Waziri Mkuu:Tushirikiane kutoa elimu kuhusu dawa za kulevya

*Asema Programu ya Kukuza Ujuzi imeanza kuwaneemesha waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu

NA GODFREY NNKO

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa ameomba wadau wote kushirikiana kwa nguvu zote katika kutoa elimu kuhusu dawa za kulevya nchini.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo Aprili 6,2022 bungeni jijini Dodoma wakati akitoa hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge kwa mwaka 2022/2023.

"Nitoe wito kwa wadau wote mkiwemo waheshimiwa wabunge wenzangu, asasi za kiraia, viongozi wa dini, vyombo vya habari na jamii nzima kushirikiana na Serikali kutoa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya nchini,"amesema Mheshimiwa Majaliwa.

Pia amesema, Serikali imeimarisha huduma za matibabu kwa watumiaji wa dawa za kulevya kwa kuongeza idadi ya kliniki zinazotoa huduma kwa waathirika wa dawa za kulevya kutoka tisa mwaka 2020/2021 hadi kliniki 15 zinazohudumia waathirika zaidi ya 10,600 mwaka 2021/2022.

"Licha ya hayo, Serikali kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi imewezesha waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu wapatao 200 kupata mafunzo ya ujuzi kupitia vyuo vya VETA na SIDO,"amesema.

Katika hotuba hiyo, Waziri Mkuu ameliomba Bunge kuidhinisha shilingi bilioni 148.9 kwa ajili ya matumizi ya ofisi yake na taasisi zake kwa mwaka 2022/23, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 101.36 zitaenda kwenye matumizi ya kawaida na zaidi ya shilingi bilioni 47.5 zitaenda kwenye miradi ya maendeleo.

Aidha, kwa upande wa Bunge, Waziri Mkuu ameomba kuidhinishiwa zaidi shilingi bilioni 132.7 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge kati ya fedha hizo shilingi bilioni 127.3 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 5.4 ni kwa ajili ya maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news