SERIKALI KUAJIRI ASKARI 600 KUKABILIANA NA WANYAMA WAKALI NA WAHARIBIFU

NA HAPPINESS SHAYO-WMU

SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeomba kibali cha kuajiri askari wa uhifadhi wapya 600 ambao watasambazwa kwenye maeneo hatarishi ili kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum, Mhe. Jacqeline Ngonyani Msongozi, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuwadhibiti tembo wanaovamia, kuharibu mazao na kujeruhi wananchi katika kata za Mindu, Kalulu na Tinginya, Wilaya ya Tunduru.

Mhe. Masanja ameongeza kuwa Wizara ina mkakati wa kuanzisha vituo vya kikanda vya Askari katika maeneo yenye changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu.

Pia, amesema Serikali itatoa mafunzo kwa askari wa wanyamapori wa vijiji; na kuelimisha wananchi kuhusu namna bora ya kupunguza athari zinazotokana na wanyamapori wakali na waharibifu.

Katika hatua nyingine, akijibu swali kuhusu mikakati ya Serikali ya kutangaza maporomoko ya Kalambo Mhe. Masanja amefafanua kuwa Wizara itatumia vyombo vya habari, itaandaa machapisho na majarida na kushiriki katika maonesho, matamasha, matukio na makongamano ya utalii na biashara yanayofanyika ndani na nje ya nchi ili kutangaza kivutio hicho.

Pia amesema njia ya kuweka mabango katika viwanja vya ndege ikiwemo uwanja vya ndege wa Songwe na maeneo mengine katika Mkoa wa Rukwa itatumika kutangaza utalii huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news