MAMBO MAPYA AONGEZA: Kwa kweli amepania, kazi kuiendeleza, Geita ametujuza

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan akisalimiana na wananchi wa Kata ya Bwanga Wilaya ya Chato mkoani Geita alipokua njiani akielekea mkoani Kagera kwa ajili ya kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu iliyoanza Juni 8, 2022 amesema kuwa, miradi iliyoanza Awamu ya Tano na ile mipya itatekelezwa kikamilifu.
"Awamu iliyopita nilikuwa Makamu wa Rais chini ya Kaka yangu marehemu John Pombe Magufuli, alinifundisha mambo mengi sana, niliisoma dhamira yake vizuri sana, jinsi ya kuipeleka nchi hii,nataka niwahakikishie dhamira ile ile tunakwenda nayo, maendeleo kwa wananchi hakuna hata mradi hata mmoja tuliouanza nyuma ambao utakufa na hatutauendeleza.

"Lakini na ile mipya ambayo inakuja ni kwa dhamira ile ile, kwa hiyo niwahakikishie halijaharibika jambo, Serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), yeyote anayekaa kuongoza Serikali, lengo ni kuhudumia wananchi,kupeleka maendeleo kwa wananchi na tutafanya hivyo, jinsi hali ya uchumi wa nchi utakavyoruhusu,"Mheshimiwa Rais ameweleza wananchi.

Ni wazi kuwa, malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita yamehakisi kuharakisha maendeleo ya wananchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyoanza huko nyuma na mipya iliyobuniwa sasa. 
 
Hii ni hatua njema ambayo kila mpenda maendeleo ana shauku ya kushirikiana hatua kwa hatua na Serikali ili iweze kutekelezwa haraka ikiwemo maji, nishati, afya, elimu, miundombinu na mingine mingi. Ungana na mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande ujifunze jambo kupitia shairi. Karibu;

A).Mambo Awamu ya Tano, ya Sita yatekeleza,
Chato kwenye mkutano, Rais ameeleza,
Amekonga nyoyo mno, jinsi amesisitiza,
Viongozi kazi kubwa, ni kuhudumia watu.

B).Akiwako ziarani, Geita ametujuza,
Ujumbe ule wa ndani, ambao watutuliza,
Miradi yote nchini, kukamilisha aweza,
Viongozi kazi kubwa, ni kuhudumia watu.

C).Awamu ya Tano ile, Magufuli liongoza,
Ilianza kazi ile, miradi kutekeleza,
Japo imekwenda mbele, mingi hakuimaliza,
Viongozi kazi kubwa, ni kuhudumia watu.

D).Samia keshaingia, azidi kutekeleza,
Pesa atutafutia, taarifa zatujuza,
Kwa kweli amepania, kazi kuiendeleza,
Viongozi kazi kubwa, ni kuhudumia watu.

E).Mwendokasi reli yetu, ujenzi aendeleza,
Na miundombinu yetu, hataki kuikawiza,
Na tena Rais wetu, mambo mapya aongeza,
Viongozi kazi kubwa, ni kuhudumia watu.

F).Tumeona shule nyingi, madarasa kaongeza,
Na watoto wetu wengi, elimu waendeleza,
Hilo jambo la msingi, taifa kuendeleza,
Viongozi kazi kubwa, ni kuhudumia watu.

H).Ona miradi ya maji, serikali yaongeza,
Rais anahitaji, umbali kuupunguza,
Wanawake wasotaji, ndoo vichwani kupoza,
Viongozi kazi kubwa, ni kuhudumia watu.

I).Rais tunamuona, marafiki aongeza,
Lengo lake twaliona, ni fursa kuongeza,
Wenye macho wanaona, wageni navyokatiza,
Viongozi kazi kubwa, ni kuhudumia watu.

J).Tena ubunifu wake, Rais twampongeza,
Kwa uigizaji wake, watalii kuongeza,
Na nchi filamu yake, mapato tutaongeza,
Viongozi kazi kubwa, ni kuhudumia watu.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news