Rais Dkt.Mwinyi apongeza mikakati ya WFP, kusaidia maendeleo Zanzibar

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza mikakati na mipango iliyowekwa na Shirika la Chakula Duniani (WFP), kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) nchini Tanzania, Bi.Sarah Gordon-Gibson.(kulia kwa Rais) akiwa na Ujumbe wake walipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu. (Picha na Ikulu).

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Mei 5,2022 wakati alipofanya mazungumzo na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) nchini Tanzania, Sarah Gordon-Gibson.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi alimueleza Mwakilishi Mkaazi huyo kwamba hatua za Shirika la Chakula Duniani (WFP) kuongeza mikakati na mipango ya kuhakikisha Zanzibar inafaidika moja kwa moja na huduma inazozitoa katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Rais Dkt.Mwinyi alifurahishwa na dhamira ya shirika hilo ya kushirikiana na Serikali katika suala zima la kukabiliana na maafa, uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake hasa wale wakulima wa mwani, lishe na usalama wa chakula, kuwasaidia wakulima wadogo wadogo hasa katika ujenzi wa barabara za ndani na kuwasaidia katika mnyororo mzima wa usafirishaji wa bidhaa.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi alizipongeza juhudi zilizoanza kuchukuliwa na Shirika hilo za kuanza mazungumzo na baadhi ya sekta husika katika kuendeleza program hizo.

Hivyo, Rais Dkt. Mwinyi alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano wake bega kwa bega kwa shirika hilo la WFP, katika kuhakikisha linatekeleza vyema shughuli zake hapa Zanzibar.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alipongeza maeneo ambayo Shirika hilo limekusudia kuongeza nguvu zake ikiwa ni pamoja na kuwasaidia akina mama wanaolima zao la mwani kwa kuwaongezea uwezo kwa kulipata thamani zao hilo pamoja na kuwatafutia soko la uhakika.

Kwa upande wa suala zima la chakula, Rais Dkt. Mwinyi aliipongeza azma ya shirika hilo ya kurejesha huduma ya chakula kwa watoto shuleni hatua ambayo itawaongezea ufahamu sambamba na kuwasaidia watoto kuwa na lishe bora.

Pamoja na hayo, Rais Dkt. Mwinyi alieleza kuwa Shirika hilo limekuwa likifanya kazi vyema hapa nchini na azma yake ya kuongeza mikakati yake katika program ilizojiwekea ziitasaidia Jamii kwa kiasi kikubwa wakiwemo wanawake na watoto.

Nae Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP), nchini Tanzania, Sarah Gordon-Gibson alimueleza Rais Dkt. Mwinyi mikakati na mipango iliyowekwa na Shirika la (WFP) kwa Zanzibar katika kipindi cha miaka mitano kuanzia Julai 2022 hadi Julai 2027 itaongezwa.

Mwakilishi huyo Mkaazi alieleza kwamba Shirika la (WFP), tayari limeshapanga program kadhaa ambazo Zanzibar kwa upande wake nayo itafaidika kwa kiasi kikubwa katika kipindi hicho cha miaka mitano zikiwemo kuwawezesha wanawake hasa wakulima wa mwani, kukabiliana na maafa, lishe na usalama wa chakula, kuwasaidia wakulima wadogo wadogo hasa katika ujenzi wa barabara za ndani na kuwasaidia katika mnyororo mzima wa usafirishaji wa bidhaa pamoja na program nyenginezo.

Aidha, Bi Sarah Gordon- Gibson alieleza jinsi Shirika hilo linavyofanya kazi zake za kutoa huduma zikiwemo za chakula kwa wakimbizi kwa kule Tanzania Bara katika pamoja na nchi nyengine za jirani.

Pamoja na hayo, Mwakilishi huyo Mkaazi wa (WFP) alipongeza mashirikiano mazuri anayoyapata kupitia Shirika hilo hapa Zanzibar na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano wake ili Zanzibar izidi kupata mafanikio zaidi katika sekta zake za maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news