TCRA yawapa neno wanahabari 'Online Media'

NA SHEILA KATIKULA

WAMILIKI wa vyombo vya habari katika mitandao ya kijamii nchini wametakiwa kuandika habari zenye ukweli na uhalisia.
Rai hiyo imetolewa leo Juni 9,2022 na Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Kanda ya Ziwa (TCRA),Mhandisi Francis  Mihayo wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Shirika la Internews kwa kushirikiana Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC). 

Mhandisi Mihayo amesema, inasikitisha kuona baadhi ya mitandao ya kijamii huweka kichwa cha habari ambacho hakiendani na habari iliyopo ndani ya taarifa hiyo.

"Sekta ya habari imezidi kupamba moto hasa kwa waandishi wa habari za mtandaoni kitendo ambacho kinapelekea wengi kudumbukia kwenye mitego ya uandishi wa upotoshaji, ni vema tujiepushe na suala la kutoa taarifa ambazo si sahihi.
"Mimi kuna siku nilimpigia mwandishi mmoja baada ya kuona alichokiandika kwenye kichwa cha habari hakiendani na kilichopo ndani akanijibu kuwa anatafuta watazamaji,"amesema Mhandisi Mihayo.

Mihayo amesema kuwa, baada ya Serikali kufungulia uhuru wa vyombo vya habari waandishi wengine wanasajli TV zao na blogu kwa gharama nafuu ya shilingi 500,000 baada ya kupewa usajili hupelekea kuweka habari zisizo sahihi.

Hata hivyo, amewataka waandishi wa habari
kufuata sheria,weledi na maadili ya kazi zao pindi wanapoandika habari zao bila kupotosha jamii.

Naye Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Lucyphine Kilanga amesema, ni vema waandishi wa habari kuangalia uhalali wa kazi zao kabla ya kurusha mtandaoni.

Amesema,  ni vema kila mwandishi wa habari kujifunza kutumia lugha ya ukarimu wa maneno ya kuandika na si kutumika lugha ya mitaani ambazo si sahihi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko amesema, lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha waandishi wa habari kusoma maadili, uandishi,taratibu na Sheria ya Vyombo vya habari ya mwaka 2016.

Amesema, kila mtu anawajibu wa kufuata misingi ya kitaaluma na maudhui ya habari ya mwaka 2010 ya EPOCA ambayo yanamtaka mwandishi kuzingatia miiko ya uandishi.

"Nawaomba waandishi wa habari muandike habari sahihi ili wananchi waweze kupata taarifa zenye ukweli na muepuke kuandika habari za kupotosha jamii,"amesema Soko.

Kwa upande mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Rose Jacob amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza uelewa katika kuandika habari kwa kuzingatia maadili, sheria na kanunu.

"Sisi kama waandishi kuna muda tunajisahau, hivyo mafunzo haya yanatukumbusha kufuata kanuni na sheria wakati tunapoandika habari na kuachana na habari za upotoshaji,"amesema Rose.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news