Waziri Dkt.Kijaji:Watanzania changamkieni fursa za kibiashara zinazoletwa na Filamu ya Royal Tour

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ametoa rai kwa Watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali ikiwemo kuzalisha bidhaa na kutoa huduma zenye ubora na viwango vya kimataifa na kujenga Hoteli kwa ajili ya Malazi ya Watalii wanaongezeka kwa kasi kubwa kutokana na uzinduzi wa Filamu ya The Royal Tour inayolenga kutangaza vivutio vya utalii na uwekezaji vilivyopo Tanzania.
Waziri Kijaji ameyasema hayo katika hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya Tisa (9) ya Biashara na Utalii ya Mkoa wa Tanga kwa mwaka wa 2022 iliyofanyika Mei 30, 2022 katika viwanja vya Mwahako jijini Tanga. Maonyesho hayo yaliyoandaliwa na TCCIA kwa kushirikiana na Uongozi wa Mkoa wa Tanga yamelenga kuongeza tija na ustawi wa uchumi wa Mkoa huo na taifa kwa ujumla.
“Serikali pia inatekeleza Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuboresha utoaji wa huduma za umma kwakupunguza utitiri wa kodi, ushuru na tozo mbalimbali zilizokuwa kero na ujenzi wa miundombinu kama Barabara, Reli, umeme, Maji, Gesi, bandari, viwanja vya ndege, meli na vivuko ili kuvutia uwekezaji, kuongeza ajira, kukuza uchumi na kuchangia Pato la Taifa.” Amesema Waziri Kijaji.

Aidha, Waziri kijaji ameziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuiga mfano wa maonyesho hayo na kuboresha utoaji wa huduma za umma kwa sekta binafsi ikiwemo upatikanaji wa ardhi, usajili na malipo ya ada na tozo za uanzishaji na uendeshaji wa biashara kwa njia ya mtandao ili kurahisisha utoaji wa huduma hizo kwa kupunguza muda na gharama za kufanya biashara na kuwekeza nchini.
Waziri Kijaji pia ametoa rai kwa Watanzania kutumia kikamilifu fursa za kibiashara na uwekezaji zinazopatika katika mikataba ya kibiashara kama vile Mkataba wa Dallas ambao ni lango la bidhaa kutoka Tanzania pamoja na Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) wenye wanachama 55 wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), soko la watu takribani bilioni 1.2, Pato la Taifa la Dola za Kimarekani Trilioni 3.4. kwa kuzalisha bidhaa kwa wingi zenye ubora na viwango vya kimataifa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa tanga Mhe. Adam Kighoma Malima akimkaribisha Mhe. Waziri kufungua maonyesho hayo yaliyoanza Mei 28 hadi Juni 6, 2022 na kuhudhuliwa na taasisi 84 ameziagiza benki kupunguza riba na Viwanda vinavyotengeneza vipodozi mkoani humo kuwawezesha wajasiliamali wadogo wanaotengeneza sabuni za mwani na bidhaa nyingine ili kuboresha vipodozi hivyo katika kiwango cha kimataifa

Post a Comment

0 Comments