Tanzania, Burundi, Congo DR zatafuta fedha kujenga reli ya pamoja (SGR)

NA BENNY MWAIPAJA, Washington DC

NCHI za Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, zimewasilisha maombi ya kupatiwa mkopo wenye masharti nafuu kwenye Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Uvinza-Msongati- Gitega, yenye urefu wa Km 939, uliokisiwa kugharimu dola za Marekani milioni 900.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati), alizungumza jambo na Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Kidemokrasia Congo, Mhe. Nicolas Kazadi (kushoto) na Waziri wa Fedha na Uchumi wa Burundi, Mhe. Dkt. Domitien Ndihokubwayo, baada ya kikao chao na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Kanda ya Afrika Mashariki, Bi. Nnenna Nwabufo (hayupo pichani) kuhusu mkopo wa kujenga Reli ya Kisasa ya pamoja (SGR), katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Washington DC, nchini Marekani.

Majadiliano ya awali kati ya Benki hiyo na Mawaziri wa Fedha wa Nchi hizo tatu, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba wa Tanzania, Mhe. Nicolas Kazadi wa DRC na Mhe. Dkt. Domitien Ndihokubwayo wa Burundi, yamefanyika Washington DC, kando ya Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, Washington DC, nchini Marekani.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alisema kuwa reli hiyo ni muhimu kwa ustawi na maendeleo ya kiuchumi ya nchi zote tatu kwa sababu itakapokamilika itarahisha usafirishaji wa mizigo, abiria na kukuza biashara na maendeleo ya viwanda ya nchi hizo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Kidemokrasia Congo, Mhe. Nicolas Kazadi (kushoto) na Waziri wa Fedha wa Burundi, Mhe. Dkt. Domitien Ndihokubwayo, baada ya kikao chao na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kanda ya Afrika Mashariki, Bi. Nnenna Nwabufo (hayupo pichani) kuhusu mkopo wa kujenga Reli ya Kisasa ya pamoja (SGR), katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Washington DC, nchini Marekani.

Alisema kuwa, mradi huo ni mkubwa ndiyo maana nchi hizo zimekubaliana kutafuta mikopo nafuu kutoka vyanzo mbalimbali na pia kwa kutumia fedha zitakazotengwa kwenye bajeti zao za ndani ili mradi huo uanze kujengwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Kanda ya Afrika Mashariki Bi. Nnenna Nwabufo, alisema kuwa Benki yake inatambua umuhimu wa mradi huo kiuchumi, kisiasa na kijamii na kwamba utasaidia pia kuziunganisha nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki na ni muhimu kwa ajili ya utengamano wa nchi hizo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Kidemokrasia Congo, Mhe. Nicolas Kazadi, Waziri wa Fedha wa Burundi, Mhe. Dkt. Domitien Ndihokubwayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kanda ya Afrika Mashariki Bi. Nnenna Nwabufo (wa pili kulia) na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Emmanuel Tutuba (kushoto), baada ya kikao chao na AfDB kuhusu mkopo wa kujenga Reli ya Kisasa ya pamoja (SGR) ya Tanzania, Burundi na DRC, katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Washington DC, nchini Marekani.
Ujumbe wa Nchi tatu za Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC), ukiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Kanda ya Afrika Mashariki Bi. Nnenna Nwabufo (wa sita kulia), baada ya majadiliano ya kupata mkopo kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) inayoziunganisha nchi hizo tatu, katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Washington DC, nchini Marekani.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango-Washington DC).

Aliahidi kuwa Benki yake itashiriki kikamilifu kuhakikisha kuwa mradi huo unajengwa kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo pamoja na maendeleo ya kiuchumi ya nchi zinazoshiriki katika kujenga mradi huo muhimu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news