Shehena ya dawa za kuongeza nguvu za kiume, kutoa mimba yanaswa Dar

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imekamata vifaa tiba na dawa zenye thamani ya shilingi milioni 294,486,590 ambazo hazijasajiliwa zilizohifadhiwa kwenye ghala bubu lililopo eneo la Mtaa wa Kitumbini katika Kata ya Mchafukoge katikakati ya Jiji la Dar es Salaam.

Sehemu ya dawa zilizokamatwa na TMDA.

Dawa zilizokamatwa katika shehena hiyo ni pamoja na zile za kuongeza nguvu za kiume, zinazotoa mimba, kutibu shinikizo la damu na nyinginezo.

Shehena hiyo imekamatwa Juni 28, 2022 kufuatia ukaguzi maalum unaoendelea kufanyika katika Kanda ya Mashariki.

Meneja wa Kanda wa TMDA, Adonis Bitegeko amesema, timu imefanya ukaguzi maalum katika ghala bubu kufuatia taarifa za kiinteligensia zilizofuatiliwa kwa muda mrefu.

“Katika ukaguzi tuliofanya tumebaini ghala hili linalomilikiwa na Mtanzania mwenye asili ya India, Ramaiya Rijendra, limehifadhi dawa mbalimbali za binadamu ambazo hazijasajiliwa kwa hiyo ubora, usalama na ufanisi wake haujulikani,”amesema.

Bitegeko amesema baada ya kukamata shehena hiyo, hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuziondoa dawa hizo baada ya kuziorodhesha.

Ameongeza kuwa, hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kuwatoza faini isiyopungua shilingi milioni 85 na kuziteketeza kwa gharama zao.

Post a Comment

0 Comments