REA YAUNGA MKONO SERIKALI KUBORESHA MAKAZI MAPYA YA WANAOHAMIA KUTOKA NGORONGORO

NA VERONICA SIMBA-REA

WAKALA wa Nishati Vijijini nchini (REA) umeunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita zinazolenga kuboresha eneo la Kijiji cha Msomera, Kata ya Misima, wilayani Handeni, ambalo ni makazi mapya ya wananchi wanaohamia kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro mkoani Arusha.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo (kulia) akizungumza na Mbunge wa Handeni Vijijini, Mhandisi John Sallu (katikati), Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni ambaye ni Katibu Tawala, Mashaka Mgeta (wa pili-kulia) na wataalamu mbalimbali wa REA na TANESCO pamoja na Wakandarasi, Juni 13, 2022 wakati wa ziara kukagua maendeleo ya mradi wa kuunganisha umeme katika makazi mapya ya wananchi wanaohamia kijiji cha Msomera mkoani Tanga, kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.(Picha zote na Veronica Simba-REA).

Hayo yamebainishwa wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo aliyefuatana na Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy wilayani Handeni, jana Juni 13, 2022.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara husika, Viongozi hao walisema REA imeunga mkono juhudi hizo za Serikali kwa kuhakikisha wananchi wanaohamia eneo hilo wanapata nishati ya umeme ambayo ni muhimu kwa kila mtu.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Msomera, Kata ya Misima, Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga, Martin Oleikayo Paraketi (wa kwanza kushoto), akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini Wakili Julius Kalolo, Juni 13, 2022 wakati wa ziara kukagua maendeleo ya mradi wa kuunganisha umeme katika makazi mapya ya wananchi wanaohamia kijiji cha Msomera kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro. Kutoka kulia ni Mbunge wa Handeni Vijijini, Mhandisi John Sallu na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy.

“Mpango wa Serikali kuwaomba baadhi ya wakazi wa Ngorongoro kuhamia katika eneo hili umefanya mahitaji ya nishati kuwa makubwa kuliko bajeti tuliyoipanga awali; hivyo tumetembelea tujionee mahitaji halisi ili tukapitishe nyongeza ya bajeti itakayokidhi mahitaji ya wananchi wote wa eneo hili,” alisema Wakili Kalolo.

Aidha, aliongeza kuwa, upelekaji umeme umehusisha pia kuongeza wigo kwa wakazi wa vijiji jirani ambao walikuwa hawajafikiwa na nishati hiyo ili nao wafaidi huduma hiyo na kuboresha hali ya maisha.

Akifafanua zaidi, Mkurugenzi Mkuu wa REA, alisema tayari ujenzi wa kilomita 23 kati ya 30 za njia ya kupeleka umeme katika eneo husika zimekwishakamilika na transfoma iko tayari kuwashwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy akizungumza na waandishi wa habari Juni 13, 2022 wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo (hayupo pichani), kukagua maendeleo ya mradi wa kuunganisha umeme katika makazi mapya ya wananchi wanaohamia kijiji cha Msomera, Kata ya Misima, Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga, kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro. Wa kwanza kulia ni Mbunge wa Handeni Vijijini, Mhandisi John Sallu.

Pia, alibainisha kuwa baadhi ya nyumba zimekwishaungiwa umeme na kwamba Mradi unaendelea.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Saidy alieleza kuwa Serikali imeahidi kutoa pesa kwa ajili ya kuongeza wigo wa upelekaji umeme kwa kilomita mbili zaidi kwa kila kijiji ili kuongezea kilomita moja ya awali ambayo kimsingi ilikuwa na lengo kuu la kufikisha umeme mkubwa katika kila kijiji.

“Kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga na maeneo yote ya Tanzania, wasiwe na hofu kwani ile kilomita moja ni ya awali, lakini kila kijiji kitapata kilomita mbili za ule umeme mdogo na hivyo tunatarajia tutafikia wateja wengi zaidi,” alisisitiza.

Mhandisi Saidy aliongeza kuwa,, REA inatekeleza pia Mradi wa Ujazilizi ambapo jumla ya vitongoji 85 vimekwishafikiwa na huduma na kuna ongezeko la vijiji 51 zaidi ambavyo pia vitapatiwa umeme kupitia Mradi husika mkoani humo.

Alisema, kuna jumla ya Kandarasi Sita zinazotekelezwa mkoani Tanga, ambazo alizitaja kuwa mbili kati yake ni za Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza, Kandarasi Tatu ni za Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili na Kandarasi Moja ni ya Mradi wa ujazilizi.
Mbunge wa Handeni Vijijini, Mhandisi John Sallu (kulia) na Mwenyekiti wa Kijiji cha Msomera, Kata ya Misima, Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga, Martin Oleikayo Paraketi, wakiwa katika picha ya ukumbusho Juni 13, 2022 wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini Wakili Julius Kalolo na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy kukagua maendeleo ya mradi wa kuunganisha umeme katika makazi mapya ya wananchi wanaohamia kijiji cha Msomera kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.

Kwa upande wake, Mbunge wa Handeni Vijijini, Mhandisi John Sallu, aliishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan akieleza kuwa imekuwa mstari wa mbele katika kuwapambania wananchi katika kuhakikisha mazingira wanayoishi yanakuwa bora zaidi ikiwemo kuwapelekea nishati ya umeme.

Akieleza zaidi, Mheshimiwa Sallu alibainisha kuwa, katika Jimbo lake kasi ya utekelezaji wa miradi ya REA inakwenda vizuri na kwamba kupitia ziara ya viongozi wa REA, baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa na upungufu yametolewa ahadi ya kufikishiwa nishati ya umeme.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Msomera, Kata ya Misima, Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga, Martin Oleikayo Paraketi (wa kwanza kushoto), akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini Wakili Julius Kalolo (mwenye kofia ya bluu), Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy (mwenye kofia nyeusi na Ujumbe waliofuatana nao Juni 13, 2022 wakati wa ziara kukagua maendeleo ya mradi wa kuunganisha umeme katika makazi mapya ya wananchi wanaohamia kijiji cha Msomera kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro. Wa pili-kushoto ni Mbunge wa Handeni Vijijini, Mhandisi John Sallu.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Msomera, Martin Oleikayo Parakett alimshukuru Mungu, Rais Samia pamoja na viongozi walio chini yake hususan wa Wizara ya Nishati, REA na TANESCO kwa kuona umuhimu wa kukipelekea kijiji hicho umeme.

Alitoa rai kuwa nishati hiyo itolewe kwa usawa kwa wakazi wote ambao wanajumuisha wenyeji pamoja na wageni wanaohamia.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mbunge wa Handeni Vijijini, Mhandisi John Sallu (wa nne kutoka kulia), Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni ambaye ni Katibu Tawala, Mashaka Mgeta (wa sita-kulia) na wataalamu mbalimbali wa REA na TANESCO pamoja na Wakandarasi, Juni 13, 2022 wakati wa ziara kukagua maendeleo ya mradi wa kuunganisha umeme katika makazi mapya ya wananchi wanaohamia kijiji cha Msomera, wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga, kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.

Wengine walioshiriki katika ziara hiyo ni Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka REA, Mhandisi Thomas Mbaga, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Tanga Mhandisi Julius Sabu, Wataalam kutoka TANESCO pamoja na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani Tanga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news