Jaji Masaju:Tutende haki kwa wote bila kujali hali zao kiuchumi

NA INNOCENT KANSHA-Mahakama

JAJI wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. George Masaju amewaasa Wahasibu na Wakanguzi wa Ndani kutumia mafunzo waliyapata yawe chachu ya mabadiliko kiutendaji kwa kutenda haki kwa wote bila kujali hali zao za kiuchumi na kijamii, ukilenga kuongeza na kuimarisha utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021 hadi 2024/2025 kwa kasi zaidi. 
Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani wakimfuatilia mada kutoka kwa mwezeshaji (hayupo pichani).

Akifunga mafunzo hayo ya kundi la pili lilokuwa na washiriki 55 yaliyoendeshwa kwa muda wa siku tano katika Ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji jijini Dodoma tarehe 10 Juni 2022, Jaji Masaju alisema, maneno haya ya kikatiba ya kutochelewasha haki bila sababu ya kimsingi ndiyo yanaunda dira ya Mahakama ya Tanzania inayosema upatikanaji wa haki kwa wakati na kwa wote. 

“Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani mnahusika sana katika mchakato wa utoaji haki kwa wakati, kila mmoja wenu kwa hatua yake akichelewesha mchakato wa matumizi ya fedha dira hii haitafanikisha adhima yake, msidhani anayeweza kuchelewa haki ni Jaji, Msajili, Hakimu au Mtengaji hata ninyi ni sehemu muhimu sana kiutendaji,"aliongeza Mhe. Masaju.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. George Masaju akisisitiza jambo kwa washiriki (hawapo pichani) wakati wa kufunga mafunzo ya Wahasibu na Wakanguzi wa Ndani yaliyoendeshwa kwa muda wa siku tano katika Ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji jijini Dodoma tarehe 10 Juni, 2022. 

Jaji Masaju akaendelea kusema, katika Muhimili huu watu wote tunategemeana na kila mtu ana nafasi yake ili kutekeleza dira awe Mlinzi, Dereva, Muhudumu, Karani na kada zote, mathalani bila mlinzi kuwepo ofisi ikaungua au mafaili yote yakaibiwa maana yake huduma hazitatolewa. 

“Msiende kufanya kazi zenu kwa mazoea ya awali mbadilike na mkawe chachu ili kwenda sambamba na maboresho yanayoendelea ndipo mtaweza kuutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama wa 2020/2021 – 2024/2025 kwa kuwa tayari mna uelewa mpana wa majukumu yanayopaswa kutekelezwa kwa kasi zaidi. Hivyo basi, Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani kile kitu mnachoweza kukifanya kwa ufanisi na kwa wakati ili kusaidia upatikanaji wa haki kwa mwananchi tukifanye kwa weledi na kwa wakati ipasavyo,”alibainisha Mhe. Jaji.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani wakimfuatilia mwezeshaji Muhasibu Mkuu Mwandamizi Bw. Juma Mwalusamba (aliyesimama mbele) kutoka Mahakama ya Tanzania akitoa mada katika mafunzo hayo. 

Katika Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muunganao wa Tanzania kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara, inaongelea usawa mbele ya sheria watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria ni wajibu wenu Wahasibu kuwahudumia wananchi wote bila ubaguzi wa aina yoyote bila kujali hali zao na hapo ndipo mtakuwa mnatekeleza dira ya Mahakama, alinukuu Jaji Masaju. 

Mhe. Masaju akazungumzia changamoto daima ni sehemu ya maisha, katumieni elimu mliyoipata kutatua changamoto za kimtandao badala ya kuwa walalamikaji. Mfano, unaposhindwa kukusanya maduhuli kwa njia ya POS jiulize utakuwa umepoteza kiasi gani cha fedha za serikali. Kuweni na tabia ya kubadilishana mawazo na vituo vingine badala ya kukaa na tatizo lako. 
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Bw. Sumera Manoti akifafanua jambo wakati wa kufunga mafunzo ya Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani (hawapo pichana), wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. George Masaju (katikati) na kulia ni Muhasibu Mkuu Mwandamizi wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Venant Kambuga wakifuatilia.

“Daima wasilianeni, shaurianeni Kanda na Kanda, Mkoa na Mkoa. Wasaidieni viongozi wenu kutekeleza majukumu yao katika kupanga na kutumia fedha za ofisi zenu. Nyie ndiyo washauri wakuu wa maafisa Masuhuli “Sub-warrant Holders” katika mambo ya fedha, hivyo tunawategemea. Toeni ushauri wa kitaalam na sio kwa woga,”alitoa rai Jaji Masaju. 

Aidha, Jaji Masaju alisema, Dunia ya sasa ipo katika wimbi la nne la maendeleo ya viwanda inayohusisha matumizi makubwa ya Teknolojia ya Habari na mawasiliano (TEHAMA). Mfahamu kuwa hata mifumo ya utendaji kazi mliyoisoma kupitia mafunzo yaliyomalizika imejikita katika matumizi ya TEHAMA. 
Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani wakimfuatilia mada kutoka kwa mwezeshaji (hayupo pichani).(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)

“Hivyo, niungane na viongozi wa juu wa Mahakama ya Tanzania kuwataka kuendelea kujifunza mifumo yote inayotengenezwa kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yetu. TEHAMA si tu inarahisisha utekelezaji wa majukumu bali inasaidia katika kuwafikia wananchi kwa wingi na kwa muda mfupi kwa mfano katika ukusanyaji wa maduhuli tunatumia Mashine za POS zenye mifumo ya TEHAMA. 

"Ninawaasa zinapotokea changamto za mifumo hiyo jitihada za utatuzi zifanyike haraka ili kuepuka kuchelewesha huduma na kupoteza mapato ya serikali,”alisisitiza Mhe. Masaju. 

Mafunzo hayo ya awamu ya pili kwa kundi la Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani inatokana na moja ya utekelezaji malengo kimkakati ya Mahakama ya Tanzania iliyoweka wa kuwajengea uwezo watumishi wa Mahakama wa ngazi zote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news