Waziri Mkuu:Undeni timu za kusimamia zao la kahawa

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Kagera uunde timu za kusimamia zao la kahawa kuanzia uoteshaji wa miche, kilimo chenyewe hadi mauzo ya zao hilo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao cha Wadau wa zao la Kahawa alichokiongoza kwenye ukumbi wa ELCT mjini Bukoba, Mei 15, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Akizungumza katika kikao cha wadau wa zao la kahawa alichokiongoza kwenye ukumbi wa ELCT mjini Bukoba leo Mei 15, 2022, Mheshimiwa Majaliwa amewataka viongozi wa Mkoa huo na wilaya zake waandae vitalu vya miche ya kahawa na kuigawa kwa wananchi ikiwa na moja ya mbinu za kuwahamasha kulima zao hilo.

Amewataka viongozi na watendaji wa mkoa na wilaya kuishawishi sekta binafsi iwekeze kwenye vitalu vya miche ya kahawa ili kupata miche ya kutosha ya kuwauzia wananchi hatua ambayo itaisaidia kujipatia fedha na kutengeneza ajira.

Pia amewataka viongozi na watendaji wa Mkoa na wilaya wahakikishe kuwa Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani unafanikiwa kwa kuwaelimisha wananchi faida kubwa watakazozipata kutokana na mfumo huo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde katika Kikao cha Wadau wa zao la Kahawa alichokiongoza kwenye ukumbi wa ELCT mjini Bukoba, Mei 15, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Amesema ili kufanikisha mfumo huo, lazima viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kagera (KCU) na kile cha Karagwe (KDCU) wabainishe maeneo itakapofanyika minada ya kahawa na wahakiki na kutangaza hadharani uwepo na wingi wa kahawa inayopigwa mnada.

“Hakuna mnunuzi atakayeruhurusiwa kwenda majumbani au kwenye Chama cha Msingi kupatana bei au kununua kahawa. Kahawa yote inunuliwe kwenye maeneo ya mnada.”

Alisisitiza kwamba wafanyabiashara lazima waratibiwe na wasipewe kabisa fursa ya kujadili bei na viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi au wananchi mashambani au majumbani kwani mipango yote ya bei na ununuzi wa kahawa inapaswa kufanyika mnadani.

Mheshimiwa Majaliwa ameagiza kuwa minada iwe wazi na maeneo ya inakofanyika yajulikane pia wakulima washirikishwe ili wajue bei ya mazao yao.
Baadhi ya washiriki wa Kikao cha Wadau wa zao la Kahawa wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipoongoza kikao hicho kwenye ukumbi wa ELCT mjini Bukoba, Mei 15, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Mheshimiwa Majaliwa pia ameagiza kuwa wanachi washawishiwe kufungua akaunti benki ili malipo ya pesa zitakazotokana na mauzo ya kahawa yao yaingizwe kwenye akaunti hizo hatua ambayo itasaidia kuondoa hatari ya wakulima kuibiwa malipo yao.

Waziri Mkuu aliwasihi viongozi wa Serikali na wa ushirika wajiepushe na biashara ya ununuzi wa kahawa kwani endapo yatatokea mapungufu watawajibika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news