BRELA inajivunia mafanikio makubwa kidigitali yaliyoongeza uwazi, ukuaji uchumi nchini-Afisa Mtendaji Mkuu

NA GODFREY NNKO

AFISA Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw.Godfrey Nyaisa amesema kuwa, usimamiaji wa majukumu ya wakala huo umewezesha kuwa na mafanikio makubwa yenye uwazi na ukuaji wa uchumi nchini.
Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa akizungumza Mei 21,2022 katika kikao kazi cha siku mbili na wahariri wa vyombo vya habari mkoani Morogoro.

Nyaisa ameyasema hayo Mei 21, 2022 mkoani Morogoro wakati akitoa neno katika kikao kazi cha siku mbili kati ya BRELA na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Amesema,hali hiyo inatokana na uboreshaji wa mazingira ya biashara na urahisishaji wa sajili na leseni zinazotolewa na BRELA hapa nchini.

"Mafanikio haya yametokana na utekelezaji wa mikakati mikuu ya Kitaifa, Sera na Mpango wa Maendeleo wa Taifa,"amesema Bw.Nyaisa.

Kuhusu BRELA

Afisa Mtendaji Mkuu huyo amesema kuwa, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ilianzishwa chini ya Sheria ya Wakala za Serikali Na.30 ya mwaka 1997 na kuzinduliwa rasmi Desemba 3, 199 chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara na sasa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.
Mkuu wa Kitengo cha habari na Elimu kwa Umma (BRELA),Bi.Rhoida Andusamile akizungumza alipokuwa akiongoza ratiba ya kikaokazi hicho cha siku mbili kinachofanyika mkoani Morogoro. 

"BRELA imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria inazozisimamia ambazo ni Kusajili Makampuni (The Companies Act.212),Kusajili Majina ya Biashara (The Business Names Act, Cap.213 R.E 2002),Kusajili Alama za Biashara na Huduma (The Trade and Services Marks Act,Cap.326 R.E.2002),

"Majukumu mengine ni Kutoa Hataza (The Patents (Registration)Act,Cap.217 R.E.2002), Kutoa Leseni za Viwanda (The National Industries (Licencing and Registration) Act, Cap 46 R.E.2002) na Kutoa Leseni za Biashara Kundi A (The Business Licensing Act, Cap.208 R.E.2002),"amefafanua Bw.Nyaisa.

Mifumo

Anabainisha kuwa, mwaka 2018, BRELA ilianzisha rasmi mfumo maalum wa sajili na utoaji wa leseni kwa njia ya mtandao (Online Registration System-ORS) na mwaka 2019 walianzisha mfumo wa National Business Portal (NBP) ambao ni maalum kwa utoaji wa leseni za biashara kundi A.

"Uwepo wa mifumo hiyo umesaidia taasisi kuhama kwenye utendaji kazi kwa njia ya makaratasi na kuwa kidijitali, lakini zaidi mifumo hiyo imewezesha taasisi kufanya kazi kwa uwazi katika kutoa huduma kwa wateja,"amesema.

Pia amefafanua kuwa, mifumo hiyo imesaidia kuondoa kero na changamoto zilizokuwa zinajitokeza na hatimaye kufanikisha kujenga mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara nchini.

Sajili na leseni

Bw.Nyaisa anasema kuwa, mbali na mifumo ya ndani ambayo inaendelea kufanyiwa maboresho siku hadi siku, BRELA imeweza kuunganisha sajili na leseni kwenye mifumo ya taasisi nyingine ili kupunguza urasimu kwa wafanyabiashara.

"Mfano, BRELA imejiunga na Mfumo wa Utoaji wa Vitambulisho vya Taifa (NIN) unaosimamiwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ambapo mfanyabiashara hatahitajika kuleta uthibitisho wa kitambulisho cha Taifa, BRELA pia imeunganishwa na mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambapo kwa sasa namba ya usajili wa kampuni ndio namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN),"amebainisha Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA.

Ushirikiano

Wakati huo huo, Bw.Nyaisa amesema kuwa, ushirikiano na taasisi zingine umewezesha kuwa na matokeo chanya kwenye kusogeza utoaji wa huduma bora kwa wateja.
"Mfano BRELA inashirikiana na mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuwajengea uwezo maafisa biashara ili kuelewa namna ya kutoa usaidizi kwa wafanyabiashara waliopo ngazi za wilaya hasa kwa upande wa sajili na utoaji wa leseni kwa njia ya mtandao,"ameeleza.

Pia amesema, BRELA imeweka dawati la utoaji huduma kwa wageni wanaofika nchini kwa lengo la kuwekeza. "Dawati hilo la usaidizi lipo kwenye Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambapo Afisa wa BRELA ana jukumu la kuhakikisa kila mgeni mwenye nia ya kuwekeza nchini anapata usaidizi wa haraka na kwa wepesi,"amesema Bw.Nyaisa.

Afisa Mtendaji Mkuu huyo amefafanua kuwa, BRELA kwa kushirikiana na Shirika la Posta Tanzania chini ya Program Maalum ya Huduma Pamoja inayosimamiwa na shirika hilo imeweka dawati la kutoa huduma kwa wananchi.
"Hii ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kuweka mazingira rahisi na wezeshi kwa wananchi kupata huduma zote za Serikali ndani ya eneo moja na kwa muda mfupi, pia ikiwa ni kusukuma maendeleo katika sekta ya mwasiliano kwa kupunguza msongamano na usumbufu kwa wananchi,"amefafanua Bw.Nyaisa.

Elimu

Katika hatua nyingine, Bw.Nyaisa amesema kuwa, BRELA imeendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara na umma kwa ujumla kuhusu huduma zinazotolewa na wakala na taratibu za utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

Aidha, Afisa Mtendaji Mkuu huyo ametumia nafasi hiyo kuvishukuru vyombo vyote vya habari hapa nchini kwa kuendelea kutoa habari mbalimbali zinazohusu BRELA.

"BRELA inavitambua vyombo vya habari kama moja ya wadau wake muhimu ndio maana hata kwenye mkataba wa huduma kwa mteja unaeleza kuwa, vyombo vya habari vina haki ya kupata taarifa kwa muda usiozidi siku mbili,"amesema.

Changamoto

Bw.Nyaisa amesema kuwa, BRELA imekuwa ikikumbana na changamoto katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo uelewa mdogo wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
"Changamoto hizi ni pamoja na uelewa mdogo wa matumizi ya TEHAMA kwa baadhi ya wateja tunaowahudumia hasa maeneo ya wilayani na vijijini.

"Pia uelewa mdogo wa wananchi kuhusu sheria mbalimbali za wakala, jambo linalowalazimu kutumia watu wa kati (vishoka) ambao pia hawana weledi hivyo kusababisha usumbufu kwa wafanyabiashara,"amefafanua Bw.Nyaisa.

Post a Comment

0 Comments