Shabiki wa Simba SC auawa kisa mpira wa tobo aliopigwa Peter Banda

NA DIRAMAKINI

SHABIKI wa Simba SC anayejulikana kwa jina la Agustino Mwangosi kutoka Kijiji cha Kingiri Kata ya Ipinda wilayani Kyela ameuawa na shabiki anayedaiwa ni wa Klabu ya Yanga (jina linahifadhiwa) kisa kikiwa ni majibizano ya mchezaji wa Simba, Peter Banda kupigwa mpira uliopita katikati ya miguu (TOBO).
Akizungumza na Kyela Fm katika kipindi cha KONA YA MICHEZO, Diwani wa Kata ya Ipinda, Eliah Mwaipetani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Ameelezea kuwa, marehemu alikuwa katika hali ya majibizano ya kishabiki na mtuhumiwa walipokuwa wakitazama mchezo wa Simba dhidi ya Pamba katika hatua ya robo Fainali ya Kombe la ASFC.

Katika majibizano hayo ilionesha mtuhumiwa kutopendezwa na majibu ya marehemu, ndipo mtuhumiwa akaondoka eneo la tukio (KIBANDA UMIZA) na kuamua kumvizia marehemu wakati akirudi na kumuua kwa kumpiga na gogo sehemu mbalimbali za mwili na kupelekea umauti wake.

Diwani Mwaipetania amesema, mwili wa marehemu umezikwa Jumapili ya Mei 15,2022 na hatua za kisheria zimechukuliwa dhidi ya mtuhumiwa.

Aidha, Diwani huyo amewataka mashabiki wa mpira kuacha ushabiki wa ovyo na mpaka kupelekea kuuana.

Katika mtanange huo, watetezi Simba SC walifanikiwa kwenda Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Pamba FC ya Mwanza .

Ni mtanange ambao ulipigwa katika dimba la Benjamin Mkapa katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Mabao ya Simba SC yamefungwa na viungo Mmalawi, Peter Banda dakika ya 45 na wazawa, Kibu Dennis mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) dakika ya 48 na Yussuf Mhilu mawili, dakika ya 53 na 89.

Simba SC itamenyana na watani wa jadi, Yanga katika Nusu Fainali, wakati Azam FC itamenyana na Coastal Union.

Post a Comment

0 Comments