Waziri Bashungwa asikia kilio cha wananchi watakaoguswa na ujenzi wa Karakana ya Mabasi ya Mwendokasi Ubungo

NA OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amemuelekeza Mthamini Mkuu wa Serikali kuzingatia sheria na haki wakati wa zoezi la uthamini kwa ajili ya ulipaji wa fidia kwa wananchi 90 wa eneo la Ubungo Maziwa jijini Dar es Salaam watakaoathirika na mradi wa ujenzi wa karakana ya mabasi yaendayo haraka.
Bashungwa ametoa maelekezo hayo leo Mei 14, 2022 Ubungo jijini Dar es Salaam wakati akisikilza kero za wananchi wanaolalamikia baadhi ya mapungufu katika zoezi la uthamini lililofanywa na Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka yanayolazimu zoezi hilo kurudiwa upya.

Amesema, atakutana na Mthamini Mkuu wa Serikali na kumuelekeza aongeze muda wa zoezi la uthamini ambalo litaanza Jumatatu ya Mei 16, 2022 na kufanyika ndani ya siku 21 hadi kukamilika ili zoezi hilo lifanyike kikamilifu ili baada yapo kusiwepo na malalamiko yoyote ya wananchi.

Aidha, Bashungwa amewahakikishia wanannchi kuwa Mheshiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Samia Suluhu Hassan anataka wananchi wake wapelekewe maendeleo kwa kufuata sheria na haki bila kudhulumu wala kumuonea mwananchi yoyote.
Waziri Bashungwa amepongeza wananchi hao kwa kutoa ushirikiano kwa Serikali wakati ikitekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo yao ambapo ameeleza tatizo sio wananchi kugomea mradi huo bali mchakato uliotumia ili kulipa fidia haukuzingatia sheria na haki.

Maeneo yanayotarajiwa kutwaliwa yapo katika eneo la Ubungo Maziwa ambayo yana ukubwa wa mita za mraba 68,900, ambapo yatawezesha ujenzi wa karakana mbadala na ile ya Jangwani ambayo inatakiwa kuhamishwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mafuriko.

Post a Comment

0 Comments