Mahakama yahairisha kesi inayomkabili Mfalme Zumaridi

NA DIRAMAKINI

MAHAKAMA imehairisha kesi ya kushambulia na kuzuia maofisa wa Serikali kutekeleza majukumu yao inayomkabili Diana Bundala (Mfalme Zumaridi) baada ya mshtakiwa namba saba katika kesi hiyo, Anitha Isaya kushindwa kufika mahakamani.

Kesi hiyo imeitwa Juni 28, 2022 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza kwa ajili ya kuendelea kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka.

Aidha, kabla ya shahidi Jamhuri kuanza kusikilizwa Wakili wa Serikali Mwandamizi, Emmanuel Luvinga akisaidiana na Dorcas Akyoo na wakili, Deogratius Rumanyika wameiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi mshtakiwa huyo atakapokuwepo mahakamani hapo.

Akizungumza mahakamani hapo, Mdhamini wa mshtakiwa huyo, Anna Daniel ameiambia mahakama hiyo kwamba Anitha ameshindwa kufika kutokana na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza ya Sekouture akisumbuliwa na ugonjwa wa Malaria tangu Juni 23, 2022.

Katika kesi hiyo mashahidi wanne wa upande wa mashtaka (Jamhuri) wameshatoa ushahidi wao huku upande huo ukimleta shahidi mwingine leo ambaye ni askari wa upelelezi wa Jeshi la Polisi mkoani humo mwenye namba F1468, Sajenti Joanes Mashaka kwa ajili ya kuendelea na kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo.

Hata hivyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Monica Ndyekobora baada ya kusikiliza hoja hiyo ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 11, 2022 itakapoitwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizaji wa ushahidi.

Katika kesi hiyo ya msingi, Mfalme Zumaridi na wenzake wanane wanaowakilishwa na Wakili, Erick Mutta na Steven Kitale wanashtakiwa kwa kushambulia na kuwazuia maofisa wa serikali kutekeleza majukumu yao kosa wanalodaiwa kulitenda Februari 23, 2022 nyumbani kwa Mfalme Zumaridi katika Mtaa wa Buguku Kata ya Mkolani jijini Mwanza.

Katika hatua nyingine, mahakama hiyo iliahirisha ya kesi ya Jinai namba 11/2022 inayomkabili Mfalme Zumaridi peke yake kwa kile kilichoelezwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Emmanuel Luvinga kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Katika kesi hiyo, Mfalme Zumaridi anakabiliwa na shtaka moja la usafirishaji haramu wa binadamu wakiwemo watoto wenye umri kati ya miaka minne hadi 17.

Baada ya Hakimu Mwandamizi wa mahakama hiyo, Monica Ndyekobora kusikiliza hoja hiyo ya upande wa mshtaka aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 11, 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news