Watakatishaji hutafuna dola bilioni 350 kila mwaka Afrika, BoT yaandaa mfumo wa kisasa

NA GODFREY NNKO

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Prof.Florens Luoga amesema,hatua thabiti za kudhibiti utakatishaji fedha barani Afrika zinaendelea kuchukuliwa ili kuokoa zaidi ya dola bilioni 350 ambazo huwa zinapotea kila mwaka kutokana na matendo hayo haramu.

Kwa mujibu wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu nchini, utakasishaji wa fedha haramu ni shughuli au vitendo vyenye lengo la kuficha ukweli au asili ya fedha au mali iliyotokana na uhalifu.

"Tatizo la utakatishaji wa fedha limeathiri nchi nyingi za Afrika na Tanzania, kwa mwaka takribani dola bilioni 350 tunapoteza, lakini kama tungechukua hatua thabiti inamaana kingeshuka hadi kiasi kisichozidi dola bilioni 10;
Prof.Luoga ameyasema hayo leo Juni 23, 2022 kando ya Mkutano wa 10 wa Viongozi wa Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha Kanda ya Afrika (AfPI) uliofanyika jijini Arusha.

Mkutano huo wa kwanza wa ana kwa ana kufanyika tangu kuzuka kwa janga la UVIKO-19 umeandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Taasisi ya Huduma Jumuishi za Fedha (AFI).
"Hili suala limechukuliwa kwa umakini na nchi za Afrika, kuna timu inafanya kazi chini ya aliyekuwa Rais wa Afrika ya Kusini Thabo Mbeki, hivyo kuna uratibu unafanyika kupata hatua ambazo kila nchi itakuwa ikizichukua kudhibiti utakatishaji wa fedha, Tanzania tumeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha tunalimaliza tatizo hilo,"amesema Prof. Luoga.

Gharama

Akizungumzia kuhusu huduma za kifedha zinazotolewa nchini na taasisi za kifedha amesema, licha ya kuwa na gharama kubwa, bado Benki Kuu imeendelea na juhudi mbalimbali kuhakikisha haziwaumizi walaji au watumiaji.

"Hizi huduma bado ni ghali ni kweli, mpaka sasa bado ni ghali kwa mfano ukienda benki zimekuwa zinatoza riba ya juu kwa sababu ya gharama za upataji wa fedha za utoaji wa huduma za kifedha ambazo Benki Kuu ilichukua hatua ikasema hakuna benki inayoruhusiwa kuwa na gharama za uendeshaji zinazozidi asilimia 52 hadi 55 maana gharama za uendeshaji benki nyingine zilikuwa zimefikia asilimia 80,"amesema.

Prof. Luoga amesema, kwa hali hiyo gharama zote za uendeshaji walikuwa wanazipeleka kwa wateja wa mabenki. 

"Hivyo tumedhibiti na tumeelekeza benki ambazo hazishushi gharama za uendeshaji hazitaruhusiwa kutoa gawio.Tumetunga kanuni ambazo ukisoma utakuta mabenki hayaruhusiwi kutoza baadhi ya gharama ambazo huko nyuma zikikuwepo na zinafanya huduma ziwe ghali sana. Tumechukua hatua kuhakikisha kila benki inatoa ripoti kwa Benki Kuu karibuni kila wiki kueleza mwenendo wa riba, tunataka riba ishuke,"amesema Prof. Luoga.

Amesema, lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ambazo gharama zake zinafaa, nafuu, rahisi na za haraka popote pale nchini.

"Pia kuna hatua nyingine ambazo tunazichuka ambazo zilikuwa zinapelekea kuwa na gharama kubwa kwenye mabenki ambazo sasa hivi tunadhibiti,hata kwa upande wa huduma jumuishi unatumia simu yako unatuma pesa na unayemtumia wote mnalipa gharama matokeo yake hiyo huduma inakuwa ghali sana.

Mfumo

"Benki Kuu tumechukua hatua ya kutengeneza mfumo, ambao tayari tumekwisha anza kuwaingiza baadhi ya watoa huduma kwenye mfumo huo, sasa hivi ukitoa pesa Tigo-Pesa inapofika Vodacom kuna aggregator (mtu wa kati) tunataka kuondoa hao aggregators ili huduma za kifedha ziwe na bei ya chini sana nchini,"amesema Prof. Luoga.

"Hiyo ni system (mfumo) tunaweza kuidhibiti sisi wenyewe katika kuhakikisha kwamba huduma jumuishi zinakuwa affordable (kuhimilika) ama zinakuwa hazina gharama,"amesema Prof. Luoga.

Aidha, Prof. Luoga amekiri kuwa, huduma za kifedha vijijini bado ni changamoto, lakini jambo hilo linaendelea kupatiwa ufumbuzi ili wananchi wote wapate huduma hizo kwa urahisi na ufanisi unaotakiwa kwa kutotembea umbali wa zaidi ya kilomita 15.

"Bahati nzuri Serikali imefikisha nishati ya umeme mpaka vijijini na pia imeondoa tozo kwenye 'smart phone' (simu janja) itasaidia wananchi vijijini kote na sisi kuboresha huduma za kifedha ziwe za ufanisi,"amesema Prof. Luoga.

Waziri 

Akifungua mkutano huo ambao umeshirikisha magavana, manaibu magavana, wakuu wa taasisi za udhibiti na usimamizi wa sekta ya fedha pamoja na watunga sera kutoka taasisi wanachama 32 kutoka nchi 30 kwa njia ya mtandao, Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Nchemba amesema, thamani ya miamala ya fedha kwa njia ya simu imechangia kuongezeka kwa pato la taifa kutoka asilimia 40 mwaka 2013 hadi asilimia 66 mwaka jana.

Amesema, hadi kufikia Desemba, mwaka jana watumiaji wa huduma za fedha kwa njia ya simu walifikia milioni 35.3, sawa na asilimia 61 ya watu wote nchini.

"Kuanzishwa kwa huduma hizi za kifedha kwa njia ya simu pamoja na huduma za benki kwa wakala na benki kwa njia ya simu kuliongeza upatikanaji wa huduma za kifedha nchini ikiwa ni pamoja na maeneo ya vijijini,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwingulu.

Post a Comment

0 Comments