Wasomi makada wa CCM wamegewa siri

NA SHEILA KATIKULA

WAHITIMU wa vyuo na vyuo vikuu ambao ni makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wametakiwa kutumia taaluma zao walizozipata vyuoni kwa kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo nchini ili kuleta maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Wito huo umetolewa na Katibu wa Uchumi na Fedha ambaye pia ni mlezi vyuo na vyuo vikuu,Frank Hawasi wakati akizungumza na wahitimu 500 kwenye mahafali ya Kumi ya Seneti ya vyuo na vyuo vikuu yaliyofanyika jijini Mwanza.
Hawasi amesema, kila mhitimu ana wajibu wa kujitoa katika kufanya shughuli mbalimbali ili kuweza kuitendea haki elimu aliyoipata.

"Inasikitisha kuona mtu anaelimu na ujuzi lakini amekata tamaa tumieni taaluma mliyoipata kwa kufanya kazi ili kuleta maendeleo".Hata hivyo aliongeza kuwa serikali inawasomesha watu ili wawe viongozi bora wa chama na taifa.
"Nyinyi ni viongozi wajao ni vema mtumie elimu yenu kutangaza shughuli mbalimbali za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.

"Chama kimewandaa wanafunzi wa vyuo mbalimbali ambao wako ndani ya chama ili waje kuwa viongozi wajao watakaolitumiki taifa kwa masilahi ya maendeleo ya nchi,"amesema Hawasi.
Hata hivyo, amesema kila mtu ana wajibu kuwa mzalendo na kutetea uhai wa chama kwa kutangaza vivutio vilivyopo nchi na maendeleo yanayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Naye Katibu wa Seneti Idara ya Vyuo na Vyuo Vikuu, Salum Mtaturu amesema wameongeza idadi ya wanachana wa Chama Cha Mapinduzi kutoka 1400 na kufikia 2000 mpaka sasa.
"Tumeongeza wanachama kwenye vyuo mbalimbali na tumehakikisha vyuoni kunakuwa na utulivu kwani mkakati wa serikali ni kuona hakuna vurugu.

"Tunaomba tuwezeshwe kadi 3000 za Jumuiya ya Vijana kwani itasaidia kuongeza wanachama na kuleta maendeleo, tunaomba tupewe miradi ili isaidie ruzuku kwenye shughuli za seneti,"amesema Mtaturu.

Post a Comment

0 Comments