupa.

Kwa upande wake Mweka Hazina wa CWT, Abubakar Allawi amesema, kufuturisha ni tabia yake ya kila ifikapo mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kwamba ataendelea kufanya hivyo kadri Mungu atakavyomjaalia.
Allawi amesema, kuhusu watoto yatima amekuwa akiwaaalika kila mwaka katika futari hiyo, lakini amekuwa akiwatembelea watoto yatima kwa kuwapa misaada mbalimbali.

Hata hivyo, Allawi amewashukuru waumini hao pamoja na viongozi mbalimbali kwa kujitokeza kushiriki futari hiyo huku akisema hana cha kuwalipa zaidi ya kuwaombea kwa Mungu maisha marefu yenye mafanikio.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news