Rais Samia awataka wananchi kuvuta subira ardhi ya hifadhi

NA RICHARD BAGOLELE

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa Kata ya Bwanga wilayani Chato mkoani Geita kuwa na subira kuhusu urekebishaji wa mipaka ya hifadhi ili kuruhusu sehemu ya ardhi hiyo kutumika katika shughuli za kibinadamu.
Mheshimiwa Rais amesema, suala la uhaba wa ardhi sio la Bwanga tu bali ni tatizo la nchi nzima kutokana na mahitaji ya ardhi kuwa makubwa.

Rais Samia ametoa rai hiyo leo wakati akisalimiana na wananchi wa Kata ya Bwanga iliyopo wilayani Chato akiwa njiani kuelekea mkoani Kagera ambapo atakuwa na ziara ya siku tatu.
"Tutachukua hatua ya kuangalia hifadhi zetu na mipaka yake, halafu tutato maamuzi," amesema Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika hatua nyingine Rais Samia amewataka wafugaji wenye mifugo mingi kupunguza idadi ya mifugo hiyo ili kukabiliana na uhaba wa ardhi ambapo amesema iwapo viwanda vingi vya nyama vyama vitaanzishwa kutasaidia kudhibiti ongezeko la mifungo na itasaidia kuuza nyama nje ya nchi.
Mapema akiongea na wananchi hao,Mbunge wa Jimbo la Chato, Mhe. Dkt.Medard Kalemani amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuridhia ombi la kutoa sehemu ardhi ya shamba la miti la Silayo angalau kilomita nane ili ziweze kusaidia wananchi wa Kata ya Bwanga ili kukidhi mahitaji ya makazi, kilimo na ufugaji.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule amesema katika kipindi cha muda mfupi mkoa wa Geita umepata shilingi bilioni 190 kwa ajili ya miradi ya elimu, afya, barabara, umeme na maji ambapo kwa upande wa Wilaya ya Chato imeweza kupata shilingi bilioni 22.2 katika miradi ya afya, elimu, maji na barabara.
Katika uwanja wa ndege wa Geita uliopo Chato, Rais Samia Suluhu Hassan amepokewa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule, vingozi wa CCM na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ambapo anaelekea mkoani Kagera kwa ajili ya kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu inayoanza leo Juni 8, 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news