Vijana:Handeni kuna uhuru zaidi ya hapa Ngorongoro, tusiwasikilize wapotoshaji

NA DIRAMAKINI

VIJANA wanaoishi ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wameshauriwa kuacha kujiingiza kwenye makundi ambayo yanasababisha kuwepo migogoro katika zoezi la wao kuhama ndani ya hifadhi kwa kuwa wapo watu wenye maslahi na migogoro hiyo.Akizungumza wilayani humo mmoja wa wakazi wa Ngorongoro, Lucas Tiamos amesema kuwa, wapo vijana wa eneo hilo wanashawishiwa kujiingiza kwenye makundi ya watu ambao kwa namna moja au nyingine wanapata manufaa huku wao wakiwa hawapati kitu.
Lucas amesema kuwa, ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro hakuna uhuru wa kutosha wa kuweza kufanya shughuli za kimaendeleo,hivyo zoezi linalofanywa na serikali la kutaka kuwahamisha ni suala la msingi kwa maslahi yao.

"Mimi nimeshajiandikisha kwa ajili ya kuhamia Handeni hapa Ngorongoro hakuna uhuru wa kuweza kulima wala kujenga nyumba ya kudumu,lakini Handeni tunapewa nyumba na hati ya kiwanja ukiachilia suala la ekari nane,tatu za makazi na tano za kilimo na mifugo kwetu ni uhuru huu,"amesema Lucas.
Aidha, mkazi wa Madukani, Endulen Phoibe Lukumai ameongeza kuwa licha ya kuishi ndani ya hifadhi hiyo,bado usalama wao ni mdogo, kwani vinatokea vifo vya mara kwa mara kwa wananchi kuliwa na wanyama wakali,lakini pia wengine husogea karibu kabisa na makazi na kihatarisha usalama wao.

Amesema, yeye binafsi anaona kama serikali ilichelewa kufanya maamuzi hayo,hivyo yupo tayari kuhama muda wowote kwenda Handeni kwenye hayo makazi mapya,ambapo anaamini serikali imetenga eneo salama na wataweza kuishi bila wasiwasi.

Hata hivyo, Paulo Mamasita mkazi wa Oloirobi kwa upande wake ameongeza kuwa, anaiona faida ya kubadili makazi kwenda mapya, kwani watapata faida ikiwemo kuweza kumiliki maeneo,kulima na kujiendeleza kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi huku wakipatiwa hati miliki za ardhi.
"Tunachokiomba kutoka serikalini ni kuboreshewa miundombinu ya maji,umeme,barabara,shule,afya na mahitaji yote muhimu yawepo na tumepata taarifa kwamba wataboresha,hivyo sisi tupo tayari kuondoka kwenye hifadhi kama serikali ilivyoona kuna umuhimu wa kufanya hivyo kwa maslahi ya taifa letu,hapa hatumiliki hati za ardhi ila kule tutapewa,"amesema Paulo.

Mkazi mwingine Saning'o Laizer amesema, ameshakwenda Handeni na kuona mazingira yake hivyo hawezi kupata shida kama ilivyo hapo Ngorongoro, kwani huingia na kibali,ila wanapokuwa Handeni katika eneo la Msomera hayo mambo hayatafanyika ya kila kitu lazima kuwa na kibali

Ameongeza kuwa, ndani ya hifadhi hiyo hakuna ruhusa kukamiti ila bila kibali ila wakiwa ndani ya Handeni watasaidiana na wenyeji kutunza mazingira lakini pia uhuru wa kufanya shughuli za kilimo na ufugaji utakuwepo.
Mpaka mwezi uliopita nyumba 103 zilikuwa kwenye hatua mbalimbali za ujenzi katika Kijiji cha Msomera kilichopo wilayani Handeni mkoani Tanga,kwa ajili ya kuhamia wananchi kutoka Ngorongoro huku lengo la serikali likiwa ni kuhifadhi mazingira ya eneo hilo yasiharibike zaidi kutokana na wingi wa mifugo uliopo ndani yake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news