Serikali yaeleza mafanikio ya ziara za Rais Samia nchini Marekani, Uganda na Royal Tour

NA DIRAMAKINI

MKURUGENZI wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, amefafanua mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, nchini Marekani iliyojumuisha uzinduzi wa Filamu ya “Tanzania; The Royal Tour." Pamoja na ziara ya Rais nchini Uganda.
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Bibi Zuhura Yunus akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini Marekani na Uganda katika Mkutano uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu jijini Dar es salaam, Bi. Yunus amesema ziara ya Rais nchini Marekani imekuwa na faida ya kusainiwa kwa mikataba saba kati ya kampuni za Marekani na Tanzania zenye lengo la kufanya biashara na uwekezaji nchini yenye gharama za zaidi ya shilingi Trilioni 11.

Nini kilifanyika Marekani

Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni akiwa katika ziara ya kiserikali nchini Marekani ameshuhudia utiaji saini wa mikataba saba kati ya makampuni ya Marekani na Tanzania yenye lengo la kufanya biashara na uwekezaji mkubwa nchini.

Mikataba hiyo na makampuni makubwa ya Marekani iliyotiwa saini jijini Washington D.C. ina thamani ya Shilingi Trilioni 11.7 inayotarajiwa kutengeneza jumla ya ajira 301,110 kwenye kilimo, utalii, biashara na sekta nyingine za uchumi.

Rais Samia alishuhudia utiaji saini wa hati za makubaliano (MoU), barua za kuonesha nia (letters of intent) na kuanza kwa mazungumzo ya uwekezaji na biashara kati ya makampuni ya nchi hizo mbili.

Miradi mingine iliyotiwa saini inalenga kuwekeza kwenye mnyororo wa thamani katika kanda ya kaskazini ya sekta ya utalii wa Tanzania, ikiwemo kwenye maeneo ya kutangaza utalii na kuongeza idadi na ubora wa huduma zinazotolewa.

Rais Samia pia alishuhudia makampuni ya Marekani yakitangaza nia na mipango ya kuongeza mahusiano yao na Tanzania kwenye maeneo ya uwekezaji na biashara. Makampuni hayo ni pamoja na Upepo Energy, Astra Energy, Crane Currency na Parallel Wireless.

Pamoja na mikutano mingine, Rais Samia alihudhuria mkutano kwenye makao makuu ya Chemba ya Biashara ya Marekani (U.S. Chamber of Commerce) uliohudhuriwa na wafanyabiashara na viongozi wa serikali wa nchi zote mbili wakijadiliana namna ya kuongeza uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwaelezea Waandishi wa Habari (hawapo pichani) mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini Marekani na Uganda katika Mkutano uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameelezea ziara ya Rais nchini Uganda ambayo iliwezesha kufanyika kwa mkutano maalum na wadau wa sekta za mafuta na gesi kuhusiana na ujenzi wa bomba la mafuta.

"Tulikuwa na mkutano maalum juu ya ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanzania, tayari hatua ya ulipaji fidia kwa wananchi imekamilika na ujenzi wa bomba hilo utaanza hivi karibuni,"amesema Balozi Mulamula.

Yaliyojiri ziarani Uganda

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa nchini Uganda alishuhudia utiaji saini wa Hati ya Ushirikano (MoU) mbili Ikulu jijini Entebbe nchini Uganda.

Hati hizo ni pamoja na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa 400KV kutoka Masaka-Mutukula-Nyakanazi -Mwanza na nyingine ni kuhusu ushirikiano wa masuala ya Ulinzi na Usalama baina ya nchi hizo mbili.

Aidha, utiaji saini huo ulishuhudiwa pia na Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni ambapo alisisitiza kuendelea kushirikiana kwenye utenngenezaji wa chanjo na dawa za binadamu na mifugo.

Makubaliano pia ni kwamba Tanzania itaanza kununua dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI (ARVs) kutoka Uganda.

Miongoni mwa mengine yaliojadiliwa ni kufunguliwa upya kwa njia ya Mwanza - Port Bell Kampala, ambayo hapo awali ilikuwa haifanyi kazi lakini hivi sasa inafanya kazi.

Kwa sasa njia hiyo imepunguza kwa kiwango kikubwa muda wake wa mpito ambapo sasa huchukua siku 4 tu tofauti na siku 9 hapo awali, hivyo kupunguza gharama za kufanya biashara.

Wakati huo huo, Tanzania imekubali kupunguza gharama za usafirishaji ambapo kwa sasa Uganda italipa Dola za Kimarekani 10 kwa lori litakalopita kila kilomita 100 katika njia ya kutoka Mutukula hadi Dar es Salaam kuanzia mwaka mpya wa fedha Julai mosi mwaka huu.

Pia, Uganda imeahidi kutuma tani nyingine elfu 10 za sukari ili kufidia upungufu wa bidhaa hiyo Tanzania.
Katibu Mkuu Wizara ya Sanaa, Utamaduni, na Michezo, Dkt. Hassan Abbas akiwaelezea Waandishi wa Habari (hawapo pichani) mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini Marekani na Uganda katika Mkutano uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Rais ya kuitangaza Tanzania, Dkt. Hassan Abbasi, amesema Filamu ya Royal Tour imeonesha mafanikio makubwa sana na kwa sasa filamu hiyo imeendelea kusambazwa katika vituo vya televisheni karibu 300 kati ya 350 nchini Marekani na kwa hapa nchini tayari filamu hiyo imesambazwa katika vituo vyote vya televisheni.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara amesema filamu ya Royal Tour ina manufaa ya moja kwa moja kwa Taifana inatarajiwa kuleta wawekezaji, watalii na wafanyabiashara na kuongeza kuwa wao kama Wizara wameandaa mkutano na wadau ili kupanga mikakati ya kuwekeza katika sekta ya utalii.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii (TTB), Bw. Amos Nko amesema TTB inatangaza kwa kasi vivutio vya utalii ili kuvutia watalii wengi kuja nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news