Watendaji wa kata Kasulu wapewa pikipiki

NA RESPICE SWETU

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, imetoa pikipiki 10 kwa watendaji wa kata zilizonunuliwa kutokana na pesa za Mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi pikipiki hizo, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isack Mwakisu, amewataka watendaji wa kata waliokabidhiwa pikipiki hizo kuzitunza na kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuongeza tija na kuboresha utendaji kazi.
Mwakisu aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo amesema, watendaji hao wanapaswa kujiepusha na matumizi yasiyo sahihi watakapokuwa na pikipiki hizo ikiwa ni pamoja na kuendesha bila leseni.

Amesema, kumekuwepo na taarifa kuwa ajali nyingi za barabarani zinazotokea nchini, husababishwa na madereva wanaoendesha vyombo vya serikali hivyo hatarajii kuiona hali hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Joseph Kashushura, ameonesha matumaini makubwa kuwa, kununuliwa kwa pikipiki hizo, kutaboresha ukusanyaji wa mapato na kurahisisha ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo iliyopo kwenye vijiji na kata za halmashauri hiyo.

"Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu imekuwa ikitekeleza maelekezo ya serikali kuhusu kutumia sehemu ya pesa zitokanazo na mapato ya ndani katika maeneo mbalimbali ikiwemo kulipa posho za watendaji wa kata, sisi tumekwenda mbali zaidi kwa tunawanunulia na pikipiki,"alisema.

Kashushura alizitaja kata zilizopata pikipiki hizo kuwa ni Kitanga, Asante Nyerere, Kwaga, Kurugongo, Kalela, Kigembe, Shunguliba, Heru Ushingo, Titye na Makere na kuahidi kuwa zitanunuliwa pikipiki nyingine kwa kata zilizobaki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news