Swali la Mwandishi kutoka Afrika kwa Rais wa FIFA lazua gumzo

*Ni kuhusu sakata la Urusi kuivamia Ukraine na kuchomolewa Kombe la Dunia Qatar2022

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino ameshindwa kujibu swali la kichokonozi lililoulizwa na mwanahabari raia wa Ghana akitaka kufahamu sababu za shirikisho hilo kuingilia masuala ya kisiasa lilipoamua kuifungia Urusi kushiriki Kombe la Dunia nchini Qatar 2022.
Mwanahabari huyo, Gary Al-Smith ambaye anafanya kazi na Joy FM ya Ghana aliuliza swali hilo Alhamisi ya Machi 31,2022 ikiwa ni siku moja kabla ya droo ya Kombe la Dunia.

Al-Smith pia alitaka kufahamu, kwa uamuzi huo uliochukuliwa na shirikisho hilo kwa Urusi, Je? Kuanzia sasa itakuwa sera ya FIFA kwamba nchi yoyote itakayovamia nyingine itapigwa marufuku kushiriki michuano ya Kimataifa kama ilivyotokea kwa Urusi.

"Naitwa Gary Al-Smith, nafanya kazi na Joy FM ya Ghana, Ninakotoka Afrika tumezoea FIFA kutushukia sana linapokuja suala la kuingiliwa kisiasa kwenye maamuzi yanayohusu soka.

"Lilikuwa jambo la kufurahisha sana kwetu barani Afrika na nina hakika kwa watu wengi Ulimwenguni kuona FIFA ikitoa msimamo wake juu ya Urusi kutangaza kwamba kinachotokea ni uvunjifu wa haki linapokuja suala la uhusiano wa kibinadamu, lakini hatuoni jambo la namna hii katika maeneo mengine.

"Tumefikia hatua ambayo taifa moja linaposhambulia lingine au kuvamia, FIFA itachukua hatua au hii itakuwa kesi maalum kwa Urusi na Ukraine?,"alihoji huku zikisikika kelele za shangwe ukumbini.
Katika jibu lake kwa swali la Al-Smith, Rais wa FIFA Infatino alisema, shirikisho hilo linafanya kazi kila mahali na wanapaswa kuchukulia hali hiyo kwa namna sawa.

Mwezi Februari, mwaka huu Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), lilipiga marufuku Urusi kushiriki Kombe la Dunia nchini Qatar 2022, na mashindano mengine ya Kimataifa baada ya Rais Vladimir Putin kuivamia Ukraine.

Kutokana na uamuzi huo, Shirikisho la Soka la Urusi (RFU) katika taarifa yake lilikaririwa likisema kuwa, hatua hizo ni kinyume na viwango na kanuni zote za mashindano ya Kimataifa dhidi ya maadili ya ari ya michezo na haki ya kucheza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news