RC Kunenge kuzindua kampeni kabambe ya utunzaji mazingira, nishati mbadala

NA ROTARY HAULE 

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge anatarajiwa kuzindua kampeni ya uhamasishaji wa utunzaji mazingira na matumizi ya nishati mbadala itakayofanyika kesho katika viwanja vya Stendi ya zamani ya Mailimoja vilivyopo Kibaha Mjini.
Mheshimiwa Abubakar Kunenge, Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

Uzinduzi wa kampeni hiyo unafanyika chini ya maandalizi na usimamizi wa Taasisi ya Vijana ya Uhamasishaji na Utunzaji wa Mazingira ya Tanzania Environment and Youth Festival (TEYF).

Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Eustard Rwegoshora,amewaambia Waandishi wa habari leo Mjini Kibaha kuwa maandalizi ya uzinduzi huo yamekamilika na kwamba ifikapo Juni 11 Mkuu wa Mkoa ataungana na wadau wa Mazingira kuzindua kampeni hiyo.

Rwegoshora,amesema kuwa baada ya uzinduzi huo taasisi yake ya TEYF itafanya kampeni kubwa ya kupita katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu juu ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa jamii .

Amesema, elimu itakayotolewa itahusisha umuhimu wa matumizi ya nishati mbadala ikiwemo gesi,umeme wa Sola pamoja na kuhakikisha jamii inaelimishwa juu ya madhara ya ukataji miti hivyo.

Aidha, Rwegoshora ameongeza kuwa mbali na kutoa elimu hiyo lakini kazi kubwa ni kuhakikisha wanashirikiana na wamiliki wa viwanda waliopo Mkoani Pwani kupanda miti katika maeneo yao ya viwanda.
Amesema kuwa, Taasisi ya Tanzania Environment and Youth Festival itapita katika Kila kiwanda na kupanda miti bure huku akisema kazi ya wahusika wa viwanda itakuwa ni kuitunza miti hiyo mpaka itakapostawi.

"Baada ya Mkuu wa Mkoa kuzindua kampeni hii,taasisi yetu kwa kushirikiana na vijana wake itapita kila kiwanda na kugawa miti bure na kisha kuipanda lakini watunzaji wakubwa watakuwa wahusika wa viwanda,"amesema Rwegoshora.

Amesema kuwa ,baada ya kumaliza Mkoa wa Pwani zoezi hilo litaendelea katika Mikoa mingine nchini na kwamba lengo ni kuhakikisha jamii inajengewa uelewa juu ya utunzaji wa mazingira.

Rwegoshora,amesema suala la utunzaji na uhifadhi wa mazingira ni jukumu la wananchi na jamii nzima kiujumla na kwamba kila mmoja anapaswa kushiriki katika maeneo anayoishi ili kuweza kulinda raslimali za nchi.
Katika hatua nyingine, Rwegoshora amesema katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ushiriki mdogo wa taasisi za Serikali.

Amesema kuwa,katika taasisi nyingi za Serikali zimekuwa na dhana ya kuwa majukumu ya utunzaji wa mazingira ya misitu lipo kwa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na kusema dhana hiyo inapaswa kuachwa na ikiwezekana kila taasisi hiwe sehemu ya kutambua umuhimu wa mazingira.

"Tusiwaachie TFS pekee yao kulinda misitu lakini hata taasisi nyingine zinaweza kushiriki jambo hili ,naiomba Serikali kuweka utaratibu mzuri ambao utawezesha kila taasisi kuona umuhimu wa kushiriki katika masuala haya ya utunzaji wa mazingira,"amesema Rwegoshora.

Hata hivyo, Rwegoshora amewaomba wananchi kuungana na taasisi ya TEYF kukabiliana na wimbi la uharibifu wa mazingira kwa kupanda miti katika maeneo pamoja na kuendelea na matumizi ya nishati mbadala.

Post a Comment

0 Comments