Rhobi Samwelly afunguka kuhusu umuhimu wa kuwapa thamani watoto

NA FRESHA KINASA

IKIWA Juni 12 ya kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira za Watoto, Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia Mkoa wa Mara Rhobi Samwelly, ameishauri jamii kushiriki kikamilifu katika kuwalinda dhidi ya ukatili na kuwawezesha watoto kusudi waweze kufikia ndoto zao. 
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT),Rhobi Samwelly akiwa na Balozi wa Marekani nchini Ufaransa,Denise Campbell Bauer (katikati).

Rhobi amesema kuwa, watoto wanapaswa kutazamwa kwa jicho la pekee kutokana na baadhi yao kukumbwa na kadhia mbalimbali ikiwemo kufanyiwa vitendo vya ukatili na ndugu wa karibu ikiwemo vitendo vya ulawiti na wakati mwingine kupewa majukumu mazito ya kuhudumia familia zao, jambo ambalo amesema linafifisha wasiweze kufikia ndoto zao kwa siku za usoni. 

Ameyasema hayo wakati akizungumza na DIRAMAKINI leo Juni 11, 2022 ambapo amebainisha kuwa, Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira za Watoto itumiwe na wazazi na walezi kufanya tathmini ya kina ambayo itawezesha watoto kuendelea kukua katika msingi bora na kuondokana na vikwazo vinavyowakabili huku akitoa rai kwa jamii kuweka msukumo wa dhati wa pamoja wa kushirikiana kuwawezesha kufika sehemu bora.

"Watoto waandaliwe vyema kwa kupewa malezi bora na mahitaji yao ya msingi, haipendezi kuona watoto wadogo umri wao unaruhusu kuwa katika masomo (shule) wakijishughulisha na biashara tena wakati mwingine wameagizwa na wazazi au walezi wao wakati mwingine wanapewa jukumu la kuhudumia familia. Si jukumu la Serikali pekee ama mashirika ya kiraia kuwalinda watoto bali jamii yote ishiriki kuwatengenezea mazingira bora ambayo yatachagiza kufikia malengo yao,"amesema Rhobi.
"Na wengine hukatisha masomo kutokana na changamoto mbalimbali katika familia zao ambazo jamii ikiungana inaweza kuzitatua, kila mmoja kwa nafasi yake awe sehemu ya kuwafanya watoto wafurahi na wapate haki zao ikiwemo haki ya kulindwa, haki ya kuishi, kushirikishwa, na pia wapate elimu na kufundishwa maadili mema wasijiingize katika vitendo vya wizi, ukahaba, uharibifu na utumiaji wa dawa za kulevya ili kesho yao iwe yenye tija kwao na taifa pia,"amesema Rhobi. 

Aidha, Rhobi amehimiza mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo zinarudisha nyuma maendeleo na haki za watoto wa kike ziachwe ikiwemo ukeketaji kwani hausaidii kufikia ndoto zao hususani katika Jamii za kifugaji ambazo bado zinakumbatia mila hiyo. 

"Ni muda umefika tujiulize na tuziache, lazima tujitathmini na kutazama ukeketaji umesaidiaje maendeleo ya mwanamke na mtoto wa kike katika jamii za kifugaji tuangalie je?, Zinadidimiza ndoto za watoto hawa ama zinasaidia kufikia ndoto zao,waliotamani kuwa wanasheria, walimu,madaktari wataalamu au viongozi wa juu katika ngazi za kitaifa wamefanikiwa,"amesema.

"Wako wanawake wangapi katika jamii hizi za kifugaji au tunazo mila na desturi ambazo zinapunguza ulinzi kwa watoto wetu hasa wa kike na wa kiume pia tuziangalieni... muda umefika tuwalee watoto wetu katika misingi mizuri, lakini tusaidie waweze kufikia ndoto zao maana hizi ni zama za Sayansi na Teknolojia," amesema Rhobi. 

Aidha, Rhobi amepongeza juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika kuwainua wanawake ikiwemo kuwateua kuhudumu katika Wizara, Mashirika ya Umma, na nafasi mbalimbali serikalini na kwamba wamezidi kuonesha umahiri na weledi katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo kwa ufanisi mkubwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news