BoT yawakutanisha wasomi Kumbukizi Miaka 100 ya Mwalimu Nyerere, wafunguka yasiyofahamika

NA GODFREY NNKO

IMEELEZWA kuwa,ni vigumu kutenganisha historia ya Tanzania na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwani kabla na baada ya Uhuru alifanya mambo mengi ambayo yamebaki katika kumbukizi muhimu kwa Watanzania na mataifa ya kigeni.

Mbali na hayo falsafa za Mwalimu Nyerere za Utu, Usawa, Haki na Ujamaa zimetajwa kuwa ni nyezo muhimu za kuimarisha na kujenga amani hapa nchini na Bara la Afrika na zisipozingatiwa kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Hayo yamebainishwa katika Kongamano la Kumbukizi ya Miaka 100 ya Kuzaliwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere katika mtazamo wa kiuchumi chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na uchambuzi wa vitabu lililofanyika kwenye ukumbi wa benki hiyo jijini Dar es Salaam.

Taasisi nyingine zilizoshiriki katika kongamano hilo ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Taasisi ya Mkuki na Nyota, ambapo mada mbalimbali zilijadiliwa ikiwemo vitabu vitatu vilivyoandika wasifu wake, vilivyozinduliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Awali mchapichaji wa vitabu, Walter Bgoya amesema, alibahatika kufanya kazi katika miaka miwili ya mwisho wa maisha yake, Mwalimu Nyerere alilipa kipaumbele suala la utu, usawa na haki katika kukuza amani na utulivu nchini, kwa sababu kusipozingatiwa kunaweza kuleta uvunjifu wa amani au vita katika Afrika.

Bgoya amesema, kutokana na kuendelezwa maono ya Mwalimu Nyerere, Tanzania imekuwa mahali salama na kimbilio la nchi rafiki za Afrika wakati wanapopata shida kwao kama nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na nyinginezo.

"Na kuna wakati,Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alisema Tanzania ndio bima yao pale inapotokea shida katika mataifa yao,"amesema.

Akielezea kwa ufupi kuhusu wasifu wa Hayati Baba wa Taifa, Prof. Issa Shivji amesema,kamwe hauwezi kutenganisha historia ya Tanzania na Mwalimu Nyerere.

"Hauwezi kabisa, Mwalimu Nyerere ataendelea kubaki kuwa Mwalimu, ni miongoni mwa watu ambao walifanikisha mtazamo wa kihistoria ambao unaagazia mapambano ya watu kutengeneza historia. Mwalimu Nyerere alitaifisha mabenki mwaka 1967 ili kuweka uchumi vizuri, ambapo mengine yalikuwa madogo na makubwa, lakini NBC ilikuwa ikifanya vizuri,"amesema.

Alieleza kubinafisha huko kulitokana na Azimio la Arusha mwaka 1967 katika kujenga uwiano na usawa wa kiuchumi katika nchi, kupitia taasisi za fedha katika mabenki pamoja na Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambalo lilitaka kubadilisha muelekeo wa Baba wa Taifa, katika kujikwamua na uchumi tegemezi.

Tujikumbushe

Mwaka 1967, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliasisi na kusimamia utekelezaji wa Azimio la Arusha likiwa na miiko ya uongozi wa umma ambayo pia alitaifisha rasilimali zote za binafsi na kuzifanya kuwa za Serikali.

Wakati huo kulikuwa na shule, hospitali na mashirika binafsi, yote yakawa ya Serikali. Hatua zote hizo zilikuwa ni utekelezaji wa sera ya Ujamaa na Kujitegemea. Ni sera ambayo haikuzifurahisha nchi za Magharibi zilizoamini katika Ubepari.

Aidha, licha ya kumshauri mara kadhaa,Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere hakubadili mawazo yake huku akionesha misimamo mikali dhidi ya nchi za Magharibi.

Mwalimu alijikita kwenye ukombozi wa nchi za Afrika ambazo wakati zilikuwa bado hazijapata uhuru. Na wakati mwingine alilazimika kutumia hata rasilimali za nchi kufanikisha ukombozi huo.

Wakati huo kulikuwa na nchi kama Afrika Kusini, Namibia, Msumbiji, Angola na Zimbabwe wapigania uhuru wake walipatiwa makazi nchini.

Uasi

Naye Prof. Saida Yahya-Othman amesema, Hayati Mwalimu Nyerere alikuwa muasi tokea akiwa mdogo ambapo alijikitia kupinga ukandamizaji na dhuluma zilizokuwa zimewekwa na wakoloni katika maeneo mbalimbali ya shule,
makanisani na vyuoni.

Amefafanua kuwa, uasi ambao aliufanya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere haukuwa kwa manufaa yake, bali kwa manufaa ya jamii na ustawi bora wa Taifa likiwemo Bara la Afrika kwa ujumla.

Amesema,wakati Mwalimu Nyerere anasoma Chuo Kikuu cha Makerere Uganda wanawake hawakudahiliwa, hali iliyomfanya aandike kitabu cha Huru wa Wanawake, kwa ajili ya kupinga vikali mila potofu dhidi ya wanawake.
Prof.Yahya akichambua Kitabu cha Development as Rebellion: A biography of Julius Nyerere, amesema Mwalimu Nyerere aliendelea kuwa muasi kutokana na upinzani aliokutana nao ndani na nje ya mfumo dhidi ya imani yake katika usawa, haki na maendeleo.

“Hata leo pia tunao waasi wastaafu na waasi watarajiwa, Mwalimu alikuwa na misimamo tofauti katika familia yake, shuleni, kanisani na serikali ya kikoloni,akitaka usawa, haki na maendeleo ya watu,”amesema na kutaja uasi ulioandikwa katika kitabu hicho kuwa ni pamoja na uasi wa kujiuzulu mara tatu ikiwemo nafasi ya uwaziri mkuu, uasi wa lugha ya kigeni na kuamini lugha ya Kiswahili.

Profesa Yahya amesema, pia Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliasi mfumo wa kibepari na kuzindua wazo la Azimio la Arusha huku akiasi mfumo wa elimu akiamini elimu ya kujitegemea ikiwemo tamaduni za viongozi kukandamiza wanafunzi, kabla ya kuasi mifumo dume iliyokandamiza mwanamke.

“Aliandika kitabu cha kupiga vita mfumo wa kukamdamiza mwanamke, lakini hakukitoa kwa sababu ilikuwa ni kutia petroli sana kwa mwanaume kutetea hilo, kwa hiyo tusome hiki kitabu,”amefafanua Prof. Yahya huku akibainisha kuwa,Mwalimu Nyerere pia alikuwa muasi hata katika mavazi ya suti za kikoloni na kutumia kaunda suti huku akilaani viongozi wa Afrika kuongoza kwa utamaduni wa kutukuzwa na mambo mengine.

Profesa Yahya amesema, Mwalimu Nyerere alifanya hvyo, licha ya kukumbana na upinzani mkali, lakini jambo ambalo lilimsaidia kushinda hayo yote ulikuwa ujasiri na kipawa cha kipekee katika uongozi.

Wakati huo huo, Profesa Yahya amewataka waandishi wa vitabu kutambua kuwa, uandishi huo unahitaji kutafiti na si kujiandikia kitabu tu ndani ya siku chache kimeisha.

Amefafanua kuwa, kutafiti kwa kina na kuandika kitabu kutaendelea kuwapa hamasa wasomaji wa vitabu nchini kuendelea kujisomea kwa kuwa licha ya kujisomea kama sehemu ya utaratibu waliojiwekea pia watakuwa wanajifunza mambo mapya kila wakati.

Dkt.Kamata

Kwa upande wake Dkt. Ng’wanza Kamata amesema kuwa, Hayati Baba wa Taifa alipitia nyakati nyingi kabla na baada ya Uhuru na kote huko alishinda.

"Mwalimu Nyerere alikuwa anapata upinzani mkubwa na vitisho vingi. Wakati mwingine alijibu kwa ukali na alifanikiwa kushinda kwa sababu alikuwa na uwezo wa kipekee,"amesema.

BoT

Mapema akifungua kongamano hilo, Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga amesema BoT inaendelea kumuenzi Mwalimu Nyerere katika maono yake.
Pia amesema, alikuwa na maono katika uchumi, kijamii katika kuendesha nchi ambapo vitabu vitatu vya kuhusu Mwalimu Nyerere vinaangazia kwa kina kuhusu maisha yake, falsafa zake na uchambuzi. 

Amesema, huu ni mwanzo wa maandalizi wa makongamano mengine ambayo huko mbeleni yanaweza pia kuwakutanisha pamoja waandishi wa vitabu vya uchumi ili kutoa uwanda mpana wa kukaa, kujadili na kutafakari pamoja.

Nao washiriki wa kongamano hilo walisema usomaji wa vitabu umekuwa changamoto sasa, ambapo watu wengi wanatumia 'soft copy' kwa kuona vitabu vinawapotezea muda.

Walishauri watengeza vitabu wafanya katika documentary au soft copy ili kuweza kuwafaidisha wasomaji wengi zaidi.

Mfuko wa Udhamini

Akizungumzia kuhusu Mfuko wa Udhamini wa Elimu ya Juu wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius K. Nyerere (Mwalimu Julius K. Nyerere Memorial Scholarship Fund),Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Yamungu Kayandabila anasema,ulianzishwa na Benki Kuu tarehe 12 Oktoba, 2009 kwa ajili ya kuenzi mafanikio ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika sekta ya elimu.

"Mfuko huu ulianza kwa kuchangiwa fedha na Benki Kuu ya Tanzania na taasisi zingine za fedha, viongozi wastaafu, wafanyakazi wa Benki Kuu na wananchi wengine kupitia harambee.

"Fedha hizo ziliwekezwa kwenye Dhamana za Serikali (Treasury Bill na Bond) ili mfuko uwe endelevu na faida inayopatikana tu ndiyo inayotumika kufadhili wanafunzi katika vyuo vikuu hapa nchini.

Anasema, ufadhili huo unatarajia kuongeza hamasa kwa wanafunzi wa kike hapa nchini wenye ufaulu wa juu katika masomo ya Hisabati na Sayansi, ili kujiendeleza kwenye masomo ya shahada na uzamili.

"Hii ni kwa sababu idadi ya wanafunzi wa kike kwenye masomo hayo imekuwa chini kwa muda mrefu. Hivyo ilichukuliwa wanafunzi kike kama kundi lenye uhitaji.

"Ufadhili huu utasaidia kuhamasisha wanafunzi hasa wa kike kufanya vizuri kwenye masomo hayo, na hivyo kuleta usawa au uwiano wa kijinsia kitaaluma kwenye masomo haya muhimu yanayochangia maendeleo ya taifa,"anasema

Anasema, ufadhili huo unajumuisha gharama zote za ada, pesa za kujikimu,mafunzo ya vitendo na vifaa vya kujifunzia ikiwemo kompyuta mpakato (laptop).

Anaendelea kufafanua kuwa,ufadhili unatolewa kwa wanafunzi raia wa Tanzania wenye ufaulu wa kiwango cha juu waliosajiliwa vyuo vikuu nchini vinavyotambulika na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Naibu Gavana huyo anasema, asilimia 50 ya ufadhili wa masomo Shahada ya Kwanza ni kwa ajili ya wanafunzi wa kike tu kwa masomo ya Hisabati na Sayansi.

Huku asilimia 50 nyingine ya ufadhili kwa masomo ya Shahada ya Kwanza ikiwa ni kwa wanafunzi wa kike na kiume katika Masomo ya Hisabati, Sayansi, Uchumi, TEHAMA, Uhasibu na Fedha.

"Ufadhili kwa masomo ya Shahada ya Pili (Uzamili) unawalenga wanafunzi wa kike na kiume katika masomo ya Hisabati, Sayansi, Uchumi, TEHAMA, Uhasibu na Fedha,"anaeleza

Vigezo

Anasema, vigezo vya udhamini kwa shahada ya kwanza ambapo asilimia 50 ya ufadhili inawahusu wanafunzi wa kike raia wa Tanzania, wanapaswa kuwa na ufaulu wa juu wa daraja la kwanza miongoni mwa wanafunzi kumi bora kitaifa wa kidato cha sita kwenye masomo ya Hisabati na Sayansi kwa mwaka husika.

"Pia wawe wamepata udahili kwa masomo ya shahada ya kwanza fani za Hisabati na Sayansi katika vyuo vilivyopo nchini (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) na vinavyotambulika na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU),"anasema

Wakati huo huo akizungumzia, vigezo vya udhamini kwa Shahada ya Uzamili (Master’s Degree) anasema kuwa, inawahusu wanafunzi wa kike na wa kiume raia wa Tanzania wenye umri usiozidi miaka 35.

Anasema, wanafunzi hao wanapaswa wawe wenye ufaulu wa juu katika shahada ya kwanza (GPA 4.0 na zaidi) kwa kozi za Hisabati, Sayansi, Uchumi, TEHAMA, Uhasibu na Fedha.

Pia wawe wamepata udahili wa kusoma fani hizo katika vyuo vilivyopo nchini (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) na vinavyotambulika na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).

Muundo

Akizungumzia kuhusu muundo wa uendeshaji wa mfuko anasema, ili kuhakikisha kuwa udhamini unatolewa kwa ufanisi, mfuko unaendeshwa na Bodi ya Wadhamini (Board of Trustees) inayoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ambaye ni Gavana wa Benki Kuu, yenye jukumu la kutoa mwongozo wa shughuli za mfuko kwa kuzingatia sera za mafunzo nchini.
Wengine ni Kamati ya Kutoa Udhamini (Scholarship Awards Committee) inayosimamia mfuko,kuratibu utoaji wa udhamini na kupendekeza kwa Bodi ya Wadhamini.

"Pia Sekretarieti ni sehemu ya majukumu ya Benki Kuu inayoratibu utekelezaji wa kazi za mfuko pamoja na kutoa ripoti mbalimbali.Na kuna Mweka Hazina wa Mfuko (Fund Treasurer).

"Wajumbe wengine wa Bodi (Board of Trustees) pamoja na Kamati (Scholarship Awards Committee) za mfuko ni pamoja na Naibu Gavana (EFP) na Viongozi wengine toka Benki Kuu ya Tanzania akiwemo mwakilishi toka Taasisi ya Mwalimu Nyerere, mwakilishi toka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (Tanzania Bara).

"Mwakilishi toka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (Zanzibar),Mwakilishi toka Chama cha Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), Mwakilishi toka Tume ya Vyuo Vikuu (TCU),Mwakilishi toka Bodi ya Mikopo ya Elimu (HESLB) na Mwakilishi toka Familia ya Mwalimu Nyerere,"anasema.

Mafanikio

Anasema, tangu kuanzishwa kwa mfuko huo jumla ya wanafunzi wa Kitanzania 62 wamepata ufadhili.Anasema, kati yao 43 ni wanawake na 19 ni wanaume ambapo kati yao wanafunzi 16 wamepata ufadhili wa masomo ya fani ya udaktari.

Benki inawafuatilia

Naibu Gavana huyo amesema, benki imekuwa ikifuatilia maendeleo ya wanafunzi wanufaika wanaofadhiliwa na mfuko kwa kuomba taarifa za maendeleo (academic progress) toka vyuoni kila baada ya muhula kuisha.

"Ufuatiliaji unafanyika ili kuhakikisha wanufaika wa mfuko wanasoma kwa bidii na wanapata ufaulu wa juu, ambao si chini ya alama ‘B’.Pia wanasoma kozi iliyoidhinishwa kwa ufadhili tu, na wanakuwepo chuoni na kuhudhuria masomo muda wote,"anasema.

Wanufaika

Baadhi ya wanufaika wa masomo kupitia mfuko huo wameishukuru Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuja na wazo hilo la kumuezi Baba wa Taifa kwa kutoa udhamini wa masomo kwa wanafunzi mbalimbali nchini, kwani mbali na kuwapa motisha ikiwemo kugharamia gharama zote pia baada ya kuhitimu wamekuwa wakipandishwa madaraja kazini.

Wamesema, umefika wakati kwa taasisi nyingine za binafsi na umma kuiga mfano huo wa BoT ili kuweza kuwafikia wanafunzi wengi zaidi nchini. Wafuatao hapa chini ni sehemu ya wanufaika wa mfuko huo;Post a Comment

0 Comments