Plan International, Wanahabari kushirikiana mapambano ukatili dhidi ya wanawake, watoto Geita

NA MUTTA ROBERT

UKATI ni mateso.Ni unyanyasaji. Ni unyama.Ni adhabu kali na isiyo ya kawaida dhidi ya binadamu inayomnyima raha na furaha. Ukatili mara nyingi husababishwa kwa makusudi.Ukatili unaweza kuwa wa kimwili,kiakili au kisaikolojia.
Pamoja na kwamba makundi yote ya watu yanafanyiwa ukatili, lakini kundi la watoto ni moja ya kundi ambalo ni tete kwa kufanyiwa ukatili kutokana na kuwa kundi ambalo halina uwezo wa kujitetea kutokana na umri wake.

Kwa mujibu wa Azimio la Kimataifa la Haki za Mtoto (Convention on the Rights of the Child),Mkataba wa Afrika juu ya Haki na Ustawi wa Mtoto (Africa Charter on the Rights and Welfare of the Child) na Sheria ya Mtoto ya Tanzania namba 21 ya Mwaka 2009 vyote vinamtaja mtoto kama mtu ambaye ana umri usiozidi miaka 18.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) mwaka 2009 lilifanya utafiti kuhusu Ukatili Dhidi ya Watoto Tanzania na Muhtasari wa Kuenea kwa Ukatili wa Kijinsia, Kimwili na Kiakili, Muktadha wa matukio ya Ukatili wa Kijinsia, Afya na Athari ya Tabia ya Ukatili iliyotokea utotoni,uiliochapishwa 2011 ulionyesha ukatili dhidi ya mtoto ni mkubwa na watoto wa kike ndiyo walikuwa wanaongoza kwa kufanyiwa ukatili zaidi kuliko wavulana.
Kutokana na matukio ya ukatili dhidi ya mtoto kuongezeka katika jamii, Serikali ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali kupambana ili kukomesha ukatili dhidi ya mtoto ikiwa ni pamoja na kutungasheria ya kumlinda mtoto ya mwaka 2009 pamoja na kuanzisha Mwongozo wa uratibu wa mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (mtakuwwa) 2017/18 – 2021/22.

Katika jitihada za kutokomeza ukatili dhidi ya mtoto hapa nchini wadau mbalimbali wanashirikia mapambano ikiwa ni pamoja na shirika lisilo la kiserikali la Plan International ambalo shughuli zake za msingi zimelenga ustawi wa mtoto.

Miradi inayotekelezwa na shirika hilo ni pamoja na miradi ya maji kwenye shule mbalimbali ili mtoto wa kike aweze kupata maji hasa kipindi cha hedhi ili aweze kuendelea na masomo yake kama kawaida bila kukatisha masomo kwa sababu ya kukosa maji kwani ni haki ya mtoto kupata elimu.
Meneja wa Plan International Mkoa wa Geita, Adolf Kaindoa amesema shirika hilo msingi wake mkubwa ni mtoto,hivyo miradi yake mingi inajikita kustawisha na kudumisha ulinzi wa mtoto ili aweze kupata haki zake.

Kaindoa ametaja baadhi ya miradi inayotekelezwa na shirika hilo katika Mkoa wa Geita ambayo inamlenga mtoto moja kwa moja ni pamoja na mradi wa elimu ambao pia unawaandaa walimu wanaofundisha watoto wa chekechea na madarasa ya kwanza ili kumudu kufundisha watoto hao kwa ufanisi hasa kusoma,kuandika na kuhesabu maarufu kama KKK tatu.

Miradi mingine ni kuwezesha wasichana kuendelea na masomo,mradi wa kutokomeza ajira hatarishi na ukatili dhidi ya mtoto katika maeneo ya madini (migodini) na maeneo ya uvuvi,mradi wa ufadhili wa mawasiliano, mradi wa kumlinda mtoto wa kike dhidi ya mila zenye madhara pamoja na mradi wa jinsia na ujumuishi.

Kaindoa amesema kuwa, katika kulinda mtoto na kuendeleza mapambano ya ukatili dhidi ya mtoto shirika hilo limeamua kuunganisha nguvu kwa kushirikiana na kundi la waandishi wa habari katika mkoa wa Geita kwa kuwatafutia wataalam waliobobea katika taaluma ya ustawi wa jamii na taaluma ya habari waweze kuwanoa zaidi ili kuongeza uwezo wa kutambua ukatili kwa kwatoto na kuripoti habari hizo kwa usahihi na kwa tija zaidi.

Amesema kuwa, shirika hilo limeamua kutoa mafunzo maalum kwa waandishi mbalimbali wa habari ambao shirika hilo linaamini kuwa watakuwa msaada mkubwa wa kuibua matukio yote ya ukali yanayotendeka katika jamii ambayo yamejificha ili hatua ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.

Meneja wa Plan International Adolf Kaindoa akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari 20 wa kiume na 10 wa kike yaliyofanyika katika Ukumbi wa Alphendo Hotel Mjini Geita kwa siku tatu kuanzia Aprili 22,2022 na kuhitimishwa Aprili 22,2022 alisema malengo ya mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari katika mkoa wa Geita ili waweze kuendelea kuibua na kuripoti ukatili dhidi ya watoto ili jamii iweze kupata uelewa na namna ya kutokomeza ukatili kwa watoto.
Mkufunzi wa mafunzo hayo, Frank Moshi ambaye pia ni Afisa Ustawi wa Jamii katika Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita amesema kuwa, hali ya ukatili katika mkoa huo siyo ya kuridhisha, lakini juhudi mbalimbali zinaendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na kuelimisha jamii kupitia vyombo vya habari.

Ameeleza kuwa, waandishi wa habari katika mkoa huo wamekuwa masaada mkubwa katika kuibua matukio mengi ya ukatili ambayo yamekuwa yakisaidia Serikali kuyajua na kuchukua hatua za kisheria kwa wahusika na wakati mwingine kutoa ushauri nasaha kwa wahusika kulingana na asili ya tatizo lenyewe.

Frank Moshi ameeleza kuwa, mafunzo hayo kwa waandishi wa habari yataboresha kiwango cha kuripoti matukio ya ukatili kwa sababu waandishi hao watakuwa na uwezo wa kutambua aina zote za ukatili, madhara yake pamoja na kuyaripoti kwenye vyombo vya habari lakini pia kuendelea kuelimisha jamii kupitia vipindi mbalimbali kwenye vyombo vyao vya habari.

Naye Dotto Bulendu ambaye ni Mkurugenzi wa Radio SAUT jijini Mwanza na Mhadhiri katika Chuo Kichuu cha Mtakatifu Agostino Mwanza ambaye alifundisha namna bora ya kuibua na kuandika habari zenye kuleta tija na kuleta mabadiliko katika jamii amesema, programu hiyo iliyoandaliwa na Plan International itasaidia kwa kiwango kikubwa mapambano ya ukatili kwa watoto.

Bulendu amesema kuwa, waandishi wa habari wana dhima ya kuandika na kutangaza habari zinazoonyesha mzizi wa tatizo lenyewe kwenye jamii inayochangia kusababisha ukatili kwa watoto ili jamii itambue na kuchukua hatua za kukomesha chanzo cha tatizo husika.

Baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo wamesema, ujuzi walioupata kutoka kwa mtaalamu wa ustawi wa jamii umewawezesha kutambua baadhi ya matendo ambayo ni ukatili kwa watoto na awali walikuwa hawayatambui kama ni ukatili.
Aidha, wamesema mafunzo hayo yamewaongezea uelewa wa namna bora ya kuandika habari za ukatili dhidi ya mtoto zenye kuchochea mabadiliko katika sera,sheria na kanuni mbalimbali au mila baada ya kupata mafunzo kutoka kwa mtaalam wa masuala ya habari na utangazaji.

Salma Mrisho ambaye ni Mwandishi wa Habari na mshiriki wa mafunzo hayo amesema kuwa, amenufaika na mafunzo hayo kwani ameelewa ni jinsi gani bora ya kuandika habari za ukatili dhidi ya mtoto na jinsi ya kumlindia hadhi yake ya leo na wakati ujao bila kumuumiza yenye na jamii inayomzunguka.

Jitihada zinazofanywa na Serikali pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali ya kupambana na ukatili dhidi ya mtoto na mwanamke jamii haina budi kushirikiana katika mapambano hayo ili kujenga jamii yaenye upendo na mshikamano kwa mustakabali na maendeleo endelevu ya taifa letu ba dunia ambayo ni salama kwa kuishi. Tunaweza kuishi bila ukatili kwa wanawake na kwa watoto.

Post a Comment

0 Comments