Bunge lapitisha Bajeti ya Bilioni 35.42/- Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

NA ELEUTERI MANGI-WUSM

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambayo ni jumla ya Sh. 35, 425,991,000 kutekeleza majukumu ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 huku ikitarajiwa kukusanya kiasi cha Sh. 900, 000,000 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo zinakadiriwa kukusanya Sh.5, 396,455,000.
Akiwasilisha Bungeni hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake Juni 6, 2022 jijini Dodoma, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa amelithibitishia Bunge kuwa pamoja na mambo mengine Wizara hiyo imejizatiti kutekeleza miradi mbalimbali ili kuwahudumia Watanzania.

Waziri Mchengerwa amebainisha kuwa kati ya fedha hizo zilizotengwa kutekeleza majukumu ya wizara, Shilingi Bilioni Sh.8, 201,882,000 zitatumika kwa mishahara ya watumishi, Shilingi Bilioni 11,392,949,000 zitatumika kwa matumizi mengineyo na Sh. Bilioni 15,831,160,000 zitatumika kutekeleza miradi ya Maendeleo ambayo ipo chini ya wizara na taasisi zake.

Miradi mikubwa inayoenda kutekelezwa na Wizara hiyo kwa mwaka 2022/23 ni ujenzi wa vituo vya mazoezi, kupumzika wananchi, Sports and Arts Arena ambayo itagharimi kiasi cha Sh.7,166,160,000, ujenzi wa eneo Changamani la michezo Dar es Salaam Sh.1,500,000,000, ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya michezo katika Shule Maalumu 56 za michezo Sh.2,000,000,000 na ujenzi wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya ambao utagharimu Sh.1,300,000,000 ujenzi wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kwa lengo la kukuza na kuendeleza vipaji na kuendelea na ujenzi wa hostel ya wanafunzi.

Waziri Mchengerwa ametaja miradi mingine itakayotekelezwa kuwa ni ujenzi wa eneo Changamani la Michezo Dodoma ambao utagharimu Sh.100,000,000, Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ambao umetengewa Sh.2,400,000,000, ukarabati wa Chuo cha Sanaa na Utamaduni Bagamoyo Sh.550,000,000, kuimarisha Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Sh.300,000,000 pamoja na uimarishaji wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika ambayo imetengewa kiasi cha Sh.515,000,000.

“Nafahamu Bunge lako Tukufu linajua kwamba kauli ya “Anaupiga Mwingi” inatokana na lugha ya kimichezo. Nathibitisha kauli hiyo kwa mambo haya kumi ndani ya mwaka mmoja wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ambapo karejesha Tuzo za Filamu, Tuzo za Muziki na karejesha mirabaha” amesema Waziri Mchengerwa.

Kupitia wizara hiyo, Serikali ya Awamu ya Sita inajivunia mambo lukuki yakiwemo Rais Samia Suluhu Hassan akiwa mstari wa mbele akitoka ofisini na kuigiza filamu ya “Royal Tour” ambayo inaendelea kuwavutia watalii na watu wengi kuja nchini kujionea vivutio na mandhari nzuri ya Tanzania, hivyo ni shahir na dhahir kuwa anaendelea kuiongoza nchi kwa umahiri, weledi, umakini na upeo mkubwa unaoendelea kulishamirisha Taifa ndani na nje ya nchi.

“Sisi na wadau wetu wote wa sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo tunamuahidi kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na kwa weledi ili kuendana na fikra, maono, na falsafa yake ya kazi iendelee na tunaendelea kumuombea dua njema kila uchao kwani Waswahili husema, “Dua njema ya msafiri ndilo tairi salama,” amesisistiza Waziri Mchengerwa.

Post a Comment

0 Comments