Ufaransa yaahidi mema zaidi kwa Tanzania

NA GODFREY NNKO

SERIKALI ya Ufaransa imeahidi kuendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa fupi iliyoonwa na DIRAMAKINI BLOG kutoka kwa Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Mheshimiwa Nabil Hajlaoui ikielezea kuhusu maadhimisho ya Miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambayo huwa yanaadhimishwa kila ifikapo Aprili 26, ya mwaka.

"Siku moja baada ya kuadhimisha Miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Balozi Nabil Hajlaoui anayo furaha kutoa pongezi za dhati kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Serikali yake na Watanzania wote.

"Ziara ya Rais (Samia Suluhu Hassan) nchini Ufaransa mwezi Februari uliopita, imehuisha na kuimarisha uhusiano kati ya Ufaransa na Tanzania. Ufaransa imedhamiria kufanya kazi na Tanzania kwa karibu zaidi ili kuimarisha ushirikiano na kukabiliana vema na changamoto zinazojitokeza katika Pwani ya Mashariki ya Afrika na katika Bahari ya Hindi,"imeeleza sehemu ya taarifa hiyo kutoka kwa Balozi Nabil wa Ufaransa nchini Tanzania.

Rais akiwa Ufaransa

Kupitia ziara hiyo ya nchini Ufaransa mwezi Februari, mwaka huu Watanzania walishuhudia neema nyingi kutoka huko ambazo zinalenga kuchochea kasi ya ukuaji wa maendeleo nchini.

Mheshimiwa Rais Samia akiwa mjini Brest nchini Ufaransa alishuhudia utiaji saini mikataba sita ya makubaliano katika uendelezaji uhusiano kati ya Tanzania na Ufaransa ukiwemo mkopo wa ujenzi wa Barabara ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) wenye thamani ya Euro milioni 178.

Mkopo huo wa masharti nafuu unalenga kugharamia ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka ikiwa ni miongoni mwa miradi ambayo inatajwa kuwa na manufaa makubwa katika sekta ya usafrishaji jijini Dar es Salaam.

Tayari mradi huo umekamilika awamu ya kwanza, huku awamu ya pili ambayo inaendelea ujenzi wake ukiwa unahusisha Barabara ya Kilwa kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam kwenda Mbagala Rangi Tatu na kipande cha Barabara ya Kawawa kwenye makutano ya Barabara ya Morogoro kwenda Mgulani katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke. Zote zikiwa na urefu wa kilomita 20.3 ambapo gharama zake ni zaidi ya Euro milioni 160.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Dkt.Edwin Mhende wakati huo alikaririwa akisema kuwa, awamu ya tatu ya mradi huo itahusisha ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka katika Barabra ya Nyerere kuelekea Gongolamboto ikiwa na urefu wa kilomita 23.6.

Aidha, Taifa la Ufaransa ambalo ni miongoni mwa washirikka wa karibu wa Tanzania wenye uhusiano wa muda mrefu, kulingana na taarifa za mwaka 2020 zilionesha kuwa, kiwango cha biashara baina ya pande hizo mbili kilifikia zaidi ya dola milioni 150.

Kupitia kiwango hicho, asilimia 90 ya mauzo ya Ufaransa nchini Tanzania yalijikita katika maeneo ya vifaa vya umeme,kielektroniki,mawasiliano na teknolojia na mitambo mbalimbali.

Wakati huo huo kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2021, mauzo ya bidhaa za Tanzania nchini Ufaransa hususani mazao ya misitu, uvuvi,vyakula na nyinginezo yalifikia dola milioni 18.8.

Wakati huo huo, katika ziara hiyo ya Mheshimiwa Rais Samia nchini Ufaransa alishuhudia utiaji saini mkataba wa masharti nafuu wa Euro milioni 80 ambao unalenga kuimarisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili iweze kufikia malengo ya kutoa mikpo ya muda mfupi na muda mrefu katika sekta hiyo muhimu hapa nchini.

Pia kwa upande wa Uchumi wa Buluu na Usalama wa Bahari,mkataba wa ushirikiano katika eneo hilo ulisainiwa ili kuiwezesha sekta hiyo kuleta matokeo makubwa nchini.

Post a Comment

0 Comments