NAIBU WAZIRI ATAKA ELIMU KUHUSU SHERIA YA MADINI ITOLEWE KWA WACHIMBAJI

NA STEVEN NYAMITI-WM

NAIBU Waziri wa Madini, Dkt.Steven Kiruswa amemuagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida kutoa elimu kuhusu Sheria ya Madini kwa wachimbaji wadogo wa madini ili waweze kuchimba kwa tija.
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Kiruswa akiwa na wachimbaji wadogo wa madini Mkoani Singida.

Amesema hayo Machi 14, 2022 alipotembelea na kuzungumza na wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Matongo kilichopo Wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida.

Ni baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wachimbaji wa Kijiji cha Matongo kuwa hawaelewi Sheria za Madini zilizopo jambo linalowapa changamoto katika utekelezaji wa shughuli za uchimbaji katika maeneo yao.

Aidha, ameiagiza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuhakikisha wanafanya utafiti katika kijiji hicho ili wachimbaji wachimbe kwa tija.
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa,akizungumza na wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Matongo kilichopo Wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida.

Wakati huo huo,Dkt.Kiruswa ametoa wito kwa sekta za kifedha zikiwemo benki kutembelea eneo hilo ili waweze kutoa elimu ya kutosha kwa wachimbaji wa madini kuhusu namna ya kupata mikopo na utunzaji wa fedha unaotokana na uchimbaji wa madini.

Kuhusu migogogro ya wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Matongo, Dkt. Kiruswa ametoa wiki mbili kwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Ofisi ya Madini ya Mkoa kuhakikisha wanamaliza migogogro yote ikiyowasikishwa na wananchi wakati wa ziara hiyo.

Akizungumzia ukosefu wa umeme, maji katika migodi hiyo na barabara, Dkt.Kiruswa amesema, Serikali itaboresha mazingira hayo ili wachimbaji hao waweze kuchimba na kupata manufaaa.

Amesema, Serikali ni sikivu itakwenda kutatua changamoto hizo kwa wakati ili waendelee na uchimbaji.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu,akizungumza na wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Matongo kilichopo Wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu ameomba ofisi za GST wasogeze huduma za kitafiti katika maeneo hayo ya wachimbaji ili waweze kuchimba kwa tija.

Amesema, wachimbaji hao kwa sasa wanachimba kwa kubahatisha jambo linalofanya wapoteze fedha nyingi.

Mtaturu ameomba Serikali kupitia Wizara ya Madini iweze kuwasaidia wachimbaji hao kupata mitaji ili iwasaidie kuweza kuchimba kwa kutumia vifaa vya kisasa vya uchimbaji kuendana na teknolojia.
 
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Chone Malembo ametumia fursa hiyo kuwataka wachimbaji kushirikiana na Ofisi ya Madini Singida ili waweze kutatua migogogro yote inayowasumbua wachimbaji.

Ameeleza kuwa, elimu kuhusu uchimbaji wenye tija itaendelea kutolewa kama ilivyoelekezwa na Naibu Waziri ili wachimbaji waweze kufanya shughuli zao kwa urahisi.

Aidha, amewataka kuzingatia sheria na kanuni zote za uchimbaji ili kuepusha migogogro inayojitokeza mara kwa mara.

Naibu Waziri wa Madini amefanya ziara ya siku mbili mkoani Singida ili kuzungumza na kusikiliza kero mbalimbali zinazowasumbua wachimbaji wadogo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news