Mahakama Shinyanga yatekeleza agizo la Jaji Kiongozi kuwanoa Mahakimu kuhusu maadili

NA EMMANUEL OGUDA-Mahakama

MAHAKAMA Mkoa wa Shinyanga imetekeleza agizo la Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani kwa Mahakimu Wafawidhi wa Mikoa yote kuendesha mafunzo kuhusu maadili kwa Mahakimu wote nchini walio chini yao ili kutekeleza moja kati ya nguzo tatu zilizopo katika Mpango Mkakati wa Mahakama wa Miaka Mitano ili kutoa haki kwa wakati kwa wananchi.
Hatua hiyo inafautia uamuzi wa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga, Mhe Mary Mrio kuendesha mafunzo hayo katika maeneo tofauti tofauti kwa Mahakimu wote mkoani hapa kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga, Mahakama ya Wilaya Shinyanga, Mahakama ya Wilaya Kishapu na Mahakama ya Wilaya Kahama.

Akihitimisha mafunzo hayo alipokuwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kishapu, Mhe Mrio aliwahimiza Mahakimu wote kuwa waadilifu wanapotekeleza majukumu yao ya utoaji haki kwa wananchi pasipo huba, chuki wala upendeleo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi huyo alisema Mahakimu wote ndani ya Mkoa wa Shinyanga wanatakiwa kuzingatia Tangazo la Serikali (GN.1001/2020) linalowataka kuzingatia mambo muhimu, hususani kuwa Huru, Kutopendelea, Mgongano wa kimaslahi, Uadilifu, Usawa, Umahiri na Uaminifu (Independence, Impartiality, Conflict of interest, Integrity, Equality, Competence and Deligence’’).

Mhe. Mrio alisema hatakubali kuona Hakimu yoyote anakiuka maadili katika kutekeleza majukumu yake na kutotenda haki kwa wananchi kinyume na kiapo chake. Aidha, aliwataka Mahakimu kutojihusisha na vitendo ya rushwa wakati wote kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma.
 

Mhe. Mary Mrio akiwa kazini.

“Mahakama ya Tanzania haiko tayari kufumbia macho masuala ya rushwa kwa Mahakimu na watumishi wote ndani ya Mhimili huu wa utoaji haki nchini,” alisema mwishoni mwa mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Mahakama ya Tanzania chini ya Mpango wa Mafunzo (Training Policy 2019) kwa watumishi wake.

Kwa upande wao, Mahakimu waliopata mafunzo wameahidi kuzingatia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa mwaka 2020/2021 – 2024/2025 pamoja na maagizo yake ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi sambamba na kuzingatia maadili katika majukumu yao ya kila siku.

Aidha Mahakimu hao wameahidi kuwa Mahakama za Mkoa wa Shinyanga zitakuwa mfano wa kuigwa katika kutoaji haki kwa wakati kufuatia shindano lililoanzishwa hivi karibuni na Mahakama ya Tanzania kutafuata Mahakama inayotoa huduma bora kwa wananchi (Court of Excellence Perfomance). Mapema mwezi Machi, 2022 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Shinyanga, Mhe Athumani Matuma aliwataka Mahakimu na watumishi wote kuhakikisha Kanda hiyo inaibuka mshindi katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments