Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar asisitiza umuhimu wa kuwajali wenye mahitaji maalum

NA DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa NURU FOUNDATION ambaye pia ni Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib, ameitaka jamii kujikita katika kuwalea na kuwatunza watoto yatima na wenye mahitaji maalum na kuhakikisha wanapata haki zao kama inavyostahili.
Mama Zainab ameyasema hayo jioni ya Juni 28, 2022, wakati wa Kikao cha Kamati Maalum ya Kuandaa Dua ya Kuiombea Nchi, pamoja na Chakula cha Mchana kwa ajili ya Watoto Yatima, Siku ya Eid Pili ya Mfunguo Tatu Mwaka huu, kilichofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil, Kikwajuni jijini Zanzibar.
Amesema suala la kuwatunza watoto yatima ni lajamii yote na kwamba kukosekana kwa wazazi ni katika mipango yake Mwenyezi Mungu na hakuna ajuwaye mwisho wake wa kuishi hapa duniani.

"Sote kwa pamoja tuungemkono juhudi za kuwalea na kuwasaidia wengine hasa watoto yatima na wenye mahitaji maalum kwani mtoto wako unayempenda anaweza kuwa ni yatima mtarajiwa wa kesho,"amesisitiza Mama Zainab.
Mama Zainab ameeleza kuwa taasisi ya Nuru sambamba na Kamati wanaendelea kupokea michango mbalimbali ili kufanikisha kwa ufanisi hafla hiyo muhimu.

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Bi. Mgeni Hassan Juma, amesema suala la kuwakutanisha watoto, kuomba Dua na kuungana nao katika chakula cha mchana kwa pamoja, ni baraka na upendo mkubwa jambo ambalo linahitaji kufanikishwa na kuendelezwa, kwa hali na mali, na kwa kadiri itakavyowezekana.
Naye Mke wa Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu Bi. Asha Balozi, amesema kukamilika kwa jambo hilo kutapelekea watoto yatima kuamini kwamba Serikali na jamii wanawajali na wako pamoja nao.

Kikao hicho cha muendelezo wa maandalizi kimewakutanisha pia wajumbe wa kamati mbalimbali za maandalizi ya hafla hiyo.

Maandalizi ya hafla hiyo yanasimamiwa kwa mashirikiano ya Taasisi ya Nuru, pamoja na Wake wa Viongozi Wakuu wa Serikali akiwemo Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Maryam Mwinyi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news