Bernard Morrison mikononi mwa polisi

NA DIRAMAKINI

MCHEZAJI wa Kimataifa wa Klabu ya Simba,Wakili Msomi Bernard Morrison anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Chang’ombe kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam kwa madai ya kumjeruhi shabiki wa Yanga na kitu chenye ncha kali.
Mkuu wa Kituo cha Polisi Chang’ombe, ASP Mohammed Simba amethibitisha kupokea kesi hiyo baada ya Derby ya Kariakoo iliyopigwa Aprili 30,2022 katika dimba la Benjamin Mkapa.

“Ndio tumepokea hiyo kesi na tunaendelea na mahojiano tukikamilisha tutawajulisha,”ameeleza kwa kifupi ASP Simba. 

Katika mtangane huo Simba SC wametoa sare ya bila mabao na vinara wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Yanga SC.
Ulikuwa ni mtanange wa aina yake ambao umepigwa Aprili 30, 2022 katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Beki Henock Inonga Baka (Varane) wa Simba na mshambuliaji, Fiston Kalala Mayele wa Yanga ndiyo walioonekana kunogesha mtanange huo kwa namna ambavyo wamepambana dimbani.

Aidha, kama ilivyokuwa kwenye mechi ya kwanza ya ligi, Inonga alimdhibti vyema Mayele, kinara wa mabao Ligi Kuu ambaye muda wote wa mchezo alipiga shuti moja tu lililogonga nyavu za pembeni, nje kulia kipindi cha pili.

Simba SC ndio pekee waliofanya jaribio la hatari lililolenga lango,ni baada ya mshambuliaji Chris Kope Mutshimba Mugalu kuunganishia mikononi mwa kipa Djigui Diarra mpira wa adhabu wa beki Shomari Kapombe kipindi cha pili pia.

Pia mtanange huo ulikuwa wa kukamiana na kuonyeshana ubabe baina ya wachezaji wa pande zote mbili.

Refa chipukizi, Ramadhani Kayoko alionekana kuumudu vilivyo mtanange huo licha ya makosa machache ya kibinadamu aliyoyafanya.

Post a Comment

0 Comments