MWENDOKASI HADI MBAGALA:Ni kasi ya Serikali, wananchi kuwajali

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuanzisha,kuendeleza na kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ile ya kimkakati ili kuhakikisha inasaidia kuharakisha maendeleo nchini na kuhudumia wananchi kwa ufanisi.

Miongoni mwa miradi hiyo, ni ujenzi wa Awamu ya Pili ya Barabara ya Mabasi ya Mwendokasi kuanzia Kariakoo hadi Mbagala ambayo ina urefu kwa kilomita 20 ambao unagharimu mabilioni ya fedha, kwa sasa mradi huo umeonesha ishara njema na wananchi huenda wakaanza kufurahia huduma zitolewazo kupitia barabara hiyo mpya.

Tayari tumedokezwa na Wakala ya Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kuwa,kuanzia Juni 24, mwaka huu watatoa huduma kwa wananchi, ingawa kwa siku chache za awali.

Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande kupitia shairi lake anakupa dondo muhimu kuhusu mwanzo huu mpya, ambao unaonesha kuwa, siku za karibuni kuna mambo mazuri na makubwa yanakuja Mbagala, hatua kwa hatua jifunze jambo hapa;


1:Mbagala tunawajali, ujumbe huo halali,
Mbagala tena siyo mbali, itatulia msuli,
Kuteleza ni halali, ule mwendo wa ukweli,
Mabasi ya mwendokasi, sasa hadi Rangi Tatu.

2:Pakuanzia mahali, ni karibu siyo mbali,
Sabasaba pale halali, maonesho ya ukweli,
Kwenda kurudi si mbali, ya kawaida nauli,
Mabasi ya mwendokasi, sasa hadi Rangi Tatu.

3:Tena ni trela hili, wiki zaidi ya mbili,
Za maonesho ni kweli, andaa yako nauli,
Mwenyewe utakubali, usafiri wa ukweli,
Mabasi ya mwendokasi, sasa hadi Rangi Tatu.

4:Kwa mwendo ule halali, na mabasi ya ukweli,
Talii wala si mbali, barabara mpya dili,
Ni kasi ya Serikali, wananchi kuwajali,
Mabasi ya mwendokasi, sasa hadi Rangi Tatu.

5:Ni vionjo hivi kweli, ambavyo twavikubali,
Huko hakuna kabali, ni utulivu kamili,
Kwa taratibu za kweli, na mkononi nauli,
Mabasi ya mwendokasi, sasa hadi Rangi Tatu.

6:Unakwenda Muhimbili, usafiri bomba kweli,
Mwendokasi ya halali, mabasi ni mengi kweli,
Wengi tumeyakubali, tuendako siyo mbali,
Mabasi ya Mwendokasi, sasa hadi Rangi Tatu.

7:Kwa kweli tunakubali, mradi wa Serikali,
Kote yaliko kwa kweli, usafiri ni kamili,
Ni mradi wa akili, hadi Kibaha kamili,
Mabasi ya mwendokasi, sasa hadi Rangi Tatu.

8:Ingawa ni wiki mbili, huo ni mwanzo kamili,
Jenga msikae tuli, tayari mna vibali,
Mbagala kuwe ni dili, kusibakie mbali,
Mabasi ya mwendokasi, sasa hadi Rangi Tatu.

9:Dasalamu jiji hili, utamu kama asali,
Usafiri ni dalili, ubora wake kwa kweli,
Ni vitendo si kauli, ifanyavyo Serikali,
Mabasi ya mwendokasi, sasa hadi Rangi Tatu.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news