Serikali yakoleza kasi ya Mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilishwa Ardhi nchini

NA ANTHONY ISHENGOMA-WANMM

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula amezitaka halmashauri zinazonufaika na mkopo wa Mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilishwa ardhi kuzingatia masharti ya mkataba wa mikopo hiyo ili iweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa. 
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akiongea na wajumbe waliofika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dodoma jana kushuhudia utiaji sahihi Mikataba ya Mkopo wa program ya Kupanga , Kupima na Kumilikisha Ardhi kwa Halmashauri za Chamwino, Kigamboni, Kishapu na Manispaa ya Lindi.

Akiongea katika zoezi la utiaji sahihi wa mkopo wenye thamani ya shilingi Bilioni 4.1 uliotelewa kwa halmashauri nne za Chamwino, Kigamboni, Kishapu na Manispaa ya Lindi, hafla iliyofanyika jijini Dodoma, Dkt.Mabula alionya kuwa mabadiliko yoyote ya matumizi ya fedha au eneo la mradi yasifanyike kabla ya kupata idhini ya Wizara yake. 

Agizo hili linakuja kufuatia baadhi ya halmashauri ambazo tayari ni wanufaika wa mikopo ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kubadili matumizi ya fedha za miradi hii kinyume na mikataba na kushindwa kurejesha fedha ili Halmashauri nyingine ziweze kuendelea kutenga na kupima ardhi kwa wananchi. 
Baadhi ya wajumbe wa Halmashauri walioshiriki utiaji sahihi wa Mradi wa Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wizara ya Ardhi, wa kwanza kushoto ni Dkt.Grace Magembe, Naibu Katibu Mkuu OR- TAMISEM I(Afya) akifuatiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Dkt.Allan Kijazi, katikati ni Waziri wa Ardhi Dkt.Angeline Mabula akifuatiwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Ridhiwani Kikwete na mwisho kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii, Bw. Ally Makoa. 

‘’Umepewa pesa kwa ajili ya kuendeleza ardhi sio umepewa fedha kwenda kuwekeza katika maeneo mengine ukiweza kuzitumia kama ilivyokusudiwa zitatusaidia kujua namna bora ya kuendelea na zoezi hili kwa manufaa makubwa,’’aliongeza Dkt. Mabula.      

Waziri Mabula ametoa kipindi cha Mwezi mmoja kwa Halmshauri zote zilizokopa fedha za kwa ajili ya mpango wa kupima, kupanga na kumilikisha ardhi kurejesha fedha hizo na ikiwa zitashindwa kurejesha fedha izo atiomba TAMISEMI kuingilia kati ili fedha hizo ziweze kurejeshwa na kutumika kama ilivyokusudiwa. 

Waziri Mabula aliongeza kuwa fedha za mikopo hiyo zinatakiwa kuanza kurejeshwa kwa kipindi cha miezi sita tangu mikopo hiyo kutolewa na kuonya kuwa kwa siku za usoni Wizara yake haitatoa mkopo kwa Halmashauri ambazo katika bajeti yake hazitatenga fedha kwa ajili ya kupanga na kupima na kumilikisha ardhi kwani kila Halmashauri inatakiwa kutenga 60% katika bajeti kwa ajili kuendeleza ardhi. 

Aidha, Waziri huyo alizitaka Halmashauri kutoa vifaa vya kutendea kazi kwa kwa Ofisi za Ardhi badala ya kusubiri Wizara ya ardhi kwani wanasahau kuwa wao pia ni mamlaka za upangaji hivyo kuwataka kuboresha ofisi za ardhi ili kutatua changamoto zilizopo. 
Naye Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete akiongea na wajumbe wa walioshiriki katika hafla hiyo fupi aliwakumbusha wajibu wao wa kurejesha fedha hizo ili hamshauri nyingine ziweze kunufaika na hatimaye nchi nzima iweze kupanga matumizi bora ya ardhi. 

Aidha Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa baada ya kukamilika kwa bunge la bajeti anatarajia kufanya ziara katika mikoa mbalimbali na majukumu yake itakuwa ni kutembelea miradi ambayo zoezi la kupanga, kupima na kumilikisha ardhi linaendelea. 

Wakati huohuo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Mbunge wa Kondoa Ally Makoa alisema zipo Halmashauri zimepima lakini zikashindwa kuweka miundombinu rafiki na hivyo maeneo hayo kugeuka vichaka na kuongeza kuwa walibaini hayo wakati kamati yake ilipotembelea baadhi ya Halmashauri na kujionea changamoto hiyo. 
Baadhi ya wajumbe wa halmashauri walioshiriki utiaji sahihi wa Mradi wa Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wizara ya Ardhi, wa kwanza kushoto ni Dkt. Grace Magembe Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI (Afya) akifuatiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Dkt. Allan Kijazi, katikati ni Waziri wa Ardhi, Dkt.Angeline Mabula akifuatiwa na Naibu Waziri wa Ardhi Ridhiwani Kikwete na mwisho kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii Bw. Ally Makoa. (Picha na WANMM). 

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Allan Kijazi alisema tukio la utiaji sahihi mikataba hiyo ni mwendelezo wa awamu ya kwanza ambapo tayari kiasi cha Bil.42.3 kishatolewa kwa Halmashauri takribani 85 ikiwemo chuo cha ardhi Tabora na Morogoro kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kupanga na kumilikisha ardhi.

Post a Comment

0 Comments