VIDEO NA PICHA 15:NGOs za Kenya zawatibua Wamasai Tanzania, watinga ubalozini Dar

NA DIRAMAKINI

KUNDI kubwa la wananchi kutoka jamii ya wafugaji ya Wamasai limeandamana kwenda katika Ubalozi wa Jamhuri ya Kenya uliopo jijini Dar es Salaam kuiomba Serikali ya Kenya kuingilia kati upotoshaji wa zoezi linaloendelea la Loliondo na Ngorongoro mkoani Arusha unaodaiwa kufanywa na asasi za kiraia pamoja na wanaharakati waishio nchini humo 
Maandamano hayo ya amani huku wakiwa wameshikilia mabango yenye jumbe mbalimbali ya kulaani upotoshaji huo, yamefanyika hadi Ubalozi wa Kenya nchini Tanzania uliopo Osterbay jijini Dar es Salaam leo Juni 17,2022.

Wamasai hao wameiomba Serikali ya Kenya kuingilia kati upotoshaji huo ambao unalenga kudhoofisha uhamaji huo wa hiari kwa wananchi hao katika Wilaya ya Ngorongoro na Tarafa ya Loliondo wilayani humo katika Mkoa wa Arusha.

Aidha, wamesema upotoshaji huo umelenga kuichonganisha jamii ya Wamasai na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo kuzorotesha jitihada mbalimbali za makubaliano zilizofikiwa na pande zote mbili.
Hayo wameyaeleza kupitia barua ya pamoja iliyosainiwa na Katibu wa umoja wao anayetambulika kwa jina la Loishiye Lashilunye iliyosomwa na Kiongozi wa Msafara aliyejitambulisha kwa jina moja la Bw.Emmanuel.
Hatua hiyo inakuja baada ya zoezi la kuweka alama za mipaka katika eneo tengefu la hifadhi Loliondo pamoja na uhamaji wa wananchi wa Ngorongoro ambao licha ya Serikali kueleza uwepo wa makazi mapya katika katika Kijiji cha Msowero wilayani Handeni mkoani Tanga, kumetokea upotoshaji wa mara kwa mara unaolenga kukwamisha jitihada hizo.

Post a Comment

0 Comments