TIRA yazipiga faini kampuni nne za bima nchini, yaonya na kuwatoa hofu wananchi

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA) imezipiga faini kampuni nne za bima kwa kukiuka sheria za bima Namba 10 ya mwaka 2009 pamoja na marekebisho yake.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 10,2022 jijini Dar es Salaam, Kamshina wa TIRA, Dkt. Baghayo A.Saqware amesema, soko la bima la Tanzania licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo lakini linakuwa kwa asilimia 10, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi kwani mamlaka hiyo inafanya kazi zake kwa umakini.

"Leo Mei 10, 2022 Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA) inasikitika kutoa taarifa kuhusu mwenendo usiofaa wa kampuni nne za bima nchini katika utoaji wa huduma za bima nchini.

"Kutokana na matakwa ya Sheria ya Bima Namba 10 ya Mwaka 2009 na marekebisho yake ya mwaka 2017,Mamlaka imebainisha pasipo na shaka kuwa Kampuni za bima za Insurance Group of Tanzania (IGT), Jubilee General Insurance, Resolution Insurance na UAP Insurance zimekiuka kifungu 131(1)(2)(4) cha sheria ya Bima Na. 10 ya mwaka 2009 pamoja na marekebisho yake,"amefafanua Dkt.Saqware.

Amesema, Kampuni ya Insurance Group of Tanzania (IGT) kwa nyakati tofauti kuanzia Oktoba Mosi, 2021 hadi Februari 15,2022 wamepokea malalamiko zaidi ya 48 dhidi ya kampuni hiyo.

"Katika malalamiko hayo, mamlaka imeyachanganua kama ifuatavyo, lalamiko moja lilihusiana na kiwango kidogo cha
fidia kilichotolewa kwa munufaika wa bima.Malalamiko nane ni kuhusu ucheleweshaji wa mchakato wa madai.

"Malalamiko matatu yanahusisha kukataa madai bila kuwa na msingi wa kuyakataa. Malalamiko thelathini na tatu ni kutolipa madai baada ya kutoa Hati ya Kukubali Madai yaani Discharde Voucher kinyume na matakwa ya Sheria ya
Bima namba 10.

"Lalamiko moja linahusu kutotekeleza maamuzi ya Ofisi ya Msuluhishi wa Bima (TIO), na malalamiko mawili ni kuhusu kuchelewa kutoa idhini na malipo ya matengezo ya magari ya wateja wa bima wanaodai fidia,"amefafanua Dkt.Saqware.

Amesema,baada ya kuchunguza malalmiko hayo, mamlaka imebaini kuwa, Kampuni ya IGT imeenda kinyume na matakwa ya kifungu namba 131(1) cha Sheria ya Bima nchini.

Pia amesema kuwa, pamoja na kukiukwa huko kwa sheria, wastani wa wateja wanane kila mwaka kuanzia mwaka 2018-2021 wamekuwa wakipeleka malalamiko yao kuhusu huduma hafifu za kampuni hiyo katika ofisi za Mamlaka na Msuluhishi wa Migogoro ya bima (TIO) nchini.

"Hii, inaonyesha mwenendo usiofaa kwa kampuni hii. Pia, mamlaka imebaini kuwa kampuni hii, imeanzisha upya uchunguzi wa baadhi ya malalamiko ambayo awali wayakubali na kutoa Hati ya Kukubali kulipa fidia, jambo ambalo linaleta dukuduku na wasiwasi wa mwenendo wa wataalam na nia ya utoaji haki kwa wateja.

"Kwa kuzingatia takwimu hizo, Kamishna wa Bima kwa Mamlaka ya kisheria kupitia kifungu namba 166(1 & 2) cha Sheria ya Bima nchini anachukua hatua zifuatazo dhidi ya Mwenyekiti wa Bodi, Afisa Mtendaji Mkuu, Afisa Fedha Mkuu na Meneja madai wa kampuni hii, kama ifuatavyo;

a. Mwenyekiti wa Bodi ya IGT

"Mamlaka inatoa faini ya kiasi cha shilingi milioni tano kwa Mwenyekiti wa Bodi ya IGT kwa kutoishauri na kutosimamia vyema menejimenti ya kampuni hivyo kusababisha wateja na wananchi kukosa haki zao.

b. Afisa Mtendaji Mkuu

"Mamlaka inatoa faini ya kiasi cha shilingi milioni tano kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa IGT kwa kutosimamia vyema utendaji wa kila siku kampuni hivyo kusababisha wateja na wananchi kukosa haki zao.

c. Afisa Fedha Mkuu

"Mamlaka inatoa faini ya kiasi cha shilingi milioni tano kwa Afisa Mkuu wa Fedha IGT kwa kutoheshimu Sheria ya Bima na kusababisha wateja na wananchi kukosa haki zao.

d. Meneja wa Madai na Fidia

"Mamlaka inatoa faini ya kiasi cha shilingi milioni tano kwa Meneja Madai na Fidia kwa kutoheshimu na kuzingatia sheria ya bima na kusababisha wateja na wananchi kukosa haki zao,"amefafanua Dkt.Saqware.

Dkt.Saqware amesema,kwa kuzingatia kifungu Namba 166(1) cha Sheria ya Bima nchini, mamlaka inaagiza kampuni ya IGT kulipa wadai wote 48 ambao imeshawapatia hati ya kukubali madai (Discharge Voucher) ndani ya siku 14 kuanzia leo.

Pia amesema, inapaswa kutoa taarifa ya utelekezaji na ulipaji wa madai yote halali ya bima kila wiki, katika kipindi cha miezi mitatu ijayo kuanzia leo.

Amesema, mamlaka itafanya ukaguzi maalumu kwa kampuni hiyo katika maeneo ya Operesheni za Biashara,Mitaji na Sifa na Weledi wa watumishi wa kampuni.

"Kampuni ya IGT inapaswa kuleta taarifa rasmi ya kikao cha bodi kilichojadili na kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Kamishna.

"Kwa mujibu wa Kifungu Na. 29 (a) na (f)ii cha Sheria ya Bima Na. 10 ya Mwaka 2009. Mamlaka inadhamiria kuiwekea zuio kampuni ya IGT kufanya biashara ya bima za magari mpaka pale kampuni hiyo itakapokuwa na mwenendo mzuri wa ulipaji wa madai yatokanayo na ajali za magari,"amefafanua Dkt.Saqware.

Kampuni ya Jubilee

Akizungumzia kuhusu kampuni hiyo, Dkt.Saqware amesema kuwa, kwa nyakati tofauti kuanzia Oktoba Mosi, 2021 hadi Mei 6, 2022 Ofisi ya Kamishna wa Bima imekuwa akipokea malalamiko zaidi ya manne dhidi ya kampuni hiyo.

Pia, mamlaka imekuwa ikipokea malalamiko dhidi ya Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo kuhusu mwenendo usiyofaa wa utendaji katika sekta ya bima hususan katika masuala yanayohusiana na madai.

"Oktoba 19,2020 mamlaka ilipokea malalamiko ya Wizara ya Maji dhidi ya Kampuni ya Bima ya Jubilee kuhusu kutokubali kulipa malipo ya fidia kutokana na Kampuni ya Ukandarasi ya Spencon kushindwa kutimiza wajibu wake wa kimkataba wa ujenzi wa miradi ya maji wenye mkataba No. ME-011/2011-2012/W/05 wa Mamlaka ya Maji ya Mji wa Kigoma ambao ulikuwa umepewa kinga na Kampuni ya Bima ya Jubilee.

"Baada ya Mamlaka kupokea malalamiko hayo, Oktoba 17,2021, Wizara ya Maji, Mamlaka ya Bima,
Kampuni ya Ukandarasi ya Spencon na Kampuni ya Bima ya Jubilee zilikaa kikao ili kutatua malalamiko hayo.

"Kikao hicho hakikutoa suluhu kutokana na mwakilishi wa kampuni ya Jubilee kutokuwa na nguvu ya maamuzi ya kiutendaji. Novemba 18, 2021 Kamishna wa Bima aliitisha kikao na wahusika wote kuhudhuria. Baada ya kutathmini kwa kina juu ya malalamiko haya, Mamlaka iliona madai ya Wizara ya Maji dhidi ya kampuni ya Jubilee ni sahihi.

"Hivyo, kikao hicho kiliimuru Kampuni ya Bima ya Jubilee kulipa fidia ya kiasi cha 511,065.49 Euro kama inavyodaiwa na Wizara ya Maji ndani ya siku 30 baada ya uamuzi huo na pia kampuni hiyo ilipigwa faini ya shilingi milioni tano ambayo tayari imeshalipwa,"amesema.

Kamshina wa TIRA, Dkt. Baghayo A.Saqware amesema, ili kufuatilia utekelezaji wa maelekezo hayo, Desemba 15,2021 Mamlaka iliiandikia barua Jubilee kutaka kupata majibu ya utekelezaji.

Amesema, Kampuni ya Bima ya Jubilee ilijibu barua kuwa italipa fidia hiyo ndani ya siku 45 toka siku ya barua majibu yao.

"Pamoja na kukubali kulipa,mamlaka imepata nakala ya barua iliyoandikwa na kampuni hii kwenda kwa Wizara ya Maji ikitaka kuanzisha uchunguzi upya na kutolipa kiasi kinachopaswa kulipwa kama
ilivyokubaliwa na pande zote.

"Kwa kuzingatia Sheria na taratibu za uendeshaji wa Biashara za Bima nchini, mamlaka inachukua hatua nne kama zifuatazo;

"Inaigiza Kampuni ya Jubilee kulipa kiasi chote cha 511,065.49 Euro kwa Wizara ya Maji kama ilivyoagizwa katika kikao cha Novemba 18, 2021 ndani ya siku 14 kuanzia leo.

"Pia mamlaka inaitaka kuacha mara moja nia ya kuanzisha uchunguzi upya wa shauri lilikwisha fungwa na wao kukubali kulipa madai na mamlka inatoa adhabu ya kiasi cha shilingi milioni 10 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hii kwa kutofuata taratibu za kibima, hivyo kuchafua taswira ya soko la bima kwa makosa mawili tofauti ambapo kila kosa litakuwa shilingi milioni tano.

Malalamiko mengine amesema kuwa ni kutoka GT Bank dhidi ya Jubilee na Innocent Masinde dhidi ya Jubilee.

"Mwananchi huyu amelalamikia utendaji mbovu wa wa Mtendaji Mkuu wa kampuni hii Ndg. Dipanka Achary na Mwanasheria Ndg, David Shoo. Kwani madai na kutolipa madai ya mteja huyu na watajwa hapo juu kutenda kinyume msingi wa uchakaji wa madai ya mteja kama inavyotakiwa na taratibu na Sheria ya Bima Na. 10 ya Mwaka 2009,"amesema.

Kampuni ya Bima ya Resolution

Kamshina wa TIRA, Dkt. Baghayo A.Saqware amesema,Kampuni ya Bima ya Resolution ilisajiliwa na kupewa leseni ya kufanya biashara ya bima nchini kuanzia Julai mwaka 2012.

Amesema, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima katika nyakati tofauti imekuwa ikikagua na kushauri namna nzuri ya uendeshaji wa kampuni hiyo baada ya kuona uwezo wake wa kifedha unazorota kutokana na usimamizi mbovu, mienendo isiyo ya kitaalamu na ukiukwaji mkubwa wa sheria na ufanyaji wa biashara ya bima unaofanywa na Wakurugenzi na Afisa Mkuu wa kampuni hiyo.
"Baada ya mamlaka kubaini hayo, ilichukua hatua mbalimbali kuhakikisha inaikwamua kampuni hii katika mdororo wa kiutendaji na kimtaji. Mnamo mwezi Februari 2018, mamlaka ilielekeza Wakurugenzi, Menejimenti na Afisa Mkuu wa kampuni kuleta mpango mkakati wa miaka mitatu wa kuhuwisha mtaji ili kampuni hii iendelee na bishara kwa mujibu wa sheria ya bima.

"Pamoja na jitihada zote hizo, bado matokeo chanya hayajapatikana. Jukumu la Mamlaka miongoni mwa mengine, ni kulinda maslahi ya wateja wa bima na wanufaika wengine. Kwa kuzingatia hilo, imefanya maamuzi na kuchukua hatua mbalimbali na inapenda kuutaarifu umma yafuatao;

"Kati ya kipindi tajwa mamlaka ya bima ilipokea malalamiko kutoka kwa mteja huyu ya kutokulipwa fidia ya bima na kampuni ya bima ya UAP. Baada ya Uchunguzi Mamlaka iligundua makosa ya kiutendaji na uzembe uliyofanywa na kwampuni.

"Katika utetezi wa kampuni ilionekana kutolewa kiasi kidogo cha tozo ya bima ingawa mteja alitoa kiasi sahihi cha tozo la bima.Kosa ambalo limesababisha mteja kukosa haki yake ya msingi kibima.

Maamuzi ya Kamishna

"Mamlaka inaigiza kampuni hii kulipa fidia mara ndani ya siku saba kuanzia tarehe ya taarifa. Ieleweke kuwa hatua hizi zinatokana na mlolongo wa malalamiko ya wahanga wa majanga yaliyopokelewa na mamlaka.

"Kutokana na Mamlaka kuwa na jukumu la kulinda watumiaji wa bima yaani wananchi na kuendeleza soko, inatoa onyo kwa kampuni za bima nchini zitakazochelewesha ama kuchezea haki ya fidia ya mwananchi.

Pia, tunawaasa watanzania kuendelea kutumia huduma za bima nchini na kutosita kuleta Malalamiko yao kwa Kamishna wa Bima pindi wanapoona kampuni za bima haziwatendei haki.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima inapenda kuujulisha umma wa Watanzania kuwa kampuni zote za bima nchini zitatakiwa kuleta taarifa za madai yote yaliyowasilishwa kwa na hatua za kiutendaji au usuluhishi walizofikia kila robo mwaka.

Hatua hii ni ishara ya dhamira ya dhati ya mamlaka katika kusimamia shughuli za bima na kuzingatia haki za wateja nawajibu wa watoa huduma ili kuboresha shughuli za utoaji wa huduma za bima katika nchi yetu,"amefafanua Kamshina wa TIRA, Dkt. Baghayo A.Saqware.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news